Wednesday 3 August 2016

DPP AWAFUTIA MASHITAKA FUIME NA WENZAKE 10




MKURUGENZI wa Mashitaka nchini (DPP), Biswalo Mganga amewafutia mashitaka washitakiwa 10, akiwemo aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Gabriel Fuime, waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya mauaji ya bila kukusudia, yaliyotokea baada ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa 16 kwenye mtaa wa Indira Gandhi, Dar es Salaam.

Wakati Fuime na wenzake hao 10, wakifutiwa mashitaka na kuachiwa huru jana, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, washitakiwa wawili, mmiliki wa jengo hilo, Raza Ladha na Mhandisi Mohamed Abdulkarim,  wanaendelea kushitakiwa.

Wakili wa Serikali Mkuu, Bernard Kongola akishirikiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi, waliwasilisha hati ya DPP ya kuwaondolea mashitaka washitakiwa hao mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Dk. Yohana Yongolo.

“Kutokana na mazingira ya shauri hili, upande wa jamhuri umeamua kuwafutia mashitaka baadhi ya washitakiwa,” alidai Wakili Kongola.

Hakimu Dk. Yongolo alimtaka Wakili huyo kueleza sababu za uamuzi huo, ambapo Wakili Kongola alidai hatua hiyo inatokana na upelelezi uliofanyika na ushahidi uliokusanywa.

Wakili Kongola alidai DPP amewasilisha hati hiyo kuwafutia mashitaka washitakiwa 10 kati ya 12, kwa kupitia kifungu cha 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).

Kongola aliwataja washitakiwa, ambao DPP amewasilisha hati ya kuwafutia mashitaka kuwa ni mhandisi wa jengo hilo, Goodluck Mmbanga, Mkaguzi wa jengo, Willbrod Mugyabuso na aliyekuwa diwani wa kata ya Goba, Ibrahim Kissoky, ambaye ni mfanyabiashara, anayemiliki Kampuni ya Lucky Construction ya Dar es Salaam, iliyojenga jengo hilo.

Wengine ni Mhandisi wa Manispaa ya Ilala Charles Ogare, Mhandisi Mshauri, Zonazea Oushoudada, anayemiliki Kampuni ya Sou Consultancy Co. Ltd, ambayo ilikuwa ikisimamia ujenzi wa jengo hilo, Msanifu Majengo, Vedasto Nzikoruhale na Mwandaaji Michoro ya Majengo Michael Hema, Msajili Msaidizi wa Bodi ya Wasanifu na Wakadiriaji Majenzi (AQRB), Albert Mnuo na Ofisa Mtekelezaji Mkuu wa AQRB, Joseph Ringo.

Kongola alidai washitakiwa waliobaki taarifa zimefailiwa kwenda Mahakama Kuu kwa ajili ya taratibu za kuwasomea maelezo ya mashitaka.

Baada ya kueleza hayo, Hakimu Dk. Yongolo alisema kwa mujibu wa maombi ya upande wa jamhuri, watuhumiwa walioorodheshwa katika hati ya kufutiwa mashitaka ya DPP, isipokuwa washitakiwa wawili, wameachiliwa huru kama ilivyoombwa.

Hakimu Dk. Yongolo aliwaeleza washitakiwa waliofutiwa mashitaka kwamba, kwa masharti ya kifungu kilichotumika kuwafutia mashitaka, hakiwazuii upande wa jamhuri kuwakamata na kuwafungulia mashitaka kama hayo.

Baada ya kusema hayo, Hakimu Dk. Yongolo aliwaachia huru washitakiwa hao 10 na kuahirisha kesi kwa washitakiwa wawili waliobaki hadi Septemba 7, mwaka huu.

Washitakiwa hao wawili wanakabiliwa na kesi ya kuwaua bila kukusudia  watu 27, ambapo wanadaiwa kutenda makosa hayo Machi 29, 2013, katika mtaa huo.

No comments:

Post a Comment