Saturday, 21 October 2017

BARIRICK WAMEBANA WAMEACHIA



NA JACQUELINE MASSANO
HATIMAYE Kampuni ya Barrick, imekubali masharti yote ya sheria mpya za madini, hivyo kuifanya Tanzania kuwa ya kuigwa, hasa kwenye sekta ya madini.
Kampuni hiyo imeonyesha nia njema kwa kukubali kutoa Dola za Kimarekani milioni 300 (sawa na zaidi ya sh. bilioni 700), wakati mazungumzo ya jambo hilo yakiwa yaendelea.
Kutokana na hali hiyo, Rais Dk. John Magufuli, ameitaka kampuni hiyo kulipa fedha hizo haraka kwa sababu, anataka kuzitumia kwa ajili ya maendeleo ya jamii.
Agizo hilo, alilitoa jana, Ikulu, Dar es Salaam, alipokuwa akipokea taarifa ya mazungumzo yaliyofanyika kati ya timu ya wataalamu aliyoiunda na ile ya kutoka kampuni ya Barrick ya Gold Mining, kuhusu madini ya dhahabu na mchanga wenye makinikia.
Rais Magufuli alisema, Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni hiyo, Profesa John Thornton, aliagiza timu yake kutoka Marekani na Canada kwa ajili ya kufanya mazungumzo kwa miezi mitatu, wakijua suala hilo siyo dogo.
"Nashukuru alifahamu nia ya Tanzania, asingeweza kuipuuza," alisema Rais Magufuli.
Alisema katika mazungumzo hayo ya timu hizo mbili, kwa mara ya kwanza, Tanzania tangu dunia iundwe, itakuwa inatapa 50 kwa 50, katika faida itakayokuwa inapatikana kwenye madini.
"Fedha hii tukiipata, tutakuwa tunaipeleka kwenye miundombinu, dawa na huduma za jamii. Lakini ile haki yetu ya asilimia 16, ipo pale pale. Kwenye masuala mengine ya kulipa kodi, zitaendelea kulipwa kama kawaida. Kwa hiyo ukijumlisha ni faida kubwa," alisema.
Pia, alisema katika menejimenti, watakuwepo Watanzania, labda kama wataweka watu, ambao watakuwa wezi ili waendelee kuliibia taifa.
"Kwa sababu unaweza ukawa unamuweka mtu unamuamini, hapo ndiyo ikawa kazi, akaenda akanunuliwa, akapata maslahi yake badala ya Watanzania. Na kwenye hili, wale tutakaowateua kwenda huko, vyombo vinavyohusika vifanye uchunguzi wa kweli," alisema.
Vilevile, alisema kama itawezekana, bodi ya wakurugenzi itakayoundwa itoke kwenye timu ya mazungumzo aliyoiunda kwa sababu, wanajua uchungu, wameshapimwa na wamekaa na hawawezi kurubuniwa.
"Lakini sijasema wengine wasiwepo kwenye bodi hiyo," alisisitiza.
Rais Magufuli alisema, mazungumzo hayo hayajawahi kufanyika mahali popote Afrika, hivyo ana hakika nchi zingine zitakuja kujifunza kupitia Tanzania.
"Mazungumzo huwa yana faida kubwa. Ndiyo maana nawashukuru wote mliohusika, na ndiyo maana nasema, itabidi niandae vyeti vya shukrani kwa wale wote waliohusika kwenye tume ya kwanza, ya pili na nyie mliofanya mazungumzo," alisema.
Alizipongeza timu hizo mbili kwa kufanya mazungumzo na kufikia makubaliano kwa sababu kazi hiyo ilikuwa ngumu na moto ulikuwa unawaka.
"Tumefikia hatua hii kwa sababu ya Mungu, kazi hii ilikuwa kubwa, haikuwa ndogo," alisema.
Aliwapongeza Watanzania kwa kuwa wavumilivu na watulivu, licha ya kuwepo kejeli za hapa na pale zilizokuwa zimejitokeza.
"Nchi yetu ni tajiri, lakini tumefika hapa kutokana na wizi na dhuluma zilizokuwa zikijitokeza. Kwa ndugu zangu Watanzania, huu ni mwanzo wa kuijenga Tanzania mpya, hakuna mtu atakayekuja kututengenezea Tanzania yetu.
"Kila mtanzania mahali alipo, lazima ajue ana wajibu wa kufanya mabadiliko ya kweli katika nchi hii," alisema.
Kutokana na hali hiyo, aliwataka Watanzania kusimamia rasilimali za Tanzania kwa sababu ipo siku zitaisha na wataanza kulaumiana.

