Friday, 3 March 2017

MAHAKAMA YAAMURU MALI ZA MSHITAKIWA ZITAIFISHWE


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeamuru kutaifishwa mali zinazomilikiwa na Mhasibu wa Kampuni ya UEE Tanzania Limited, Pastory Mayila, zinazodaiwa kuwa na thamani ya zaidi ya sh. milioni 362, baada ya kubainika zilipatikana kwa njia haramu.

Mali hizo ni nyumba tano, ambazo zimejengwa Buhongwa, wilayani Nyamagana, Mwanza, katika eneo ambalo halijapimwa na nyingine ipo Ilemela, mjini humo.

Nyingine ni hekari tano za ardhi, ambazo hazijapimwa, zilizoko Mwandu, Buhongwa, wilayani Nyamagana na magari manne, ambayo mawili ni aina ya Toyota Chasser, Toyota Landcruiser na Mitsubishi Fusso.

Uamuzi huo ulitolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Respicious Mwijage, kutokana na maombi yaliyowasilishwa mahakamani hapo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na kuungwa mkono na kiapo kilichoapwa na Wakili wa Serikali, Shadrack Kimaro.

Maombi hayo yaliletwa chini ya kifungu cha 9(1)(a) ya Sheria ya Mapato ya Uhalifu dhidi ya mlalamikiwa Mayila, ambaye alishitakiwa kwa makosa ya kughushi na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, lakini alitoroka.

Akitoa uamuzi huo, Hakimu Mwijage alisema, alibaini kuwa kutokana na hoja za AG, zilizowasilishwa mahakamani hapo, mlalamikiwa alijipatia sh. milioni 362.7 na mali hizo kwa njia ya udanganyifu.

Hakimu Mwijage alisema kutokana na hoja hizo, mlalamikiwa alinufaika kwa makosa aliyoyafanya, hivyo mali hizo zilipatikana kwa njia haramu.

"Hivyo ni lazima zitaifishwe kwa mujibu wa sheria,"alisema.

Ilielezwa kuwa, Machi 18, 2016, mlalamikiwa alishitakiwa kwa makosa matano katika mahakama hiyo, ambapo manne ya kughushi na moja la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Upande wa Jamhuri ulidai kuwa, kati ya Agosti 29 na Desemba 29, 2008, jijini Dar es Salaam, kwa nia ya kudanganya, alighushi fomu ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ya kuhamisha fedha, akidai kuwa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), iliilipa  kampuni yake kwa huduma mbalimbali sh. 3,392,812,190.28.

Upande wa Jamhuri ulidai kuwa, kati ya Agosti, 2008 na Februari, 2009, jijini Dar es Salaam, kwa nia ya kudanganya, mlalamikiwa alijipatia sh. milioni 362.7, kwa kudanganya alikuwa anastahili malipo hayo.

Mashitaka hayo yalifunguliwa mahakamani bila ya mshitakiwa kuwepo, ambapo upande wa Jamhuri uliomba mahakama kutoa hati ya wito kwa mshitakiwa kwa kutangaza kwenye magazeti. Maombi yalikubaliwa, lakini mlalamikiwa hakutokea.

No comments:

Post a Comment