Saturday, 21 October 2017

WANAOCHAKACHUA VIPIMO WAONYWA

 
SERIKALI imetoa onyo kwa baadhi ya wananchi wanaofanya uchakachuaji wa vipimo, hususan mizani kwa lengo la kujiongezea faida kibiashara.
Imesema haitasita kumchukulia hatua kali yeyote atakayebainika kuwaibia wananchi kwa kutumia mizani mbovu kwa vipimo vya bidhaa.
Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhandisi Stella Manyanya, aliyasema hayo jana, alipozitembelea ofisi za makao makuu ya Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA), Ilala jijini Dar es Salaam.
Alisema kumekuwa na tabia ya baadhi ya watu kuchakachua vipimo, hasa kwenye upimaji wa mitungi ya gesi asilia na kusababisha watumiaji kulalamika kutokudumu kwa gesi hizo.
"Unakuta mtu ananunua mtungi wa gesi wa uzito fulani, anautumia kidogo tu gesi imeisha, kumbe uzito ulioainishwa haukuwa ujazo halisi wa gesi, huu ni wizi," alisema.
Pamoja na hilo, alisema lumbesa ambayo inaendelea kudhibitiwa na WMA kwenye maeneo yote nchini, ni uonevu kwa mkulima, ambaye anavuja jasho jingi, lakini badala ya kunufaika, mfanyabiashara anamlalia kimaslahi.
"Gunia ni kilo 100, lakini kuna magunia mengine yana mpaka kilo 170, kutokana na ziada zilizoongezwa wakati wa kulifunga, eti ili lipendeze, hii haikubaliki nawaomba muendelee kuwabana wahalifu," alisisitiza.
Naibu waziri huyo alitumia fursa hiyo kuwaagiza watumishi wa Wakala wa Vipimo, kuendelea kufanyakazi kwa bidii kwa ajili ya ujenzi wa taifa lao.
Alisema anatambua wanazo changamoto za mishahara midogo, tatizo ambalo kwa namna fulani linaweza kupunguza morali ya utendaji, lakini wanapaswa kuwa wavumilivu wakati serikali inaendelea kulishughulikia.
"Tunaomba muendelee kuiunga mkono serikali yenu, Rais Dk. Magufuli kajitoa kwa ajili yetu, tumsaidie na mahitaji yetu yatatatuliwa kwa wakati.
"Mimi namshukuru kwa kuniteua kumsaidia Waziri wa Viwanda, namuahidi nitafanyakazi kweli kweli, sitakubali mtu aturudishe nyuma kwenye kuiletea hii nchi maendeleo," alisema.
Mhandisi Manyanya alisema vipimo sahihi ni muhimu kwa maendeleo ya taifa, kwa sababu vinatoa nafasi kwa pande mbili kupata haki zinazostahili, badala ya kuwepo uonevu na dhuluma.
Kwa upande wake, Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa wakala huo, Dk. Ludovick Manege, alisema mbali na changamoto zao, wamejitahidi kwenye utumishi, ambapo wamefanikiwa kufungua ofisi zake kwenye mikoa 28, Tanzania ili kusogeza huduma zao karibu na wananchi.
Aliahidi kutoa ushirikiano kwa Mhandisi Manyanya huku akikumbushia suala la kushughulikiwa kwa maombi yao kwa serikali, hususan suala la uboreshaji wa maslahi na upandishaji wa vyeo vya watumishi.

No comments:

Post a Comment