Wednesday, 15 June 2016

MKAPA:FANYENI KAZI, ACHENI KUILAUMU SERIKALI

RAIS mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, amewataka Watanzania kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano kwa kufanyakazi kwa bidii  na kupunguza lawama.

Amesema ni kwa kufanya hivyo, Watanzania watakuwa wakionyesha kwa vitendo uzalendo ulioachwa na  Baba wa Taifa  Hayati  Mwalimu Julius Nyerere.

Mkapa alisema hayo jana, katika mkutano wa nane wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere, uliofanyika kwenye ukumbi wa Nkrumah wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Alisema Watanzania wengi wamekuwa na desturi ya kutumia muda mwingi kuilaumu serikali badala ya kufanyakazi kwa maendeleo ya nchi.

“Watanzania tunatakiwa tufanye kazi kwa bidii ili tuifikishe nchi yetu kwenye maendeleo na sio kutumia muda mwingi kuilaumu serikali, ” alisisitiza Mkapa.

Rais huyo mstaafu alisema ili uzalendo uwepo, Watanzania wanatakiwa
kutumia vizuri uhuru wa kuzungumza, kujadili  masuala yanayoleta maendeleo na sio kuleta uchochezi na kusababisha uvunjifu wa amani, iliyoasisiwa na Mwalimu Nyerere.

Alisema Tanzania itaendelezwa na Watanzania wenyewe na si taifa lolote la nje, na kwamba hata kama watakuja wawekezaji, lazima yafanyike makubaliano juu ya pande zote mbili kuhusu zitakavyonufaika.

"Inapaswa kukaa na kujadili na wenye nia ya kuwekeza nchini ili kukubaliana katika uwekezaji watakaoufanya, wao watanufaika vipi na sisi tutanufaikaje," alisisitiza.

Mkapa alisema hayupo tayari kuzungumzia suala la kusimama kwa mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya, badala yake alitaka ufanyike utafiti ni kwa nini ulisimama.

"Baada ya kupatikana kwa matokeo ya  utafiti huo, ndipo sasa ifanyike mijadala ya kuzungumzia suala hilo, badala ya kuzungumza juu juu tu," alisema.

Aidha, alisisitiza kuwa taifa linapaswa kufuata nyayo za Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, ambaye alipinga rushwa na kuhamasisha demokrasia, ambapo alikuwa mstari wa mbele katika utekelezaji wake.

"Yeye mwenyewe alikuwa mstari wa mbele kutekeleza aliyoyazungumza na kuhamasisha. Mfano katika kupigana vita na nduli Iddi Amin wa Uganda," alisema.

Alizitaja sifa za kiongozi kuwa ni lazima awe na muda wa kusikiliza maoni ya wengine, ndipo ashauri juu ya mambo husika ama kuchukua hatua.

"Baba wa Taifa alikuwa akisikiliza watu na kuangalia changamoto ili kuona namna ya kukabiliana nazo na kupiga hatua," alisema.

Alisema ni muhimu nchi kujifunza kutoka kwa wengine kwa kuangalia ni wapi walianguka na wakainukaje ili iweze kusonga mbele.

"Ni muhimu kujitazama tuko wapi ili kuona namna tunavyoweza kujikwamua kutokanaa na kujifunza kwa wengine walioshindwa, lakini baadaye wakainuka," alisema.

Katika mkutano huo, Mkapa pia alizindua kitabu cha uchumi wa kisiasa wa madiliko ya Tanzania, kinachojulikana kwa jina la Political Economy of Change in Tanzania, ambacho kina lengo la kukuza uchumi na siasa nchini. 

Mkutano huo wenye lengo la kudumisha uzalendo na kukuza uchumi, ulihudhuriwa na wawakilishi mbalimbali wa kitaifa na kimataifa, wakiwemo baadhi ya mabalozi na wanazuoni kutoka ndani na nje ya nchi.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha  Dar es Salaam,  Profesa Rwekaza Mukandala, alisema mkutano huo unalenga kudumisha na kuendeleza yaliyoachwa na Mwalimu Nyerere.

Aliwataka Watanzania kumuenzi Baba wa Taifa kwa kufanyakazi kwa bidii ili kujikwamua kiuchumi na kuendeleza ujamaa aliouacha.

No comments:

Post a Comment