Thursday, 2 March 2017
MBOWE AITWA NA TRA MAHAKAMANI
MWENYEKITI wa CHADEMA, Freeman Mbowe na wenzake wawili, wanaokabiliwa na mashitaka matatu, likiwemo la kutotoa risiti za kielekroniki, wametakiwa kufika katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala ili kujibu tuhuma hizo.
Wakili wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Marcel Busegano, alisema jana kuwa, washitakiwa hao wanadaiwa kutofika mahakamani tangu kesi hiyo ilipofikishwa Desemba, mwaka jana.
Kutokana na juhudi za kumtaka Mbowe kufika mahakamani kugonga mwamba, (TRA) waliomba mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mfawidhi, Ritha Tarimo, itoe barua ya wito ili washitakiwa hao waweze kufika baada ya siku 21.
Mbali na Mbowe, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Meneja wa klabu ya Bilicanas, Steven Mligo na mke wa Mbowe, Dk. Lilian Mtei.
Washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka matatu, ambayo ni kushindwa kutoa risiti za za kielektroniki, kutumia nyaraka za uongo na kushindwa kutekeleza matakwa ya kodi kinyume cha sheria.
Taarifa ambazo gazeti la Uhuru, ilizipata zinaeleza kuwa, TRA walijaribu kumpelekea barua ya wito Mbowe na wenzake, lakini hawakupatikana.
Kesi dhidi ya Mbowe na wenzake namba 402/2016 ya jinai, imefunguliwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala. Tangu kesi hiyo ifunguliwe, washitakiwa hawajawahi kufika mahakamani kujibu mashitaka yanayowakabili.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment