Thursday, 2 March 2017
BUNDUKI 10 ZA KIVITA ZAKAMATWA NGORONGORO
JESHI la Polisi Mkoa wa Arusha, limefanikiwa kukamata bundiki 10 za kivita katika kipindi cha wiki mbili, kufuatia operesheni iliyofanyika katika maeneo mbalimbali wilayani Ngorongoro mkoani hapa.
Akithibitisha kukamatwa kwa silaha hizo, mbele ya waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, alisema operesheni hiyo ilianza Februari 10 hadi 24, mwaka huu.
Kwa mujibu wa Mkumbo, silaha zilizosalimishwa na wananchi ni pamoja na Chinese SMG sita, Rifle mbili, Mark 1V na Mark III moja.
Aidha, Kamanda Mkumbo alisema kukamatwa kwa silaha hizo ni kufuatia mahojiano makali yaliyofanywa na polisi dhidi ya wazee wa kimila wa kabila la Wamasai na Wasonjo, ambao walifichua baadhi ya silaha zilipo, lakini pia kuzungumza na wananchi wanaowaongoza ili wakubali kusalimisha silaha hizo.
Kamanda Mkumbo alisema silaha aina ya Rifle (S.A.R), yenye namba KN 250374, iliyokuwa na risasi nne na Chinese 56 SMG, yenye namba MT 70B 12730021, ikiwa na risasi 21, zilitelekezwa kwenye ofisi ya Kijiji cha Mogaiduru, kata ya Olorieni.
"Katika kijiji cha Oldonyosambu, ilipatikana silaha aina ya Mark 1V, yenye namba ZKK 5602, iliyokuwa imetelekezwa kwenye kichaka na katika kijiji cha Jema, askari waliokuwa wanaendelea na oparesheni walifanikiwa kupata silaha nne aina ya Chinese 56 SMG pamoja na risasi 19," alisema.
Kwa mujibu wa Mkumbo, kati ya silaha hizo moja ilikuwa namba RT 7663, ya pili 563631144, ya tatu haikuwa na namba huku ya nne ikiwa imeandikwa STAR KRUJEVAC OSLA.
Operesheni hiyo pia ilifanikiwa kukamata silaha tatu katika kijiji cha Sale, ambazo ni Chinese SMG 56, yenye namba 89020539, ikiwa na risasi 15, S.R.R yenye namba 25032534 na MARK III yenye namba 263126.
Alisema katika msako huo, hakuna mtu yeyote aliyekamatwa na kwamba, wananchi wengi wa wilaya ya Ngorongoro, wanamiliki silaha kinyume cha sheria kutokana na mapigano baina ya Wamasai na Wasonjo.
Kamanda Mkumbo alisema licha ya mapigano hayo ya mara kwa mara, pia silaha hizo zinatumika kufanya matukio ya uhalifu, hasa ya ujangili, ambao unamaliza nyara za serikali.
Katika hatua nyingine, Athnath Mkiramwene anaripoti kuwa, Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro, amewataka madereva wa bodaboda kuangalia usalama wao kwanza wakati wanapofanya kazi zao nyakati za usiku.
Sirro alitoa wito huo jana, wakati wa mkutano uliowakutanisha waandishi wa habari, ukiwa na lengo la kutoa tathmini ya matukio ya uhalifu yaliyotokea mkoani Dar es Salaam.
Alisema madereva hao ni vyema wakaangalia kwanza usalama wao, hasa nyakati za usiku, kwa sababu kipindi hicho ndipo matukio mengi ya kiuhalifu yanatendeka.
“Ninasema tena polisi wana nia njema na watu wa bodaboda, hivyo ni vyema mkaangalia kwanza usalama wenu na kuhakikisha ifikapo saa sita, hakuna mtu kijiweni. Hii ni kutokana na kuanzia saa saba hadi saa tisa, kuwepo na matukio ya uhalifu na watu wa bodaboda mara nyingi kutumiwa pasipo kujua,” alisema.
Sirro alisema ni vyema kuwepo na sheria wakati wa utoaji wa leseni, ambayo itataja muda wa dereva wa bodaboda kumaliza kazi na kuepukana na matukio ya kiuhalifu.
“Wewe unayepiga kelele ni kwa sababu aliyeuawa sio mtoto au jirani yako, hivyo inatakiwa kila mtu kufuata sheria bila shuruti ili kutokomeza matukio ya kiuhalifi katika mkoa wetu wa Dar es Salaam,” alisema
Wakati huo huo, Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imefanikiwa kukamata majambazi 12, wa unyang’anyi wa kutumia silaha katika operesheni iliyofanyika Februari Mosi, mwaka huu.
Majambazi hao walikamatwa kwa nyakati tofauti, ambapo mara nyingi wamekuwa wakitumia usafiri wa pikipiki katika kutekeleza azma yao ya uhalifu wa kutumia silaha.
Sirro alisema, majambazi hao wamekamatwa wakiwa na pikipiki sita, ambazo zimekuwa zikitumika katika matukio ya kiuhalifu na nyingine zikiwa zimeporwa kwa wananchi.
Kamishna Sirro alisema katika mahojiano ya awali, majambazi hao wamekiri kutumia silaha katika matukio ya ujambazi, ikiwa ni pamoja na kuua na kujeruhi, ambapo upelelezi unaendelea na ukikamilika watafikishwa Mahakamani.
Katika hatua nyingine, Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 100, kwa kosa la dawa za kulevya, kuanzia Februari 25 hadi Machi Mosi, mwaka huu, katika operesheni ya kupiga vita dawa hizo.
Sirro alisema katika operesheni hiyo, jumla ya kete 413, za dawa za kulevya zimekamatwa, puli 50, misokoto ya bangi 86 na pombe haramu ya gongo lita 43.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment