AFYA ya Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA),
Tundu Lissu, imeimarika na sasa ameondolewa kwenye Chumba cha Wagonjwa Mahututi
(ICU), katika hospitali anayotibiwa ya Aga Khan, jijini Nairobi, nchini Kenya.
Hayo yalisemwa jana na Mwenyekiti wa CHADEMA,
Freeman Mbowe, alipozungumza na vyombo vya habari, kuhusu hali ya afya ya Lissu,
ambaye alishambuliwa kwa risasi nyumbani kwake, Dodoma.
Mbowe alisema, Lissu alitoka ICU, wiki iliyopita,
ambako alikuwa akipatiwa matibabu ya kuondolewa risasi katika mwili wake.
“ Kwa sasa Mheshimiwa Lissu ametoka ICU, baada ya
kufanyiwa upasuaji mara 17 mpaka sasa. Mashine zilizowekwa katika mwili wake
zimeondolewa.
“Sasa hivi hatumii mipira ya oksijeni, hatumii
mipira ya chakula na anakula mwenyewe bila ya kutumia mipira,”alisema .
Alisema kwa sasa,
Lissu anaweza kukaa mwenyewe, huku akitembelea kiti cha kusukuma na
kwamba, mwishoni mwa wiki, alitembezwa katika baadhi ya maeneo ya karibu ya jiji
hilo ili kupata hewa safi.
Alisema kutokana na hali yake kuimarika, picha zake
na pamoja na anavyozungumza, zitaanza kurushwa katika mitandao ya kijamii, ili
jamii iweze kumuona hali yake.
“Kuanzia leo (jana), mtaanza kusikia sauti yake na
kuiona video yake, tulikataa kutoa picha zake zaidi ya mwezi, lakini kwa sasa
tutatoa,”alisema.
Akizungumzia matibabu yake, alisema mpaka sasa
yako katika awamu ya pili katika hospitali hiyo, ambapo ya kwanza yalifanyika
katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Alisema awamu ya tatu ya matibabu yake, itafanyika
hospitali nyingine nje ya Kenya, kwa ajili ya kuendelea na matibabu zaidi.
Hata hivyo, alisema kwa sasa hospitali na nchi
anayokwenda kutibiwa hawawezi kuitaja kutokana na sababu za kiusalama.
Alisema kabla ya mwisho wa mwezi huu, wanatarajia
mbunge huyo kuruhusiwa, iwapo madaktari
wa hospitali hiyo wataridhika na afya yake.
Kuhusu
waliochangia gharama za kumtibia Lissu, aliwashukuru wananchi bila ya
kujali itikadi za vyama, serikali na wadau nje ya nchi, kwa kuchangia gharama
za matibabu hayo.
Septemba 7, mwaka huu, Lissu alipigwa risasi na
watu wasiofahamika, wakati akirejea nyumbani kwake, baada ya Bunge kuahirishwa
nyakati za mchana.
000000000
No comments:
Post a Comment