Sunday 28 August 2016

VIONGOZI WA DINI WAONYA VURUGU ZA SIASA




VIONGOZI waandamizi
wa dini wametoa ya moyoni
kuhusu vuguvugu la kisiasa
linazoendelea nchini na kuwaasa
Watanzania, kutomjaribu Rais
Dk. John Magufuli, badala
yake wape muda na nafasi ya
kuiongoza nchi.
Wakizungumza kwa nyakati
tofauti, baadhi ya viongozi hao
wamemtaja Rais Magufuli kuwa
ni kiongozi ‘aliyejitolea sadaka’ ili
kuivusha Tanzania kutoka hapa
ilipo.
Akizungumzia hali ya kisiasa
nchini na uongozi wa Rais
Magufuli, Kiongozi wa Kanisa
la Ufufuo na Uzima, Askofu
Josephat Gwajima, alisema Rais
Magufuli ni kiongozi mzalendo
mwenye kuchukua uamuzi
mgumu wenye tija kwa taifa.
Alisisitiza kuwa ni vyema
wananchi wakampa ushirikiano
na kumpa muda kiongozi
huyo, ili aweze kutimiza ahadi
alizoahidi kwa Watanzania.
“Sitasahau wakati Rais
Magufuli aliposema amejitoa
sadaka kwa taifa hili. Hii
inaonyesha kwa namna ya pekee,
ambavyo Rais wetu ana nia ya
dhati ya kufanyakazi kwa busara,
akili na nguvu zake zote ili taifa
hili lisonge mbele,” alisema
Askofu Gwajima.
Aliongeza kuwa anamuona
Rais Dk. Magufuli kuwa kiongozi
wa kipekee, anayepaswa
kuungwa mkono, badala ya
watu kujaribu kumzuia kwa
kufanya vitendo vinavyoashiria
uvunjifu wa amani, ikiwemo
maandamano yaliyotangazwa na
baadhi ya vyama vya siasa.
Akizungumzia maandamano
hayo yaliyotangazwa na
CHADEMA na kupangwa
kufanyika nchi nzima Septemba
Mosi, mwaka huu, Askofu
Gwajima aliwataka viongozi wa
dini kutumia nafasi zao vizuri
kwa kuhubiri amani, ikiwa ni
pamoja na kuwataka viongozi
wa vyama vya siasa kutafuta
suhulu ya tofauti zao kwa njia ya
mazungumzo.
Askofu Gwajima aliwaasa
vijana kuachana na maandamano
ya Septemba Mosi, badala yake
watumie siku hiyo kwenda
kufanyakazi za kujiletea
maendeleo.
Kwa upande wake, Mchungaji
wa Kanisa la Maombezi
(GRC), Mchungaji Anthony
Lusekelo, maarufu kama Mzee
wa Upako, alisisitiza kuwa ni
vyema Watanzania wakawa
wanyenyekevu kwa serikali kwa
vile unyenyekevu sio unyonge
bali ni hekima.
“Tusiharibu amani yetu
bali tuiangalie nchi hii. Mwaka
huu tuunganishe mioyo yetu
na tumpe nafasi Rais Magufuli
awatumikie Watanzania. Ni
mwaka wa kusameheana,’alisema
Mchungaji Lusekelo.
Aliongeza kuwa Tanzania ina
heshima yake, ambayo ni umoja
na upendo wa Watanzania na
dunia yote inafahamu, hivyo ni
vyema amani iliyopo ikalindwa
kwa nguvu zote.
Mchungaji Lusekelo alisisitiza
kuwa, kwa kuwa Tanzania ni
nchi yenye kufuata misingi
ya demokrasia, wanasiasa
wakubaliane kuwa wakati wa
kampeni na uchaguzi umepita na
kilichobaki ni kusaka maendeleo
na watu kuponya majeraha.
“Tusiharibu nchi yetu, sisi
ni matajiri na bila kuwepo
kwa amani hatutaweza kupata
maendeleo kupitia utajiri wa
rasilimali tulizonazo. Tusiweke
rehani amani ya taifa letu,”
alisema Mchungaji Lusekelo.
Kuhusu baadhi ya viongozi
wa vyama vya siasa, wanaotoa
maneno ya kumkashifu Rais
Magufuli, Mchungaji Lusekelo
alisema hata maandiko yanaonya
juu ya hilo.
“Watanzania hawapaswi
kuwasema vibaya viongozi wao,
bali watoe ushirikiano katika
kuwasaidia watekeleze vyema
majukumu yao,”alisema na
kuongeza:
“Viongozi nao wanapaswa
kutokuwa waoga katika
kuyasemea mambo ya nchi
na hasa kuhubiri amani.
Watanzania lazima waonyeshwe
jinsi ambavyo nchi zilizowahi
kukumbwa na machafuko
zilivyokithiri kwa umasikini kwa
sababu ya vita za wenyewe kwa
wenyewe”
Hivi karibuni, viongozi
wengine waandamizi wa dini,
akiwemo Sheikh Mkuu wa Mkoa
wa Dar es Salaam, Alhad Mussa
Salum, alisisitiza pia kuhusu
Rais Magufuli kupewa nafasi ya
kutekeleza ahadi zake, badala
ya baadhi ya wanasiasa kutaka
kumkwamisha.
Kauli ya Askofu Gwajima
na Mchungaji Lusekelo ni
mwendelezo wa matamko ya
kuwaasa viongozi wa vyama vya
upinzani nchini, kubadili mfumo
wa kuingiza siasa hata katika
masuala ya maendeleo kwa nia
ya kumpa muda Rais atekeleze
Ilani yake.

No comments:

Post a Comment