POLISI mkoa wa Arusha, wanawashikilia watuhumiwa wawili wanaodaiwa kumuua mtoto wa Waziri Mkuu wa zamani, Hayati Edward Moringe Sokoine, Tumaini Sokoine (41), maarufu kwa jina la Kereto.
Akizungumza na Uhuru, jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, alisema tukio hilo lilitokea juzi, saa 3.30 usiku, nyumbani kwa marehemu, Monduli Juu, mkoani hapa.
"Ni kweli mtoto wa tano wa mke mkubwa wa hayati Sokoine, aliuawa juzi, usiku na katika tukio hilo, polisi tunawashikilia watu wawili na upelelezi bado unaendelea,"alisema.
Kamanda Mkumbo alisema, polisi walipofika eneo la tukio, walikuta mwili wa marehemu ukiwa na majeraha mbalimbali, hali ambayo ilionyesha dhahiri kulikuwa na ugomvi.
Mkumbo alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hosptali ya Wilaya ya Monduli na kwamba, utafanyiwa uchunguzi muda wowote.
Akizungumza kwa niaba ya familia, msemaji wa familia ya hayati Sokoine, Lembris Kipuyo, alisema Kereto alipoteza maisha kwa kuguanguka, siyo kuchomwa kisu kama baadhi ya mitandao ya kijamii inavyoandika.
Kipiyo alisema, Kereto aliruka ukuta wa uzio wa nyumbani kwa mama yake mzazi, Naponi na kuanguka, kisha kugonga kichwa na damu kuvuja kwenye ubongo na kumsababishia mauti.
Alisema wamesikitishwa na taarifa zinazosambazwa mitandaoni huku zikiwa hazina baraka za familia kuwa, Kereto aliuawa kwa kuchomwa kisu kwenye ugomvi na mke wake, Maria Tumaini.
"Taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa marehemu Kereto aliuawa kwa kuchomwa kisu na mkewe, ni za uongo, hazina ukweli wowote, Watanzania wazipuuze,"alisema.
Kwa mujibu wa Kipuyo, taarifa hizo za uzushi, zinasambazwa na baadhi ya wanasiasa wenye nia ovu kwa lengo la kuitia doa na kuichafua familia ya hayati Sokoine.
"Kuna baadhi ya wanasiasa wanaotaka kuutumia msiba huu kupata umaarufu kwa kutoa taarifa mbalimbali. Hawa ni wanasiasa wenye nia ovu dhidi ya familia yetu, lengo lao ni kutuchafua kwa kuwa ni mahasimu wetu wa kisiasa,"alisema.
Akifafanua kuhusu kifo hicho, Kipuyo alisema Keretio alitoka nyumbani kwake, Monduli Juu, saa 3.30 usiku, Oktoba 17, mwaka huu, kwenda kwa mama yake na baada ya kufika, alikuta lango kuu likiwa limefungwa.
"Alikuwa amekunywa pombe kidogo na baada ya kukuta lango limefungwa, alilazimika kuruka ukuta na kwa bahati mbaya, alianguka na kugonga kichwa chini, hali iliyosababisha ubongo kuvuja damu.
"Kereto alikuwa akiishi umbali wa mita 600, kutoka nyumbani kwa mama yake na juzi, kwa bahati mbaya, alikuwa amekunywa kidogo na akilewa. Huwa anakuwa mkorofi kwa hiyo hakuvuta subira ya kufunguliwa lango kuu,"alisema.
Kwa mujibu wa Kipuyo, watu waliokuwa nyumbani hapo walisikia kishindo kikubwa kwenye lango kuu na walipokwenda kuangalia, walimkuta marehemu amelala chini akivuja damu nyingi kichwani.
Alisema kutokana na hali hiyo, walimkimbiza katika Kituo cha Afya cha Engwiki, kilichopo karibu na nyumbani hapo, ambako alipatiwa huduma ya kwanza.
Kipuyo alisema, baada ya kupatiwa huduma ya kwanza, alikimbizwa Hosptali ya Wilaya ya Monduli, ambako alipoteza maisha akiwa njiani.
Kereto enzi za uhai wake, alijihusisha na shughuli za kilimo na ufugaji. Maziko yake yanatarajiwa kufanyika keshokutwa, nyumbani kwao Monduli Juu.
No comments:
Post a Comment