Monday, 6 June 2016
MAREKANI KUIPATIA TANZANIA TRILIONI 1.752/-
MAREKANI imeahidi kutoa Dola milioni 800 (takriban sh. trilioni 1.752) kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini.
Balozi wa Marekani nchini, Mark Childress, amesema hatua hiyo ni uthibitisho kuwa, kutotolewa kwa fedha za awamu ya pili ya Mradi wa Changamoto za Milenia (MCC-2), hakujaondoa uhusiano na ushirikiano wa Tanzania na nchi yake, ikiwemo utoaji wa misaada ya maendeleo.
Kwa mujibu wa balozi huyo, aliyekutana na kuzungumza na Rais Dk. John Magufuli, wanatarajia kutiliana saini mkataba wa Dola milioni 400 katika mwaka ujao.
"Tumezungumza mambo mbalimbali na wiki hii Tanzania na Marekani kupitia Shirika la Misaada Marekani (USAID), tunatarajia kutiliana saini mkataba wa zaidi ya dola milioni 400, kwa ajili ya mwaka ujao. Pia tumezungumza kuwa kutakuwa na Dola milioni 800, zitakazotolewa na Marekani kwa ajili ya miradi mbalimbali na hii haihusiani na MCC.
"Ukweli ni kwamba tunayo mengi ya kufanya pamoja katika sekta mbalimbali, zikiwemo afya, elimu na kilimo na tutafanya kila juhudi kuhakikisha haya yanafanikiwa," alisema Balozi Childress, muda mfupi baada ya kumaliza mazungumzo na Rais Magufuli.
Kwa upande wake, Rais Magufuli alisema serikali yake itaendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano na Marekani na kwamba, fedha za msaada kutoka nchi hiyo ni muhimu kwa maendeleo ya Tanzania.
"Amekuja kutuhakikishia kwamba, watatoa fedha kwa ajili ya Tanzania na amesema sasa hivi watatoa zaidi ya Dola milioni 800 na mkataba mwingine tunaweza kutia saini hata kesho, ambao unahusisha Dola za Marekani milioni 410.
"Balozi ametueleza kwamba, kutotoa fedha za MCC, hakuna maana ya kupotea kwa urafiki wa Tanzania na Marekani, ambao upo pale pale na sasa wanaongeza fedha nyingi zaidi ili kuonyesha kwamba juhudi za HAPA KAZI TU zinaendelea," alisema Rais Magufuli.
Wakati huo huo, Dk. Magufuli amekutana na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ubelgiji, Didier Reynders, Ikulu, Dar es salaam na kuzungumzia kuendeleza na kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo mbili, hususani katika nyanja za maendeleo.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano, Ikulu, alisema viongozi hao pamoja na kuzungumzia miradi ya ushirikiano inayotekelezwa kati ya Tanzania na Ubelgiji katika mkoa wa Kigoma, pia wamekubaliana kuongeza ushirikiano kwenye biashara na uwekezaji.
Ilisema waziri huyo ameahidi kuzishawishi kampuni nyingi za Ubelgiji kuja kuwekeza hapa nchini.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli ameagana na Balozi wa Italia hapa nchini, Luigi Scotto, ambaye amemaliza muda wake wa utumishi wa miaka mitatu, alipokuwa akiiwakilisha nchi yake.
Balozi Luigi Scotto alisema katika kipindi chake, amewezesha kuongezeka kwa biashara kati ya Italia na Tanzania kwa asilimia 35 na ameielezea Tanzania kuwa ni nchi nzuri, aliyoipenda na kwamba ataendelea kutangaza fursa zilizopo hapa nchini atakaporudi Italia na kwingineko.
Mapema jana, Rais Magufuli alitia saini kitabu cha maombelezo katika Ofisi ya Ubalozi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Nchi za Kiarabu ya Saharawi, iliyoko Mikocheni, Dar es salaam, kutokana na kifo cha Rais wa nchi hiyo, Mohamed Abdelaziz, aliyefariki dunia Mei 31, mwaka huu.
Rais Magufuli, ambaye alipokelewa na Balozi wa Saharawi hapa nchini, Brahim Salem Buseif, alisema marehemu Mohamed Abdelaziz, ambaye pia alikuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Polisalio Front, atakumbukwa kwa juhudi zake za kupigania ukombozi na uhuru wa Saharawi.
"Kwa niaba ya serikali na wananchi wa Tanzania, napenda kutoa salamu za pole kwa serikali na wananchi wa Saharawi kwa kumpoteza kiongozi, ambaye alijitoa kwa ajili ya kupigania ukombozi na uhuru wa Jamhuri ya Saharawi.
"Namuombea kwa Mwenyezi Mungu, aipumzishe roho yake mahali pema peponi, Amina," alisema Dk. Magufuli katika salamu hizo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment