Saturday 21 October 2017

SERIKALI YALIPA MADENI YA SH. BILIONI 190


NA BENNY MWAIPAJA, KAGERA
SERIKALI imelipa madeni ya wazabuni, wakandarasi na malimbikizo ya wafanyakazi yanayofikia kiasi cha sh. bilioni 190 katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia Julai hadi Septemba mwaka huu baada ya kufanya uhakiki wa madeni halali inayodaiwa na wafanyakazi na watoa huduma mbalimbali.
Hayo yalisemwa Mjini Bukoba mkoani Kagera na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, wakati akizungumza na Jumuiya ya Wafanyabiashara wa mkoa huo akiwa katika ziara ya kikazi kukagua utendaji wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Wakala wa Huduma ya Ununuzi  Serikalini (GPSA).
Dk. Kijaji alisema kuwa wazabuni wamelipwa kiasi cha shilingi bilioni 67.2, wakandarasi wamelipwa shilingi bililioni 24.2, watoa huduma mbalimbali wamelipwa Sh. bilioni 38, watumishi wa umma wamelipwa Shilingi bilioni 37, huku wadai wengine wakilipwa sh. bilioni 24.
Alisema kuwa, katika bajeti ya mwaka 2016/2017, serikali imetenga zaidi ya sh. trilioni moja kwa ajili ya kulipa madeni mbalimbali na kwamba, itaendelea kulipa madeni yote yaliyohakikiwa.
Dk. Kijaji aliiambia Jumuiya ya Wafanyabiashara mkoani Kagera kuwa, serikali inatambua mchango wao mkubwa katika maendeleo ya Taifa kutokana na kulipa kodi zinazochangia kuboresha miundombinu na huduma mbalimbali za jamii.
Alitoa wito kwa wafanyabiashara kutumia mashine za kielektroniki katika biashara zao, kutoa stakabadhi wanapouza bidhaa na huduma huku wananchi wakiaswa kudai stakabadhi wanapofanya manunuzi ya aina yoyote na kuhakikisha kuwa stakabadhi hizo zinaonesha kiasi halisi walicholipia huduma na bidhaa walizonunua.
Akizungumza kwa niaba ya Jumuiya ya Wafanyabiashara mkoani Kagera, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Seif Mkude, alipongeza jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano kwa namna inavyohamasisha na kushikia bango masuala ya kodi kwa manufaa ya Taifa.
Alisema kuwa wafanyabiashara wameridhika na namna kodi wanazolipa zinavyosimamiwa kikamilifu na kutekeleza miradi dhahiri ya maendeleo na kuahidi kuwa wataendelea kulipa kodi hizo ili  kujenga uchumi wa nchi.
Alitoa wito kwa wafanyabiashara wenzake kuendelea kulipa kodi kwa hiari ili kuunga mkono juhudi za Rais Dk. John Pombe Joseph Magufuli huku akiishauri Serikali kuondoa kero ndogo ndogo zilizotolewa na wafanyabiashara wakati wa mkutano huo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Kagera, Mkuu wa wilaya ya Bukoba, Deodatus  Kinawiro, aliwashauri wafanyabiashara hao kupanua wigo wa biashara zao ili waweze kunufaika na uwepo wa soko huru katika nchi zaidi ya nne zinazopakana na mkoa huo ikiwemo Uganda,  Rwanda, Burundi, DRC Kongo, Kenya na nchi nyingine.

No comments:

Post a Comment