Wednesday 3 August 2016

MSUKUMA ASEMA TANZANIA SIO SAWA NA KAMBALE




CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mkoani hapa, kimesema watu wanaotaka kuvuruga amani na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama, inayotekelezwa kwa kasi na Rais Dk. John Maguifuli, waache kwani Tanzania si sawa na samaki aina ya kambale.
Aidha, kimepongeza hotuba ya Rais Magufuli, aliyoitoa mkoani Singida, ambapo aliwataka viongozi wa CHADEMA, wasichochee vurugu kwa maandamano wanayokusudia kuyafanya nchi nzima.
Mwenyekiti wa CCM mkoani Geita, Joseph Kasheku ‘Msukuma’, alisema hayo juzi, wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa Rais Magufuli, uliofanyika kwenye uwanja wa Kalangalala.
“Tunakupongeza Rais Magufuli kwa hotuba mzuri uliyoitoa mkoani Singida, ulisema rais hajaribiwi, hivyo Tanzania sio sawa na kaya ya kambale, ambayo kila mmoja ana sharubu,” alisema.
Alisema vyama vya upinzani vina hali mbaya baada ya kuona kasi ya utendaji inayofanywa na Rais Magufuli na ndio maana viongozi wakuu wa vyama hivyo wanataka kuchochea vurugu.
Msukuma, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Geita Vijijini, alimuomba Rais Magufuli awaruhusu wananchi wapewe Magwangara.
Aidha, alimchongea Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Salama Geita (GEUWASA) na Mgodi wa GGM kwa Rais Magufuli kwamba, hana uwezo na utendaji wake ni mdogo.
 “Mheshimiwa Rais Mkurugenzi wa GEUWASA hana uwezo wa kazi, ni tatizo muondoe. Maji hakuna, tunalipa bili hewa, mgodi wa GGM (Geita Gold Mine) umetuletea ambulance (gari la wagonjwa), tunaomba na dawa, wamehodhi maeneo ya watu kwa  bikoni, wayaachie au wawalipe fidia haraka,” alisema.

No comments:

Post a Comment