Wednesday 3 August 2016

MAREKANI YAIPATIA TANZANIA SHILINGI BILIONI 895


SERIKALI ya Marekani kupitia Shirika la Misaada ya Maendeleo (USAID), imeipatia Tanzania msaada wa Dola za Marekani milioni 407 (sh.bilioni 895), zitakazotumika kwa ajili ya kuendeleza sekta za kilimo, afya, nishati ya umeme, elimu na utawala bora, katika kipindi cha miaka mitano ijayo, kuanzia mwaka 2016/2020.

Hati za makubaliano hayo zilitiwa saini juzi, Dar es Salaam, kati ya Mkurugenzi wa USAID, Sharon Cromer na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dk.  Servacius Likwelile.

Msaada huo ni sehemu ya Dola milioni 800, sawa na zaidi ya sh. trilion 1.76 ambazo serikali ya Marekani kupitia USAID, imepanga kuipatia Tanzania ili kufanikisha Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa katika kipindi cha miaka mitano ijayo, wenye lengo la kuiwezesha Tanzania kufikia uchumi wa kati kupitia sekta ya viwanda ifikapo mwaka 2025.

Kiasi hicho cha fedha kitatumika na serikali ya Tanzania kupitia mfuko mkuu moja kwa moja, wakati kiasi kingine kitatumiwa na taasisi zisizokuwa za kiserikali, zinazofanya shughuli zake hapa nchini ili kufanikisha malengo ya msaada huo.

Miradi iliyopewa kipaumbele ni pamoja na kupambana na ukimwi na kifua kikuu, uzazi wa mpango, kupunguza vifo vya mama na mtoto, kukuza utawala wa kidemokrasia, usimamizi wa rasilimali za taifa na kuwekeza kwenye sekta ya umeme ili kuimarisha sekta ya viwanda na uzalishaji mali.

No comments:

Post a Comment