ZAMU YA ALMASI NA TANZANITE
Rais Magufuli alisema, baada ya kumalizika kwa mazungumzo ya dhahabu, timu hiyo inatakiwa kufanya makubaliano kwenye kampuni za Almasi na Tanzanite.
"Mpange mapema, muanze haraka, hakuna kulala, zege halilali. Lazima twende kwa spidi hii ili tuanze mazungumzo na wanaochimba almasi na tukubalinae nao ili tuweze kupata faida na Tanzanite nayo hivyo hivyo," alisema.
Alisema wawaite wahusika ili wazungumze nao, watakaokataa waondoke moja kwa moja na wasirudi nchini.
"Ambaye hatakuja kufanya majadiliano na kukubaliana na sisi wakati tanzanite na almasi tumepewa na Mungu, ni zawadi yetu, waondoke, wasirudi. Tutafanya hivyo hata kwenye madini mengine. Ndugu zangu, mimi leo nina furaha sana," alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni hiyo, Profesa Thornton alisema, wamekubali kulipa Dola za Kimarekani milioni 300 (sawa na sh. bilioni 700), kwa ajili ya kuonyesha uaminifu.
"Nampongeza Rais Magufuli kwa uamuzi wa kutaka muafaka juu ya makinikia. Tumekubaliana kulipa Dola za Kimarekani milioni 300 kama sehemu ya kujenga uaminifu na kuendeleza biashara," alisema.
Waziri wa Katiba na Sheria, ambaye pia ni mwenyekiti wa tume hiyo, Profesa Palamagamba Kabudi, alisema baada ya mazungumzo ya pande hizo mbili, Barrick imekubali masharti yote yaliyomo kwenye sheria mpya za madini, zilizotungwa na Bunge.
"Wamehakikisha masharti hayo yote yanaingia katika mfumo wa fedha ambao tumekubaliana," alisema.
Pia, alisema wamekubali serikali itapata hisa katika migodi hiyo kwa asilimia 16, kama sheria ilivyotamka.
"Lakini pamoja na kuwa na asilimia 16, kama sheria ilivyotamka, wamekubali linapokuja suala la kugawana, itakuwa nusu kwa nusu. Kwa hiyo, sisi (Tanzania) wenye asilimia 16 na wao wenye asilimia nyingi zaidi, litakapokuja suala la mgawo, itakuwa ni 50 kwa 50," alisema.
Alisema wamekubaliana kwamba, migodi hiyo itaweka fedha zao zote za madini katika akaunti zilizopo hapa nchini.
Profesa Kabudi alisema, wamekubalina ofisi za migodi hiyo zilizoko London na Johannesburg, zitahamishiwa Tanzania na makao makuu yake yatakuwa Mwanza, ili iwe karibu na machimbo hayo.
"Lakini, tumekubaliana kuna umuhimu wa kuanzisha kampuni mpya ya kusimamia na kuendesha migodi itakayoongozwa na Mtendaji Mkuu, Mkurugenzi wa Fedha na Mkurugenzi wa Manunuzi kutoka Tanzania.
"Ingawa serikali itakuwa na asilimia 16 na mgao wa 50 kwa 50, wamekubali serikali iwe na wawakilishi  katika bodi ya wakurugenzi katika kampuni hiyo," alisema.
Aliongeza: "Pia, wamekubali sehemu kubwa ya kazi za migodini kwa kiasi kikubwa zitafanywa na kampuni za Tanzania na Watanzania. Wamekubali kuimarisha huduma za jamii katika maeneo yatakayozunguka migodi ya wananchi wenyewe."
Pia, alisema wamekubali kuwa kila kampuni itakayoendesha mgodi, itahakikisha inaachana na utaratibu wa kutumia wafanyakazi wa mikataba, badala yake kuajiri wafanyakazi wazawa.
Alisema Barrick wamekubali kujenga maabara kubwa ya kisasa na kiwanda cha kuchakata makinikia hapa nchini.
"Mafanikio mengine ambayo tumeyapata ni kwamba, wamekubali serikali itakuwa na umiliki wa madini mengine yote katika makinikia kama yatapatikana," alisema.
Profesa Kabudi alisema katika mazungumzo hayo, wamekubali kuwa kesi na mashauri yote ya madini yatafanyika hapa nchini, siyo nje ya nchi kama ilivyozoeleka.
Kuhusu suala la fidia, alisema: "Jambo hili limekuwa gumu kwa sababu mambo yaliyofanyika yalifanywa kwa miaka 16. Na eneo hili ndilo lilichukua muda mrefu wa mazungumzo yetu, ilibidi tupitie nyaraka na risiti zote na kuona kuwa ni jambo ambalo linahitaji muda," alisema.
Kutokana na hali hiyo, alisema ili kuonyesha nia yao njema, wamekubali kutoa sh. bilioni 700, wakati mazungumzo ya jambo hilo yanaendelea.
Alisema mazungumzo hayo hayakuwa mapesi, yalikuwa magumu ambapo kuna muda walitetereka, lakini pande zote mbili ziliona ni muhimu wakakubaliana mambo ambayo yatajenga msingi imara.
"Tulifika mahali tukaona ni muhimu tukakubaliana mambo ambayo yatajenga msingi imara wa mahusiano yetu ya siku za usoni, lakini pia bila kufunika chini ya zuria yale yote yaliyofanyika huko nyuma," alisema.
Malengo ya serikali katika majadiliano hayo, yalikuwa kuainisha fidia kutokana na makosa mbalimbali yaliyofanywa na Kampuni ya Barrick hapa nchini, kujadili na kuweka mfumo mpya wa uendeshaji wa shughuli za uchimbaji na biashara ya madini ili kuleta mgawo sawa kwa sawa wa mapato kati ya serikali na kampuni za Barrick.
Mengine ni kujadili na kukubaliana muundo na mfumo wa uendeshaji, utakaowezesha Tanzania kupata manufaa zaidi kutokana na uwekezaji unaofanywa kwenye migodi.
Makubaliano mengine ni kubadilisha mikataba ya uendeshaji migodi ili iendane na marekebisho ya sheria ya madini na kuhakikisha wananchi na jamii inayoizunguka midogo, inapata manufaa zaidi kutokana na uwepo wa migodi kwenye maeneo yao.

No comments:

Post a Comment