NA MWANDISHI WETU-MAELEZO
JITIHADA za serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk. John Magufuli za kuimarisha uchumi na kuvutia wawekezaji, zimeanza kuzaa matunda, baada ya Tanzania kutajwa kwenye ripoti maalumu ya dunia, juu ya ushindani wa kibiashara, uchumi na uwekezaji, kuwa ni nchi inayopiga hatua.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, iliyotoka hivi karibuni, Tanzania imetoka nafasi ya 116, duniani hadi 113, ikionyesha itafanya vizuri katika kipindi kijacho kutokana na sera za kuvutia wawekezaji na kupambana na rushwa na ufisadi, kunakofanywa na serikali iliyo madarakani.
Mbali na changamoto kadhaa zinazoikabili sekta ya uwekezaji na uchumi nchini, ripoti hiyo imebainisha kuwa, katika kipindi cha miaka michache ijayo, Tanzania itakuwa miongoni mwa nchi zitakazopiga hatua kubwa katika uwekezaji wa viwanda.
Baadhi ya changamoto zilizoainishwa kwenye ripoti hiyo, ambazo kama nchi zimeshaanza kufanyiwa kazi ni upatikanaji wa mitaji, mfumuko wa bei, uhaba wa miundombinu rafiki na urasimu katika mamlaka za maamuzi, hasa kwenye ngazi za halmashauri na mikoa.
Hivi karibuni, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, alinukuliwa akisema, wizara yake inajitahidi usiku na mchana, kuhakikisha inaweka mazingiza wezeshi ya uwekezaji, hasa kwenye sekta ya viwanda ili kufikia azma ya nchi ya viwanda.
Miongoni mwa jitihada hizo ni kufufua viwanda vilivyobinafsishwa, ambavyo havijaendelezwa, kuanzisha vipya na kuleta nchini wawekezaji katika viwanda, kilimo na uzalishaji mali.
Aidha, ripoti hiyo ya dunia, ambayo ni ya mwaka 2017/2018, imebainisha kuwa, Tanzania ni miongoni mwa nchi chache za Afrika Mashariki, ambazo zinaaminika na wawekezaji, hasa kwa kuwa hatua za kupambana na rushwa zinaonekana wazi na nia ya dhati ipo.
Utulivu wa kisiasa pia imeelezwa katika ripoti hiyo kuwa ni miongoni mwa vigezo vinavyoifanya Tanzania kuaminika na kupata nafasi za juu kiuwekezaji duniani.
Mbali na Tanzania kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki, Rwanda inaonekana kufanya vizuri kwenye vita dhidi ya rushwa na ufisadi, jambo ambalo limesaidia kuvutia uwekezaji katika nyanja mbalimbali nchini humo.
Ripoti ya Dunia ya ushindani na uwajibikaji kiuchumi ni taarifa inayotolewa kila mwaka na Jukwaa la Uchumi la Dunia (World Economic Forum), tangu mwaka 2004, kwa lengo na kutathmini vigezo vya uwajibikaji katika nchi.
Baadhi ya vigezo vinavyotumika katika tathmini na kuzipa nchi maksi ni uwepo wa taasisi bora za uchumi na uwekezaji, ubora wa miundombinu, huduma za afya, upatikanaji wa elimu bora ya msingi, vyuo na taasisi za elimu ya juu, upatikanaji wa masoko na mitaji na ukuaji wa ajira.
Vigezo vingine ni matumizi ya teknolojia katika ukuzaji wa masoko ya ndani na nje, ubunifu na uongezaji wa thamani na ubora katika mazao.
No comments:
Post a Comment