Tuesday 30 August 2016

RAIS MAGUFULI SIYO DIKTETA- MANGULA


 
MAKAMA Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula amesema Rais Dk. John Magufuli siyo dikteta bali ni kiongozi mtiifu na mwadilifu, anayetekeleza maagizo ya Chama yaliyoko katika Ilani ya Uchaguzi  ya 2015-2020.

Amesema udikteta ni kuingia madarakani bila demokrasia, lakini Dk. Magufuli aliingia madarakani kwa uchaguzi uliopitia hatua mbalimbali, baada ya mchujo wa vikao vya Chama, ambapo alipatikana kutoka katika kundi la wanachama 42, waliomba kuteuliwa na CCM.

Mangula alisema hayo jana, alipozungumza na Uhuru, kuhusu maandamano ya CHADEMA, waliyoyabatiza jina la Umoja wa Kupinga Udikteta (UKUTA), yaliyopangwa kufanyika Septemba Mosi.

Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM alisema, baada ya kuteuliwa na CCM, Rais Dk. Magufuli alipita kwa wananchi kunadi Ilani ya Uchaguzi, ambapo watu zaidi ya milioni nane walikubaliana nayo na kumchagua kuwa Rais wa Tanzania.

“ Ushauri wangu kwa vijana wanaohamasishwa kujenga ukuta wa kufikirika barabarani, ni bora wakajenge kuta za shule,nyumba za walimu, watengeneze na madawati kama ilivyofanya CCM kutoa madawati zaidi ya 1,000,”alisema na kuongeza kuwa, Rais Dk. Magufuli anafanya kazi nzuri ya kutekeleza Ilani.

Alisema katika kifungu cha 13, cha Ilani ya Uchaguzi kinasema: “Katika kipindi cha miaka mitano, CCM itazielekeza serikali  zake zote  kupambana na rushwa  na kuchukua hatu dhidi ya kiongozi yeyote atakayejihusisha na rushwa.

“Serikali zote zitatakiwa kushughulikia kwa ukali zaidi tatizo la ubadhirifu wa mali za umma,” inaeleza sehemu hiyo ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2015-2020.

Mangula alisema katika kipindi kifupi, Rais Dk. Magufuli ametekeleza maagizo hayo kwa vitendo kwa kuwachukulia hatua watuhumiwa wa rushwa na wabadhirifu wa mali za umma, hivyo haiwezekani kumwita dikteta mtu mwadilifu, anayetekeleza Ilani iliyokubaliwa na Watanzania.

“Sioni hoja ya msingi ya kumwita Rais Dk. Magufuli dikteta wakati alichaguliwa kwa kura kuanzia ndani ya Chama hadi kwa wananchi.
Mgombea urais wa CHADEMA alipigiwa kura na nani na alipata kura ngapi katika uchaguzi wa ndani ya chama chao?”Alihoji Mangula.

Alisema kwa bahati mbaya, wanaodai demokrasia wenyewe hawana demokrasia hata kidogo, wakati CCM wanapokezana uongozi kila baada ya kipindi fulani. Alisema CHADEMA wamekuwa wakiendesha chama kama kampuni hadi viongozi wengine wanakerwa na kuamua kuondokana na siasa.

“CHADEMA walishindwa kutumia demokrasia kwenye uchaguzi wa 2015, hadi Katibu Mkuu wao, Dk. Willibroad Slaa akaondoka. Nafasi ya mwenyekiti kila wakati ni Freeman Mbowe. Hebu ajitokeze hadharani aseme kama chama chao hakina watu wengine wenye uwezo wa kuwa wenyeviti,” alisema.

Mangula aliongeza: “Hata James Mbatia, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, ambaye yuko kwenye kundi la UKAWA, tangu mwaka 1999 mpaka sasa yeye ndiye mwenyekiti. CUF nako hakuko salama, ndio maana Mwenyekiti wao, Profesa Ibrahimu Lipumba alijiuzulu baada ya kukerwa na utaratibu wa kumpata mgombea urais.”

Mangula alisema kinachofanywa na viongozi hao wakiwa madarakani ndiyo udikteta halisi.

Alisema CHADEMA wamekosa ajenda hivyo imekuwa kawaida yao kuzua mambo ya kuwaunganisha pamoja  na sio mara ya kwanza kwani iliwahi kuanzishwa Operesheni Sangara, M4C na zote hazikuwa na manufaa yoyote zaidi ya kuhamasisha vijana waingie barabarani, lakini wenyewe wanajificha.

“CHADEMA ajenda yao kubwa ilikuwa rushwa na ufisadi, lakini utendaji wa awamu ya tano umeshughulikia kwa vitendo kero hizo, hivyo hawana tena ajenda, ndio wamezua UKUTA, lakini hakuna hoja ya udikteta kwa Dk. Magufuli,”alisema.

Mangula alisema kama wana hoja ya msingi, CHADEMA walipaswa watumie Baraza la Vyama vya Siasa, ambalo lilizinduliwa rasmi na Rais mstafu Benjamin Mkapa, ambaye katika uzinduzi huo Julai 23, 2005, aliwasisitiza juu ya kulinda amani.

“Nakumbuka wakati analizindua baraza hilo, Mkapa alituleleza yafuatayo ‘Ni makosa makubwa na jambo la hatari kwa wanasiasa kupanda mbegu za chuki na uhasama ndani ya nyoyo za vijana wa Tanzania dhidi ya vijana wenzao wa Tanzania, eti kwa sababu za kisiasa.”


No comments:

Post a Comment