MWENYEKITI wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dk. John Magufuli, amesema licha ya wapinzani
wachache kutaka kukwamisha utendaji wake wa kazi na utekelezaji wa Ilani ya
Chama, CCM itaendelea kutawala Tanzania.
Amesema uwezo inao wa
kutawala milele, inakubalika kwa wananchi na kuwaomba wanachama wapya anaowaita
ng’ombe waliokatika ‘mikia’, wanaotaka kurudi zizini la CCM mkoani Geita,
wamsubiri atakapofanya ziara ya kichama.
Rais Magufuli alisema
hayo juzi, kwenye uwanja wa Kalangalala, wakati akihutubia maelfu ya wananchi
waliofika kumlaki na kumsikiliza alipokuwa akitokea mkoani Shinyanga.
“Wana-CCM wote waliopo
hapa na wengine wote, nawashukuru kwa kunichagua, niko pamoja nanyi na
sitowaangusha. Changamoto zilizoko kwenye Chama tutazishughulikia na kuzitatua
pamoja,” alisema na kushangiliwa.
Aliamsha tena shangwe
alipovikejeli vyama vya upinzani, kikiwemo kinachopanga kufanya vurugu kwa
kuandamana, akisema: “CCM itaendelea kutawala milele, uwezo inao na inakubalika
kwa wananchi.
Wale wasio na mikia,
wanaotaka kuhamia na kurudi tena CCM, wasubiri nikija nimevaa kijani.”
Mwenyekiti huyo mpya
wa CCM alisema hayo kufuatia sauti za baadhi ya wananchi waliokuwa wakidai
wanataka kurudisha kadi za vyama uchwara ili wachape kazi, baada ya kuruhusiwa
kupatiwa mawe yenye mabaki ya dhahabu, maarufu kwa jina la ‘Magwangala’.
Ahadi ya kujenga
kilometa 10 za lami Geita iko
palepale
RAIS Dk. John Magufuli
amesema serikali itajenga barabara yenye
urefu wa kilometa 10 za lami katika mkoa wa Geita, ikiwa ni moja ya utekelezaji
wa ahadi alizozitoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka jana, kwa
wananchi wa mkoa huo.
Aidha, amesema barabara
ya Kahama- Geita, ambayo upembuzi yakinifu na usanifu umekamilika, nayo
itajengwa kwa kiwango cha lami.
Rais Magufuli alisema
hayo juzi, mjini hapa, wakati akihutubia maelfu ya wananchi wa Geita katika uwanja
wa Kalangalala.
Aliwataka wananchi wasing’ang’anie
matuta ya barabarani na kudhani ndiyo suluhisho la mwisho la ajali za
barabarani.
“Kilometa kumi za lami
nilizoahidi, tutazijenga. Mheshimiwa Kanyasu na wenzake wakae wapendekeze
zijengwe wapi, lakini wananchi msing’ang’anie matuta, hatuwezi kujenga barabara
ikajaa matuta, ingekuwa hivyo gari zingekuwa zinapita hata kwenye matuta ya
viazi,” alisema.
Alisema waendesha
pikipiki (bodaboda) ni moja ya chanzo cha ajali, wakigongwa au kugonga wanasema
‘weka matuta’, hivyo ni vyema kila
mtumiaji wa barabara akatimiza wajibu wake kwa kufuata sheria za barabarani.
“Barabara nyingine ya
Kahama-Geita, upembuzi wake umekamilika na tumetenga shilingi milioni 400, kwa
ajili ya ujenzi wa barabara hiyo,” alisema.
Hata hivyo, alisema
barabara zilizoahidiwa kupandishwa hadhi zitapandishwa, ambapo aliwaomba
wananchi waendelee kumuamini kwani atasimamia vyema Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
Rais Magufuli alilipongeza
Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani kwa kudhibiti ajali nyingi,
kupambana na vitendo mbalimbali pamoja na kudhibiti matukio ya uhalifu.
Awali, mbunge wa Jimbo
la Geita Mjini, Costantine Kanyasu, alimuomba Rais Magufuli awapatie wananchi
mabaki ya mawe yenye dhahabu, maarufu kwa jina la Magwangala.
No comments:
Post a Comment