Monday, 6 June 2016

TUTAWAUMBUA


CHAMA Cha Mapinduzi (CCM),  kimeonya mkakati wa viongozi wa Umoja wa Vyama vya Upinzani (UKAWA), kufanya ziara nchi nzima kwa lengo la kuishitaki kwa wananchi serikali  ya awamu ya tano chini ya  Rais Dk. John Magufuli.

CCM imesema daima haitavumilia jambo lolote litakaloonekana kuwa na nia mbaya na kumchafua Rais Dk. Magufuli na kwamba, itakula sahani moja na UKAWA katika kampeni hiyo chafu.

Imesema inatambua hila zilizo nyuma ya mpango huo, ikiwa ni pamoja na kutumika kwa vigogo mbalimbali waliokuwa wakinufaika na miradi ya kiuchumi, ikiwemo uingizaji mafuta, ambao hivi sasa wamekabwa koo.

Chama kimesema  kinaandaa orodha ya vigogo  wanaopinga utendaji kazi wa serikali ya Rais Dk. Magufuli na kwamba, ikibidi itaiweka hadharani ili kila mtanzania awatambue.

Akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam, jana, Msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka, alisema wamesikitishwa  na kauli  zinazotolewa na  viongozi wa upinzani, kupinga kasi ya Rais Magufuli, hususan katika dhana yake ya utumbuaji majipu, kubana bajeti na matumizi ya serikali pamoja na kuzitafutia ufumbuzi  changamoto za wananchi katika sekta mbalimbali.

Sendeka alisema upo mkakati mchafu, ambao wapinzani wamekuwa wakiupanga  kwa nia mbaya ya kutaka kuchafua taswira ya Rais Dk. Magufuli, ambao amesema hauwezi kuungwa mkono na wananchi.

Alisema tangu Mei 16, mwaka huu, baada  ya kikao cha Kamati Kuu ya CHADEMA, habari za mwanzo zilianza kuandikwa katika vyombo mbalimbali vya habari juu ya yaliyojiri katika mkutano huo.

Sendeka alisema mkakati huo unaegemea katika kuuandaa umma kwa kile kinachoitwa kwenda kumshitaki Rais Dk. Magufuli kwa wananchi.

“Wanadai serikali ya  Rais Dk. Magufuli  inaendesha nchi kifashisti na inalenga kuipeleka nchi  katika utawala wa kidikteta, ambao haujazoeleka katika nchi yetu,”alisema Sendeka.

Alisema katika kipindi cha nyuma, moja ya mambo ambayo yalikuwa yakipigiwa kelele na vyama vyote ni ufisadi, rushwa  na  suala la  serikali kutokuwa na uamuzi na kwamba, baada ya uchaguzi  mkuu uliopita na Dk. Magufuli kuchaguliwa, amesimama kidete kupambana na mambo hayo kama ilivyoahidiwa kwenye Ilani ya uchaguzi.

“Wenzetu baada ya kumpata mgombea wao (Edward Lowassa), ujasiri wa kuzungumzia rushwa na ufisadi ulipungua. Kwa sababu ambazo  kila mtanzania anajua ni kwa nini wamekosa utashi wa kuendelea kulikemea suala la rushwa, ufisadi na ubadhirifu wa mali za umma,”alisema Sendeka.

Alisema baada ya Rais Dk. Magufuli kuingia Ikulu, mapambayo dhidi ya mambo hayo ameyafanya kwa kasi ya aina yake, ikiwa ni pamoja na kuziba mianya  ya rushwa, upotevu wa fedha za serikali, kubana matumizi kwa kufuta bajeti kubwa za sikukuu, kufuta safari za nje na wakati mwingine kuelekeza fedha katika maeneo  ambayo yana matatizo makubwa.

Alisema anachokifanya Rais Dk. Magufuli ni kumalizia ngwe ya mwisho ya bajeti ya mwaka wa fedha 2015/16 na kwamba, atafanya vizuri zaidi baada ya bajeti ya mwaka wa fedha 2016/17 kupitishwa.

“Katika  mapambano hayo,  ambayo  rais ameyafanya kwa utashi mkubwa,  tunajua kwamba yamegusa watu wengi. Hakuna mashaka kwamba katika nchi hii, tayari kuna watu ambao wametengeneza utajiri wa muda mfupi, ambao  unatia ukakasi  unaoweza kumuudhi yeyote mwenye mapenzi na nchi hii,”alisema.

Alisema utendaji huo ulifanya kutolewa kwa sifa nyingi zilizoelekezwa kwa Rais Magufuli kutokana na utendaji wake, lakini baada ya kikao cha Kamati Kuu ya CHADEMA,  walibaini wazi kwamba, anayoyafanya yanaipandisha chati ya CCM.

“Serikali  iliyopo madarakani isipotekeleza matarajio ya wananchi, uhalali wake haupo. Utendaji wa Rais Dk. Magufuli hauna mashaka kwamba Watanzania  wanaunga mkono na dunia imefanya hivyo.  Hata Umoja wa Mataifa kupitia Shirika lake la Maendeleo (UNDP), umeunga mkono uwajibikaji huo katika  mapambano dhidi ya rushwa, ukusanyaji mapato na nidhamu ya uwajibikaji kwa watumishi wa umma,”alisema Sendeka.

Aliongeza kuwa inashangaza kuona CHADEMA wanadai suala la kupambana na rushwa na ufisadi, Rais Dk. Magufuli amelipora kutoka kwao na kusahau kwamba, ajenda hiyo ilikuwa ni ya CCM tangu enzi ya TANU.

