Monday, 6 June 2016
MKENYA KORTINI KWA WIZI WA MIL. 800/-
MENEJA Mwendeshaji Biashara, Stanley Mwaura (38), raia wa Kenya, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na mashitaka 58, yakiwemo ya kughushi hundi mbalimbali na kujipatia zaidi ya sh. milioni 800, kwa njia ya udanganyifu kutoka Benki ya Azania.
Mwaura, alipandishwa kizimbani mahakamani hapo jana, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi na kusomewa mashitaka hayo na Wakili wa Serikali, Simon Wankyo.
Wakili Wankyo alimsomea mshitakiwa huyo mashitaka 28 ya kughushi hundi na mengine 28 ya kuwasilisha hundi hizo za uongo katika Benki ya Azania.
Pia, alimsomea mashitaka ya kujipatia sh. 805,358,880, kwa njia ya udanganyifu kutoka Benki ya Azania na kutakatisha fedha hizo wakati akijua kwamba ni zao la uhalifu wa kosa la kughushi.
Wankyo alidai mshitakiwa huyo alitenda makosa hayo kati ya Januari 5, mwaka jana hadi Mei 31, mwaka huu, jijini Dar es Salaam.
Katika makosa ya kughushi, mshitakiwa huyo anadaiwa katika tarehe tofauti jijini Dar es Salaam, alighushi hundi zenye namba mbalimbali na zenye thamani tofauti, akidai kwamba zimetiwa saini na Ahmad Zacharia na Vida Zacharia.
Pia, katika makosa ya kuwasilisha nyaraka za uongo, mshitakiwa huyo anadaiwa kuyatenda tarehe tofauti Dar es Salaam, ambapo aliziwasilisha hundi hizo za kughushi katika Benki ya Azania.
Katika shitaka la 57, la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, mshitakiwa huyo anadaiwa tarehe tofauti kati ya Januari 5, mwaka jana na Mei 31, mwaka huu, Dar es Salaam, kwa njia ya udanganyifu alijipatia kiasi hicho cha fedha kutoka Benki ya Azania.
Wakili Wankyo alidai mshitakiwa huyo alijipatia fedha hizo baada ya kudanganya kwamba, zilikuwa ni malipo halali kutoka Kampuni ya Professional Paint Centre Limited kwenda Stano Enterprises kwa ajili ya kusambaza kazi.
Katika shitaka la 58, la kutakatisha fedha, mshitakiwa huyo anadaiwa katika kipindi hicho jijini Dar es Salaam, alijipatia fedha hizo kupitia akaunti inayoendeshwa na Kampuni ya Professional Paint Centre Limited, iliyoko katika Benki ya Azania wakati akifahamu fedha hizo zilipatikana kwa kosa la kughushi.
Mshitakiwa alikana mashitaka hayo, ambapo Wakili Wankyo alidai upelelezi haujakamilika na kuomba shauri hilo liahirishwe hadi tarehe nyingine kwa kutajwa.
Hakimu Shaidi aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 20, mwaka huu na kusema mshitakiwa ataendelea kuwa mahabusu. Mshitakiwa huyo ataendelea kuwa mahabusu kwa kuwa shitaka la kutakatisha fedha halina dhamana kwa mujibu wa sheria.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment