Monday, 6 June 2016

WATUMISHI 12 WATUMBULIWA MAJIPU SIKONGE



WATUMISHI 12 katika Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora, akiwemo Mweka Hazina, Evans Shemdoe, wamesimamishwa kazi kwa tuhuma mbalimbali, ikiwemo uzembe, matumizi mabaya ya madaraka na ubadhirifu wa fedha za serikali.

Uamuzi huo umetolewa katika kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo kilichoketi juzi, wilayani humo, kikiwa na ajenda moja ya kujadili hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG), baada ya halmashauri kupata hati yenye mashaka.

Akitangaza uamuzi wa kikao hicho, kilichomshirikisha Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Peter Nzalalila, alisema baraza limelazimika kuchukua hatua hiyo ili kupisha uchunguzi kutokana na tuhuma zinazowakabili, ambazo zimesababisha halmashauri hiyo kupata hati yenye mashaka.

Aliwataja watumishi waliosimamishwa kuwa ni Evance Shimdoe, ambaye ni Mweka Hazina wa halmashuri ya wilaya hiyo na Richard Ndalo, ambaye ni Mhasibu wa halmashauri, ambao wanatuhumiwa kwa kushindwa kuwachukulia hatua watendaji hao wa kata kwa kupoteza vitabu vya mapato.

Wengine ni Ofisa Utumishi wa halmashauri, Elly Aketch, Mganga Mkuu Mfawidhi wa Zahanati ya Kitunda, Fredrick Mtao, Mtendaji wa Kata ya
Kitunda, Ally Kicko, Mtendaji wa Kata ya Kipanga, Emmanuel Kalumay, Ofisa Mipango Miji wa halmashauri, Emmanuel Magembe na Ofisa Sheria wa halmashauri, Rebecca Liyanga ambao licha ya kusimamishwa, wanafanyiwa uchunguzi.

Watendaji kata watano waliosimamishwa kwa tuhuma za upotevu wa vitabu vya kukusanyia mapato ya halmashauri ni Rehema Raymond, Godfrey Sungura , George Mlimanzi, Matha Masanja na Waziri Juma, ambao wanatakiwa kujibu tuhuma zinazowakabili katika vyombo vya dola.

Nzalalila alimwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa halmashuri hiyo, Philemon Magesa, kuchukua hatua mara moja na kuwaandikia barua ya kusimamishwa kazi watumishi hao na kuongeza kuwa, hawaruhusiwi kuingia katika ofisi walizokuwa wakitumikia mpaka uchunguzi utakapokamilika.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri alisema kutokana na taarifa iliyowasilishwa na CAG, ni dhahiri watumishi hao walishindwa kutimiza wajibu wao ipasavyo na kufanyakazi kwa mazoea na hiyo ndio sababu kubwa ya halmashauri kuwa na hoja nyingi zisizo na majibu.

Alisema suala la uzembe haliwezi kuvumilika hata kidogo, hivyo hatua zakinidhamu zitazidi kuchukuliwa  kwa watumishi wanaoshindwa kutimiza wajibu wao ili kulinda heshima ya serikali.

Alitoa rai kwa kila mkuu wa idara, kufanyakazi huku akiwataka madiwani kusaidia katika kuwawajibisha watumishi wasiokuwa na sifa za utumishi bora ili kuokoa upotevu wa fedha za umma kwa watu wa wachache wasiokuwa waaminifu mahali pa kazi.

Mkuu wa Wilaya ya Sikonge, Hanifa Selengu alipongeza hatua iliyochukuliwa na RC Mwanri ya kuhakikisha mkoa wa Tabora unakuwa na watumishi wawajibikaji, kwani itasaidia kurejesha nidhamu kazini
sambamba na kuinua uchumi wa mkoa.

Alisema kwa kasi hii, mkoa wa Tabora na wilaya zake zote zitakuwa na watumishi bora kama mkuu  huyo ataendelea kushirikiana na madiwani katika halmashauri zote.

Hanifa alisema hatua za kuwasimamisha kazi watumishi hao ni kuunga mkono jitihada za Rais Dk. John Magufuli, kudhibiti vitendo vya uzembe kazini na kuhakikisha kila mtumishi wa halmashauri anafanya kazi kwa juhudi na maarifa na kuondokana na tabia ya mazoea.

No comments:

Post a Comment