Wednesday, 15 June 2016

MREMA AWAZODOA WAPINZANI, AWATAKA WAMWACHE RAIS MAGUFULI AFANYEKAZI


MWANASIASA mkongwe nchini na Naibu Waziri Mkuu mstaafu, Augustine Mrema, amewataka wapinzani kumwacha Rais Dk. John Magufuli afanyekazi yake kwa kuwa amechaguliwa kihalali na bado hajamaliza hata kipindi cha kwanza cha uongozi wake.

Amewatahadharisha wananchi kuwa makini na wanasiasa kwa kuwa wapo baadhi wasio na nia njema na nchi, badala yake wamekuwa wakipigania maslahi yao binafsi, hata kama nchi inaweza kuingia kwenye majanga.

Pia, amevitaka vyombo vinavyohusika na uratibu wa mambo ya siasa nchini, hususani Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kuwatazama kwa macho mawili viongozi wa dini wanaotumia nyumba za ibada kuwa majukwaa ya kisiasa, huku wakiwayumbisha wananchi kwenye haki yao ya msingi ya kuchagua viongozi wanaowataka.

Aidha, amezitaja sababu zilizomfanya ashindwe kulichukua jimbo la Vunjo, katika uchaguzi mkuu mwaka jana, kuwa ni pamoja na kitendo cha Rais Magufuli kumpigia debe jimboni humo, hali iliyosababisha wapinzani wamwonee donge na kupanga mikakati ya kuhakikisha halipati.

"Nawashangaa wapinzani wenzangu, hawajui kuwa Rais Dk. Magufuli anathamini zaidi mchango wangu nilioutoa nilipokuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri Mambo ya Ndani ya Nchi, jinsi nilivyokuwa nafanya kazi kwa nguvu moja kwa ajili ya kuliletea taifa maendeleo,"alisema.

Mrema alisema hayo jana, alipozungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam, kuhusu hali ya kisiasa nchini.

Alisema analaani kitendo cha wapinzani kudai kuwa Rais Magufuli hawatendei haki wananchi, anavunja sheria, katiba na anakiuka haki za binadamu na kuua demokrasia ya nchi.

Mrema alisema hivi sasa kumeibuka vuguvugu la kisiasa, hususan kwa wapinzani, kutangaza kuwa serikali ya awamu ya tano chini ya Dk. Magufuli, inakiuka haki za binadamu na kuponda demokrasia, jambo ambalo si la kweli.

Alisema wapo wanasiasa wanaodai Rais Magufuli hawatendei haki wananchi, anavunja sheria na kukiuka haki za binadamu, wao ndio
vinara wakuu wa kukiuka haki hizo.

"Wapinzani wenzangu ndio vinara na waliokubuhu na vitendo vya kuharibu demokrasia nchini na kuwapotosha wananchi,"alisema.

Aliongeza kuwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana, Mbunge wa Vunjo, James Mbatia alikiuka sheria na maadili ya uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani wa mwaka 2015.

Alisema NEC na taasisi zingine zinazosimamia shughuli za kisiasa nchini, zinapaswa kuwa makini na baadhi ya viongozi wa dini, ambao wameacha jukumu lao kuu la kuwajenga kiroho waumini wao na kutumia vyombo vya dini kama kinga yao kwenye siasa.

"Wakati wa harakati za uchaguzi mkuu wa mwaka jana, wapo viongozi wa dini waliosimama kwenye nyumba za ibada na kuwahubiria wafuasi wao kwamba, mwaka huu rais lazima atoke kanda ya kaskazini. Maneno hayo hayapaswi kuachwa yaendelee kwa kuwa ni hatari kwa mustakabali wa siasa na maendeleo ya demokrasi hapa nchini,"alisema.

Aliwataka wananchi wawe makini kwa sababu sio kila mwanasiasa anayekuja mbele yao anakuwa na nia njema na taifa hili, wengine lengo lao ni kutaka nchi iingie kwenye matatizo ili wanufaike.

Mrema alisema ana hakika endapo Rais Magufuli atakabidhiwa uenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM, atamtafutia nafasi ya kumsaidia kusukuma mbele maendeleo ya Tanzania.

No comments:

Post a Comment