Wednesday, 12 October 2016

BAKHRESSA KUONGEZA VIWANDA VYA MATUNDA

KAMPUNI ya Bakhresa Foods, imedhamiria kuongeza viwanda vingine vya usindikaji matunda hapa nchini ili kuongeza thamani kwa mazao ya wakulima.

Ahadi hiyo ilitolewa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Said Bakhersa,alipokutana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na kufanya naye mazungumzo ofisini kwake, Magogoni jijini Dar es Salaam.

Bakhresa alisema wana mpango wa kujenga kiwanda kimoja kwenye mikoa ya kanda ya ziwa na kwamba, wamefikia uamuzi huo baada ya kubaini kuwa watu wanapata usumbufu wa kusafirisha matunda kutoka ukanda huo hadi Dar es Salaam, kwa ajili ya soko.

"Kuanzia Oktoba 15, tutaanza kupokea matunda kutoka Kahama na maeneo ya jirani na kwa siku tunapata semi trela zaidi ya 30. Yakimalizika ya kule, tunaanza kupokea mengine kutoka mikoa ya Pwani na Kusini.

“Hivyo tukijenga kiwanda kanda ya ziwa, tutapunguza adha ya wadau kusafirisha matunda kutoka kule hadi hapa kiwandani, badala yake sisi tutakuwa tunasafirisha juisi iliyosindikwa na kuileta hapa kwa hatua zaidi za usindikaji,” alisema.

Mkurugenzi huyo alisema wana mpango wa kuendeleza usindikaji wa vyakula vya nafaka kwenye mikoa ya kusini na kwamba, hadi sasa wameajiri wafanyakazi zaidi ya 8,000, wakiwemo Watanzania 180, ambao wako kwenye matawi yake nje ya nchi.

Alisema hadi kufikia sasa, kampuni hiyo imekwishafungua matawi mengine kwenye nchi za jirani na Tanzania, ikiwemo Rwanda, Burundi, Msumbiji, Malawi, Zimbabwe na Afrika Kusini.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu Majaliwa alimhakikishia Bakhresa kuwa, nia ya serikali ya awamu ya tano ni kushirikiana na wafanyabiashara na wamiliki wa viwanda kwa sababu imedhamiria kukuza uchumi wa Tanzania kupitia uzalishaji wa viwandani.

“Serikali inathamini mchango wa wenye viwanda katika nchi yetu. Tunawashukuru ninyi, ambao ni wakongwe kwenye sekta hii, kwa hiyo tunawaomba msikate tamaa, muendelee kufungua viwanda zaidi ili wananchi wetu wapate mahali pa kuuzia mazao au bidhaa zao,”alisema.

Alimuomba mfanyabiashara huyo aangalie maeneo mengine zaidi ya kuwekeza kama vile sekta za hoteli na utalii ili kusaidiana na serikali kukuza uchumi wa Tanzania.

Kampuni ya Bakhresa Foods, inatengeneza vyakula zikiwemo juisi, soda, maji, biskuti, ice-cream, vyakula vya nafaka kama ngano, mahindi, mchele na bidhaa za kuokwa.

No comments:

Post a Comment