“Kilichofanyika ni kumpata kada, ambaye anaweza kusimamia na kutekeleza hayo, jambo ambalo limeanza kuwafanya wapinzani kuamini kwamba, upinzani utakufa na kwamba, hofu yao ni uwezekano wa kupoteza  wabunge wengi katika uchaguzi mkuu wa 2020,”alibainisha msemaji huyo.

Alisema baada ya kufanya tathimini hiyo, ndipo walipokubaliana kwenda kwa wananchi  wakiwa na ajenda  ya kupotosha umma juu ya utendaji  wa Rais Dk. Magufuli na serikali yake.

“Walianza na kampeni ya rais ya utumbuaji wa majipu na wao kupitia kwa mgombea wao wa urais, Lowassa kisha kwa mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, walikemea  ajenda hiyo kwamba ni ukiukaji wa haki za binadamu. Hivi unapokwenda bandarini na kukuta makontena 2,000 au 3,000 hayajalipiwa kodi, unamuacha huyo kamishna na wasaidizi wake? Hiyo ndiyo haki ya binadamu?” Alihoji Sendeka.

Alisema  viongozi hao pia waliponda kwamba serikali ya Rais Dk. Magufuli inatanguliza vitendo kuliko fikra.

“Hivi jamani, umemkuta mtu na kila  dalili za kufanya ufisadi, unamuacha na kuanza kufikiria jambo la kufanya? Serikali ya Magufuli inasema kaa pembeni, jitetee kisha hatua  zaidi zinachukuliwa. Hii ni kwa nia njema ya kuleta maendeleo ya nchi kwa kutumia  vyanzo vya mapato yetu na kutoa huduma muhimu zinazostahili kwa wananchi.
Na kazi hiyo ameifanya kwa ufanisi mkubwa kwa muda mfupi aliokaa katika uongozi,”alibainisha Sendeka.

Aliongeza: “Sasa haya yamewaudhi. Walijaribu kupima kina cha maji kwa mti, wamebaini kwamba hawayawezi na wamebaini kwamba watanzania wote wamechoka na wanaunga mkono hatua hizi za rais.”

Sendeka alieleza kushangazwa na wapinzani  kulalamikia hatua ya Rais Magafuli kutumbua majipu  kwa madai kwamba ni udikteta na ufashisti wakati rais ana nia njema ya kutetea wanyonge na maslahi mapana  ya taifa.

Alisema binafsi anamuunga mkono Lowassa kwa kauli yake aliyoitoa hivi karibuni  kwamba, kazi yake kubwa sasa  ni kuigeuza CHADEMA kutoka kuwa katika kikundi cha wanaharakati na kuwa chama kamili.

“Najiuliza kama miaka 20 zaidi ya uwepo  wa CHADEMA, hakikuweza kubadilika kutoka katika kikundi cha wanaharakati mpaka Lowassa alipokikuta na kutaka kukibadilisha ndani ya miaka minne ijayo kiweze kuwa chama kamili cha siasa, nina uhakika muda huo hautoshi,” alisema Sendeka.

"Lakini najiuliza kama  Rais Magufuli anatumbua majipu, wapinzani wanadai ni dikteta na fashisti. Magufuli  anaziba mianya ya rushwa   wanachukia. Najiuliza wametumwa na nani? Wanamwakilisha nani? Kutetea maslahi ya nani? Na nani kawafadhili?" Aliendelea kuhoji.

Alisema  ni dhahiri anayetetea ufisadi  anawasemea waliotumbuliwa na ambao mianya yao ya rushwa imezibwa.

“Wakati wa kashfa ya ukwepaji wa kodi ya sukari, hakuna aliyetoka kwenda kwa wananchi kuitisha mikutano au kuingia barabarani    kuandamana kwa sababu kodi haijalipwa. Wakati wa kashfa ya Escrow, hakuna chama kilichofunga safari kwenda mikoani kuitisha mikutano na kuwaeleza wananchi kwamba kuna ufisadi huo,”alisema Sendeka.

Alisema inashangaza kuona wakati serikali inajitahidi kupambana na changamoto  za wananchi,  wapinzani wanajipanga kwenda mikoani kupinga hatua hizo.

“Dhamira ya wenzetu sasa ni kujitahidi  kutumia nguvu zao na za wale  wanaowatuma kuchafua jina la Rais Magufuli bila kuelewa kwamba, Watanzania,  hasa wanyonge wataendelea  kutumia jina la Rais Magufuli kama alama kuu na muhimu katika mapambano dhidi ya ukiritimba, ufisadi wa viongozi  na watendaji wanaokubali kufanyakazi ya ukuwadi kwa manufaa  yao binafsi na kuyaweka pembeni maslahi ya taifa,”alionya Sendeka.

Alisema CCM haipingi  ziara hizo za viongozi, lakini  daima haitavumilia iwapo mikutano yao italenga kumchafua rais.

“Wakijaribu kumchafua rais, watakapokanyaga, nitakanyaga pia. Watakapoondoa  mguu wao, naweka mguu wangu ili kuwaeleza ukweli wananchi juu ya kazi kubwa inayofanywa na serikali. Tuna wasemaji wengi  na tuna uwezo wa kufika popote,”alionya Sendeka.

"Watanzania watapima kauli ya watu wanaotetea mafisadi, wakwepa kodi na wala rusahwa na CCM inayotetea wananchi wanyonge  ili waweze kufaidi matunda ya nchi yao,” alisema.

Aliongeza kuwa kama hoja zao ni  za kumchafua Rais Magufuli, CCM inawaonea huruma na wasifiriki Watanzania walio timamu kiakili watawaunga mkono.

“Siyo kwamba Watanzania hawatawaunga mkono, bali watawashangaa na heshima yao itashuka. Watanzania wana akili, hawawezi kutetea wezi wakati rais anafanyakazi nzuri ya kuwatetea,” alisisitiza.

No comments:

Post a Comment