Friday, 3 March 2017

SERIKALI YAMBWAGA MBOWE KORTINI


MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, imeyatupilia mbali maombi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe ya kutokamatwa na kuwekwa kizuizini, baada ya kukubaliana na hoja ya pingamizi la awali la serikali.

Jopo la Majaji watatu wa mahakama hiyo, likiongozwa na Jaji Sekiet Kihiyo, lilikubaliana na hoja iliyokuwa imewasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ya kwamba maombi hayo hayana nguvu kisheria kwa kuwa yamefunguliwa kwa kutumia kifungu cha sheria kisicho sahihi.

Mbowe alifungua maombi hayo kupitia jopo la mawakili wake likiongozwa na Tundu Lissu dhidi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (Paul Makonda), Kamishna wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam (Simon Sirro) na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa kanda hiyo (Cammilius Wambura).

Uamuzi huo ulitolewa jana mahakamani hapo, baada ya Jaji Kihiyo akishirikiana na majaji Pellagia Khaday na Lugano Mwandambo, kusikiliza hoja za pande zote kuhusu pingamizi la awali lililokuwa limewasilishwa na serikali.

“Mahakama inakubaliana na hoja mojawapo ya pingamizi la awali la upande wa Jamhuri kwamba kifungu cha 2(3) cha Sheria ya Usimamiaji Haki na Matumizi ya Sheria (JALA) kilichotumiwa na mleta maombi kuleta maombi haya si sahihi.
 

“Kutokana na hilo, mahakama inaona hakuna haja ya kuangalia hoja nyingine za pingamizi hilo. Hivyo maombi haya yanatupiliwa mbali,” alisema Jaji Mwandambo alipokuwa akisoma uamuzi huo kwa niaba ya jopo hilo la majaji.
 

Jopo hilo lilisema kesi ya msingi ya kikatiba iliyofunguliwa na Mbowe mahakamani hapo dhidi ya walalamikiwa hao na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, itasikilizwa Machi 8, mwaka huu.
 

Baada ya kutolewa kwa uamuzi huo, mawakili wa Mbowe, Jenerali Ulimwengu na Peter Kibatala walidai wanakaa kufanya marekebisho ya kifungu cha sheria ili wayawasilishe upya maombi hayo.
 

Wakili Ulimwengu alidai wataangalia sheria za Uingereza ili ziweze kusaidia kuyafungua upya maombi hayo na kwamba watayawasilisha mahakamani hapo leo.
 

Mbowe alifungua kesi ya kikatiba namba 1 ya mwaka huu, akipinga mamlaka ya Mkuu wa Mkoa kukamata na kumdhalilisha mtu, ikiwa ni siku chache baada ya Mkuu wa Mkoa Makonda kumtaja kuwa miongoni mwa watu 65 wanaotuhumiwa kujihusisha na dawa za kulevya na kutakiwa kufika Kituo Kikuu cha Polisi cha Kati.
 

Hata hivyo, Mbowe alikaidi wito huo, hivyo polisi walilazimika kumkamata kwa ajili ya kuhojiwa, ambapo aliamua kuwasilisha maombi mahakamani hapo kutaka amri ya kuzuia  polisi kumkamata na kumtia kizuizini.
 

Baada ya kufungua maombi hayo, upande wa jamhuri uliwasilisha pingamizi la awali likiwa na hoja tano za kuyapinga ikiwemo ya kwamba hayana nguvu kisheria kwa kuwa yamefunguliwa kwa kutumia kifungu kisicho sahihi.
 

Hoja nyingine za upande wa jamhuri za kupinga maombi hayo, zilizowasilishwa mahakamani hapo na jopo la mawakili wa serikali likiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Gabriel Malata akishirikiana na Mawakili wa Serikali Waandamizi Sylvester Mwakitalu, Haruni Matagane na Paul Shaidi ni kwamba mahakama hiyo haina uwezo wa kukubali maombi hayo.
 

Mawakili hao wa serikali walidai mahakama hiyo ni ya madai, hivyo haina mamlaka ya kusikiliza masuala ya jinai.
 

Walidai suala la Mbowe kukamatwa na polisi ni la kijinai na polisi wamefanya kazi yao kwa mujibu wa sheria. Alidai maombi hayo hayakupaswa kupelekwa katika mahakama hiyo, hivyo walitakiwa kuyapeleka kwenye mahakama husika.
 

“Sheria inaruhusu polisi kufanya uchunguzi na wana wajibu na mamlaka ya kumhoji mtu. Mambo yote haya yanafanywa na polisi kwa muda wanaotaka, hivyo mleta maombi atakuwa amejiweka juu ya sheria kwa kuiomba mahakama iwazuie polisi wasifanye kazi zake wala kuwakamata,” ilidaiwa na upande wa jamhuri.

Aidha, walidai hati ya kiapo inayounga mkono maombi hayo ina upungufu kisheria kwa kueleza mambo yanayohitaji ushahidi, suala ambalo ni kinyume na sheria.

Walidai kutokana na hati hiyo kuwa na upungufu huo, hati ya madai nayo inakuwa haipo sahihi mahakamani hivyo wanaomba itupiliwe mbali.

Mbali na hayo, walidai wakati Mbowe akiwasilisha maombi hayo mahakamani tayari,  polisi walishamkamata, kumhoji na kumuachia wenyewe baada ya kumaliza mahojiano, hivyo  wanaomba jambo ambalo limeshapitwa na wakati.

Wakijibu hoja za mapingamizi hayo, mawakili wa Mbowe, Lissu na  Peter Kibatala walidai mapingamizo hayo hayana mashiko kisheria na wanaiomba mahakama kuyatupilia mbali.

Lissu alidai mahakama hiyo imekaa kama mahakama ya haki za binadamu ambayo inaundwa pale panapokuwa na jambo muhimu na si kama mahakama kuu ya kawaida.

Alidai kwa mujibu wa sheria, Mahakama Kuu itakuwa na uwezo wake wa pekee wa kusikiliza na kuamua jambo lolote litakalofanywa na mtu yeyote chini ya Katiba.

Kibatala alidai upande wa jamhuri unaodai maombi hayo yamefunguliwa na kifungu ambacho si sahihi, haukueleza kifungu ambacho ni sahihi na hati ya kiapo imekidhi vigezo vya kisheria.

No comments:

Post a Comment