Friday, 3 March 2017
BAADHI YA VIWANDA VYA VIROBA VYAFUNGWA, WATENDAJI WAKAMATWA
MSAKO wa wauzaji, wazalishaji na watumiaji wa pombe kali aina ya viroba, umeendelea, ambapo baadhi ya viwanda vimefungwa na vingine kupewa amri ya kusitisha uzalishaji na baadhi ya watendaji wakiwekwa chini ya ulinzi.
Katika operesheni hiyo, iliyoshirikisha Jeshi la Polisi, baadhi ya viwanda na maghala yalibainika kuwa na stika feki za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), huku wawekezaji wakikimbia kukaguliwa.
Msako huo katika Jiji la Dar es Salaam, jana ulifanyika kwa makundi matatu, ikiwemo Temeke, Kinondoni na Ilala, ambapo lengo lilikuwa kuhakikisha viwanda vinavyokutwa na mzigo, vinazuiwa na kufungwa kwa ajili ya ukaguzi na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Katika hatua hiyo, kiongozi wa msafara wa timu ya Temeke, ambaye ni Mkaguzi kutoka Mamlaka ya Chakula na Dawa( TFDA), Aron Nzalla, alisema wafanyakazi wa kiwanda cha Global Distilleries Limited, akiwemo mhasibu, ofisi ya ugavi na manunuzi na mlinzi (majina yao yamehifadhiwa), waliwekwa chini ya ulinzi kwa ajili ya kuhojiwa.
Alisema katika kiwanda hicho cha kutengeneza pombe kali kwenye vifungashio vya viroba aina ya Premium Vodka na Ginja, walikamata katoni 1,500, huku kwenye ghala la Tema wakikamata katoni 650.
"Pia tumetembelea kiwanda cha Raenco Distillery Limited, watengenezaji wa pombe kali ya aina ya Officer's, ambapo tumekamata katoni 700 na kiwanda cha John Beverages (T) Limited, watengenezaji viroba aina ya Cuca Vodka, zaidi ya katoni 492 zimekamatwa," alisema.
Kwa upande wa Kinondoni na Ubungo, Mwanasheria wa Baraza la Mazingira, Heche Suguta, alisema katika Kiwanda cha Blue Nile, kilichoko Mbezi Africana, walibaini wanazalisha viroba aina ya Kitoko na Rivela Vodca.
Aidha, Kiwanda cha True Bell na Kibo Sprit, zimekutwa viroba aina ya Suke katoni 166 na Bonanza katoni 131, hivyo viwanda vyote uzalishaji umesimamishwa.
Heche alisema kikosi kazi hicho kinahakikisha taratibu za kisheria zinafuatwa na kusimamisha uzalishaji,utengenezaji,uuzaji na matumizi ya viroba ndani ya nchi na mipakani, ambapo tayari kila mpaka wamepewa amri ya kuzuia na kurejesha vilikotoka.
Alisema ukaguzi huo unaofanywa kwa kushirikiana Kamati za Ulinzi na Usalama na Kamati za Mazingira, kwa kufuata kanuni namba 76 ya 2017 ili kuzuia vifungashio vya pastiki vya pombe hizo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment