UMOJA wa Mataifa (UN), umepongeza jitihada zinazofanywa na serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo, ikiwemo kuruhusu kupokea wakimbizi kutoka nchi zinazokabiliwa na machafuko.
Pia, UN imesisitiza kuendelea kushirikiana na serikali pamoja na wadau wa maendeleo, katika kuunga mkono juhudi hizo za serikali.
Akizungumza Dar es Salaam, jana, Mwakilishi Mkazi wa UN, Alvaro Rodriguez, alisema umoja huo kupitia taasisi zake, utahakikisha Tanzania inanufaika na fursa mbalimbali za kiuchumi zinazotolewa na UN.
“Mabadiliko makubwa yamekuwa yakifanywa na serikali kwa lengo la kuifanya nchi kuwa yenye uchumi wa viwanda na kipato cha kati.
“UN tunapongeza juhudi za serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo. Ushirikiano kati ya Tanzania na UN, ni mzuri katika kuhakikisha maendeleo endelevu yanaendana na wananchi,” alieleza.
Katika kufanikisha hilo, Rodriguez alieleza namna UN inavyotekeleza mradi wa kuwajengea uwezo na kuwawezesha wananchi wa Mkoa wa Kigoma, ambao umekuwa ukipokea idadi kubwa ya wakimbizi.
Alisema Kigoma ni miongoni mwa mikoa ambayo ipo nyuma kiuchumi kutokana na kukabiliana na wimbi la wakimbizi, hivyo miradi mbalimbali ya kiuchumi imeibuliwa katika kuwawezesha wananchi.
Mwakilishi huyo wa UN, pia alizungumzia maadhimisho ya siku ya Umoja wa Mataifa, inayotarajiwa kufanyika Oktoba 24, mwaka huu.
Alisema katika maadhimisho hayo yatakayofanyika kwenye viwanja vya Karimjee, yatakuwa na kauli mbiu isemayo “Maendeleo ya viwanda yazingatie utunzaji wa mazingira na maendeleo endelevu”.
Zaidi ya wageni 500, kutoka taasisi mbalimbali za serikali, kigeni, mabalozi na wanafunzi, watahudhuria maadhimisho hayo, ambayo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Kimataifa na Kikanda, Susan Kolimba, alisema bado serikali imekuwa ikishirikiana kwa karibu na UN.
Alisema programu inayotekelezwa na UN mkoani Kigoma, imelenga kuwainua wananchi kiuchumi, kuwajengea uelewa na kutoa misaada kwa wakimbizi.
Susan alieleza kuwa, utekelezaji wa programu hiyo ni wa miaka miwili, ambapo awamu ya kwanza ilijikita kuwaendeleza wananchi kiuchumi.
“Awamu ya pili itahusisha kuhamasisha amani, umoja na maendeleo endelevu kwa wananchi,” alisema.
Alieleza umoja huo pia umetoa fedha zaidi ya sh. milioni 100, katika Chuo Cha Polisi Moshi (CCP), kuwajengea uwezo walimu wa chuo hicho kupambana dhidi ya ukatili wa wanawake.
No comments:
Post a Comment