Saturday, 21 October 2017

WANAFUNZI 10, 196 KUKOPESHWA BIL. 34.6/-


HATIMAYE Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB), imetoa majina ya awamu ya kwanza ambapo jumla ya wanafunzi 10,196 wamefanikiwa kupata mkopo kwa mwaka wa masomo wa 2017/2018.
Majina hayo yalitangazwa jana na Mkurugenzi wa bodi hiyo, Abdul-Razaq Badru alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari wakati akitaja idadi ya wanafunzi waliopata mkopo huo.
Alisema, zaidi ya sh. bilioni 34.6 zimetengwa kwa ajili ya wanafunzi hao ambao wamepata mkopo kwa awamu ya kwanza.
“Orodha ya kwanza ya majina yote ya wanafunzi waliopata mkopo, inapatikana katika tovuti ya bodi ya mikopo www.helsb.go.tz na itatumwa kwa vyo husika. Orodha nyingine (batches) zitafuata kadri taratibu za udahili na uchambuzi zinavyokamilika.
"Lengo ni kutoa majina ya wote kwa waliofanikiwa kupata mkopo kabla ya vyuo kufunguliwa mwishoni mwa mwezi huu wa Oktoba,” alisema.
Vilevile, alisema kwa mwaka huu wa masomo, zaidi ya sh. bilioni 108.8, zitatolewa kwa ajili ya wanafunzi 30,000 wa mwaka wa kwanza.
“Wanafunzi waliopata udahili katika chuo zaidi ya kimoja na ambao wana sifa za kupata mkopo, watapangiwa mikopo baada ya kuthibitishwa chuo watakachojiunga kwa ajili ya masomo kwa mwaka huu wa masomo 2017/2018,” alisema Badru.
Wakati huo huo, alisema wanafunzi waliofaulu mitihani yao na wanaondelea na masomo fedha zao zitaanza kutumwa vyuoni kuanzia leo (jana).
Alisema, kiasi cha sh. bilioni 318.6 kitatolewa kwa wanafunzi 93,295 wanaoendelea na masomo kwa mwaka 2017/18.
"Tayari serikali imeshatuma fedha hizo, lengo la bodi ni kuhakikisha zinafika vyuoni kabla ya kufunguliwa kwa vyuo ili kuwaondolea usumbufu wanafunzi," alisema.
Naye, Kaimu Mkurugenzi wa Upangaji na Utoaji Mikopo wa HESLB, Dk. Veronica Nyahende alisema kwa upande wa wanafunzi waliokosea kujaza fomu za mkopo, majina yao yatafanyiwa uchambuzi na  kazi ikikamilika majina hayo yatatolewa tena.
Alisema kwa mwaka huu waliingia kwenye mfumo mpya ambao ni wa mtandao ambapo mwombaji akikosea kuomba anatakiwa kufanya hivyo upya nakuweka viambatanisho vyote.
"Hivyo kwa mwaka huu baada ya wanafunzi hao kukosea hatukuwa na utaratibu wa kuwaita waje hapa makao makuu, lakini wataomba upya,” alieleza Dk. Nyahende.
Hata hivyo, aliwasihi waombaji wa mikopo kuwa na subira wakati bodi hiyo ikiendelea kukamilisha maandalizi ya orodha zinazofuata za wanafunzi walioomba mikopo.
Awamu ya kwanza ya wanafunzi 10,196 waliopata mkopo, imepatikana baada ya bodi ya mikopo kupokea na kuchambua  majina ya wanafunzi 32,495 waliopata udahili katika chuo kimoja.

No comments:

Post a Comment