Friday, 3 March 2017
MIL. 396/- ZA MRADI WA MIKOKO ZADAIWA KUTAFUNWA
NAIBU Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Luhaga Mpina, amebaini madudu katika matumizi ya sh. milioni 396 za ufadhili wa Mfuko wa Nchi Maskini Zaidi Duniani, katika utekelezaji wa mradi wa upandaji na uendelezaji wa mikoko katika Delta ya Kaskazini ya Mto Rufiji.
Katika mradi huo, matumizi ya zaidi ya sh. milioni 364, mchanganuo wake hauridhishi huku vikundi vinavyodaiwa kulipwa fedha hizo, vikikana kulipwa na kusema kwamba, hawakuwa na mkataba bali walifanya kazi kama vibarua kwa posho ya sh. 10,000, kila wanapomaliza kazi na hawakuwa na mkataba.
Kutokana na hatua hiyo, Mpina amemuagiza Mkaguzi wa Ndani Ofisi ya Makamu wa Rais, Mwatano Maganga, kuhakikisha ndani ya mwezi mmoja anafanya uhakiki wa matumizi ya fedha hizo na kuelekeza hatua za kuchukua kwa kuwa vielelezo alivyokabidhiwa na msimamizi wa mradi kutoka Halmashauri ya Rufiji, Sabastian Gaganijas, vina mashaka.
Akizungumza baada ya kukagua Delta, hiyo yenye kilomita zaidi ya 15, alisema amesikitishwa na mradi huo wa fedha za wafadhili zaidi ya sh. milioni 396, kuwa na madudu na amejionea kuwa hauna usimamizi na kuna dalili ya fedha hizo kutumika ndivyo sivyo, kwa kuwa hata hekta 792, kati ya 1,000, zilizodaiwa zimepandwa ni udanganyifu.
“Huu ni uhuni, ambao haukubaliki kwa serikali hii. Tuliposema hapa kazi tu, tulimaanisha hatuwezi kudanganywa. Watu wamezoea kuona waziri hawezi kuja kwenye mazingira kama haya, nimejionea mwenyewe mikoko iliyopandwa haiendani na thamani ya matumizi ya fedha hizo na sehemu kubwa imevamiwa na kupandwa mpunga, badala ya mikoko,”alisema.
Alisema katika mchanganuo aliokabidhiwa na msimamizi wa mradi, zaidi ya sh.milioni 364, imedaiwa matumizi yake ni pamoja na kulipa vikundi 28, vilivyokabidhiwa mradi, ambavyo havipo.
Mpina alisema cha kushangaza, katika fedha hizo kipo kikundi kimelipwa zaidi ya sh. milioni 30, kwa kupanda hekta tatu huku kingine kikilipwa sh. milioni tatu kwa hekta hizo hizo.
"Mnataka kunidanganya, hamjui kwamba mimi sio mtu wa kudanganywa?
Mmepewa fedha za kupanda mikoko, fedha gani za serikali zinakuwa hazina ushahidi wa matumizi? Mkiwa mnajua tunakuja kukagua mradi, vitu vya msingi hamkuja navyo, mnaniletea karatasi yenye hesabu za ujanja ujanja,"alisema.
Alisema mradi huo unatia hasira zaidi baada ya kuona hauna usimamizi wa kutosha kuanzia Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), kwa kuwa hakuna aliyewakamata na kuwafikisha katika vyombo vya sheria wananchi wanaodaiwa kung'oa mikoko katika hifadhi na kupanda mpunga.
Kwa upande wake, Omari Kimlaga, aliyetajwa kuwa msimamizi wa kikundi, alisema mradi huo umekuwa na ubabaishaji kuanzia hatua ya awali, kwa kuwa baada ya makubaliano, walitakiwa kuwasilisha mikataba, bajeti na mpango kazi.
"Cha kushangaza tulipowasilisha vielelezo hivyo, hatukujibiwa kitu wala hatukuingia mkataba, ambao ulieleza tutakabidhiwa mbegu na kupewa maelekezo ya kitaalamu jinsi ya kupanda, kutunza hadi kukabidhi mikoko hiyo,"alisema.
Alisema mradi huo umefikia hatua mbaya zaidi kwa kuwa mbali na wao kuwa wanachukuliwa kama vibarua na kulipwa posho ya sh.10,000, hivi sasa wanachukuliwa vibarua bandarini kwa mtu yeyote kwenda kupanda na kulipwa.
Kwa upande wake, Mratibu wa mradi huo kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Cretus Shengena, alisema baada ya ofisi yake kukabidhi fedha za mradi kwa Halmashauri ya Rufiji, matarajio yalikuwa ni kuwa na vikundi 28 na kufanya kazi kwa mujibu wa makubaliano.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment