Wednesday, 15 June 2016

PROFESA LIPUMBA APINGWA KILA KONA

UAMUZI wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, kurejea ndani ya chama hicho, umepingwa kila kona huku kigogo mmoja wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), akiweka wazi msimamo wa umoja huo wa kutomuamini Lipumba kwa sababu ana maamuzi ya kitoto.

Aidha, Chama cha CHADEMA kimesisitiza kuwa, hakitomuamini Profesa Lipumba kurejea kwenye umoja huo, kwa sababu hakuna alichokifanya katika kipindi chote akiwa kiongozi wa CUF.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Naibu Mwenyekiti wa CUF (Bara), Profesa Jumbe Safari, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, kuhusu ombi la Profesa Lipumba, kutaka arejeshwe kwenye nafasi yake ya uenyekiti ndani ya CUF.

Profesa Safari alisema hawezi kumwamini Lipumba kwa kuwa sababu alizozitoa awali za kujiengua hazijabadilika.

“UKAWA imeisaidia CUF, hivyo mimi simuamini. Sababu zake zilizomuondosha hazijabadilika, kwani UKAWA bado ipo na (Edward) Lowassa anaweza kugombea tena urais. Je, atatoka tena? Huo ni utoto,” alisema Profesa Safari.

Aliongeza kuwa UKAWA imeisadia CUF na sio Lipumba, kwa sababu wakati akiwa mwenyekiti, hakuna lolote alilolifanya, hivyo hawezi kuaminika.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Benson Banna, alisema Lipumba alijiuzulu uongozi na sio uanachama,
hivyo kwa kutaka kurejea kwenye nafasi yake, anapaswa kuwaridhisha Watanzania kwa kueleza kama sababu alizozitaja wakati anajiuzulu  zipo au hazipo.

Alisema endapo Lipumba atazitaja sababu hizo, wananchi watamwelewa, lakini akishindwa kufanya hivyo, watahoji kwa sababu kiongozi anapaswa kuwa na msimamo na chama chake hata kama kikiwa kinapitia mitafaruku mbalimbali.

“Kiongozi anapaswa kuwa muaminifu kwenye chama chake katika mazingira ya mitafaruku au raha, hivyo ndivyo inaonyesha namna viongozi wa vyama vya siasa nchini wasivyozingatia misingi ya demokrasia,” alisema Profesa Banna.

KUNG’ANG’ANIA UONGOZI

Msomi huyo alisema Profesa Lipumba hakuzaliwa kuongoza CUF milele, amekuwa kwenye nafasi ya uenyekiti kwa muda mrefu, hivyo alihoji iwapo chama hicho kimekosa watu wenye uwezo wa kikiongoza.

Alibainisha kuwa kama angekuwa ametimiza wajibu wake kama kiongozi, angekwishawaandaa watu kukiongoza, lakini tatizo la baadhi ya viongozi wa kisiasa hawana demokrasia ya ukweli.

“Viongozi wetu wana uimra, wanaweza kugombania demokrasia nje, lakini kwa ndani, taasisi zao zinakosa demokrasia ya kweli,” alisema mhadhiri huyo.

Aidha, mmoja ya viongozi wa CUF, ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema dhumuni la Profesa Lipumba kurudi kwenye chama hicho ni kutaka kuwania nafasi ya uenyekiti.

Alisema hata wanachama wa CUF, waliokusanyika kwenye ofisi za chama hicho kumuunga mkono, walikuwa wamekodiwa kwa kulipwa fedha ili kumshangilia.

“Siamini kama kuna mwanachama atakayeweza kumpokea Lipumba.
Alituacha kwenye wakati mgumu na kwa kulitambua hilo, hata watu waliokuwa wakimshangilia walilipwa fedha,”alisema.

Kauli za wanasiasa na wasomi hao zimekuja siku chache baada ya Profesa Lipumba, kudai kuwa ameandika barua kwa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharrif Hamad, kuomba arejeshwe kwenye nafasi yake.

Alisema uamuzi huo ameufanya baada ya kuombwa na viongozi wa dini na wanachama wa CUF, kutokana na chama hicho kukosa muelekeo kwa upande wa Tanzania Bara, tangu ajitoe uenyekiti.

Aliongeza kuwa Maalim Seif ameshaipokea barua hiyo, lakini kwa mujibu wa sheria za CUF, hakuijibu mpaka utakapofanyika mkutano mkuu wa chama hicho Agosti, mwaka huu.

Profesa Lipumba alisema ametumia katiba ya chama hicho ibara ya 117, inavyoeleza namna ya viongozi wanavyoweza kujiuzulu kwenye wadhifa huo na  pia kutumia ibara hiyo katika kurudi kwenye wadhifa wake.

No comments:

Post a Comment