Sunday 28 August 2016

RAIS DKT MAGUFULI AHUDHURIA MISA YA JUBILEI YA DHAHABU (MIAKA 50) YA NDOA YA RAIS MSTAAFU BENJAMIN MKAPA NA ANNA MKAPA





Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William Mkapa leo tarehe 27 Agosti, 2016
ameadhimisha Jubilei ya Dhahabu ya Miaka 50 ya Ndoa yake na Mama Anna Mkapa
katika kanisa la Mtakatifu Petro lililopo Oysterbay Jijini Dar es Salaam.

Hafla ya Jubilei hiyo imefanyika nyakati za mchana katika ukumbi wa Kardinali Rugambwa uliopo kando ya kanisa la Mtakatifu Petro-Oysterbay na imetanguliwa na Misa ya
shukrani iliyofanyika katika kanisa hilo majira ya asubuhi.

Jubilei hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Mkewe Mama Janeth Magufuli, Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais Mstaafu wa Awamu ya Sita wa Zanzibar Dkt. Amani Abeid Karume, Mke wa Baba wa Taifa Mama Maria Nyerere, Mawaziri Wakuu Wastaafu Mhe. Cleopa Msuya, Dkt. Salim Ahmed Salim, Jaji Joseph Warioba na Mhe. Edward Lowassa.

Misa Takatifu ya Shukrani imeongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha Mhashamu Askofu Josephat Lebulu na kuhudhuriwa na Maaskofu na Maaskofu Wakuu saba akiwemo Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam Mwadhama Polycarp
Kardinali Pengo.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa Misa Takatifu Rais Magufuli amempongeza Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa kwa kutimiza miaka 50 ya ndoa na ameeleza kuwa ndoa hiyo iliyowaunganisha wanandoa wanaotoka katika madhehebu tofauti ya Kikristo imetoa
fundisho kubwa kuwa binadamu wanapaswa kuwa wamoja hata kama wana tofauti
mbalimbali zikiwemo za kimadhehebu ya dini, siasa na kanda.

Rais Magufuli amesema miaka 50 ya ndoa ya Mhe. Benjamin William Mkapa ambaye ni Muumini wa Kanisa Katoliki na Mkewe Mama Anna Mkapa ambaye ni Muumini wa Kanisa la Kilutheri inawafundisha watanzania wote hususani wanasiasa kuishi kwa upendo na
kuilinda amani waliyonayo na ametoa wito kwa viongozi dini kuendeleza juhudi
zao za kuliombea taifa na kuwaunganisha wananchi licha ya tofauti walizo nazo.

Kwa upande wake Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William Mkapa pamoja na kuwashukuru Viongozi wote, ndugu, jamaa na marafiki waliohudhuria Misa ya Shukrani na Jubilei hiyo ya miaka 50 ya ndoa yake amemshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuijaalia
ndoa yake umri mrefu.

Rais Mstaafu Mkapa pia ametoa wito kwa watanzania kupenda na kushirikiana huku akibainisha mafunzo aliyoyapata kutoka kwa viongozi wa dini kuwa "Kila mmoja ni zawadi kwa mwenzake"

Nae Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amempongeza Rais Mstaafu Mkapa na Mkewe Mama Anna Mkapa kwa kuadhimisha miaka 50 ya ndoa na amewasihi watanzania kuiga mfano mwema uliooneshwa na wana ndoa hao ambao wamedumu katika imani bila kuyumba.

Kardinali Pengo amesema ndoa ya Rais Mstaafu Mkapa anaifundisha jamii kuwa tunaweza kuishi kwa imani zetu bila kubadili dini.

Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Petro  Fr. Stephano Kaombwe akiongoza Ibada ya

ukumbusho wa ahadi za ndoa wakati wa Misa ya Jubilei ya Dhahabu (miaka 50) ya ndoa ya Rais Mstaafu Mhe Benjamin Mkapa na Mama Anna Mkapa katika kanisa la Mt. Petro
jijini Dar es salaam leo Jumamosi Agosti 27, 2016

Rais Mstaafu Mhe Benjamin Mkapa na Mama Anna Mkapa wakipokea hati maalumu kutoka kwa Baba Mtakatifu  Francis  toka kwa  Askofu  Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo  wakati wa Misa ya Jubilei ya Dhahabu ya ndoa ya Rais Mstaafu Mhe Benjamin Mkapa na Mama Anna Mkapa katika kanisa la Mt. Petro jijini Dar es salaam leo Jumamosi Agosti 27, 2016

Rais Mstaafu Mhe Benjamin Mkapa akitoa shukurani  wakati wa Misa ya Jubilei ya Dhahabu ya ndoa yake na Mama Anna Mkapa katika kanisa la Mt. Petro jijini Dar es salaam leo Jumamosi Agosti 27, 2016

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli akitoa salamu zake za pongezi wakati wa Misa ya Jubilei ya Dhahabu ya ndoa ya Rais Mstaafu Mhe Benjamin Mkapa na Mama Anna Mkapa katika kanisa la Mt. Petro jijini Dar
es salaam leo Jumamosi Agosti 27, 2016

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli katika picha ya pamoja viongozi wa dini na viongozi wastaafu na wake zao  wakati wa Misa ya Jubilei ya
Dhahabu ya ndoa ya Rais Mstaafu Mhe Benjamin Mkapa na Mama Anna Mkapa
katika kanisa la Mt. Petro jijini Dar es salaam leo Jumamosi Agosti 27,
2016

Rais Mstaafu Mhe Benjamin Mkapa na Mama Anna Mkapa  wakikata keki  katika hafla ya chakula cha mchana waliyoandaa baada ya Misa ya Jubilei ya Dhahabu ya ndoa yao  katika kanisa la Mt. Petro jijini Dar es salaam leo Jumamosi Agosti 27, 2016.

No comments:

Post a Comment