Sunday 23 October 2016

SERIKALI YAILIPA NSSF DENI LA BILIONI 722


SERIKALI imesema imelilipa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), deni la sh. bilioni 722.7, kati ya deni la michango iliyokuwa inadaiwa, ambayo ni sh. bilioni 964.2.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, wakati akifungua mkutano wa sita wa wadau wa mfuko huo, uliofanyika jijini hapa.

Alisema serikali inakamilisha uhakiki wa madeni ya miradi ya mifuko ya hifadhi ya jamii ili iweze kutoa hati fungani.

Majaliwa alisema kiasi cha fedha kilichosalia, ambacho serikali inadaiwa, inaendelea kufanya mchakato kwa ajili ya kuhakikisha fedha hizo zinalipwa ili ibaki bila deni lolote wanalodaiwa na mfuko huo.

Aidha, aliwataka waajiri nchini kuheshimu sheria na kuwasilisha michango ya watumishi wao kwa wakati ili kuepuka usumbufu wanaoupata wanachama baada ya kustaafu, kutokana na waajiri wengi kutokupeleka michango kwa wakati, jambo ambalo halikubaliki kisheria.

“Kuna changamoto kubwa ya waajiri nchini kutolipa michango yao kwa wakati. Nitoe wito kwa waajiri wote nchini kulipa kwa wakati na watambue kuwa mafanikio ya mfuko yanatokana  na michango kuwasilishwa kwa wakati,”alisema.

Waziri Mkuu alimwagiza Mkurugenzi Mkuu wa NSSF,  Profesa Godius Kahyarara, kuwaandikia barua wadaiwa wote walionunua nyumba za NSSF pamoja na wapangaji, ambao hawalipi kodi kwa wakati na wawape tarehe maalumu ya kulipa fedha hizo na endapo hawatatekeleza agizo hilo, wachukulie hatua kali za kisheria.

“Kuna watu walionunua nyumba za NSSF na hawataki kulipa fedha wanazodaiwa pamoja na wapangaji sugu. Nakuagiza mkurugenzi mkuu kuwaandikia barua walipe fedha hizo na watakaogoma, hatua za kiesheria zichukuliwe mara moja dhidi yao na mimi nipate taarifa ya hatua zilizochukuliwa,”alisema.

Majaliwa alisema NSSF imeanza mchakato wa kujenga Kiwanda cha Sukari mkoa wa Morogoro, eneo la Mkulazi, ambacho kitazalisha tani 200,000, kwa mwaka pamoja na kutoa ajira kwa vijana  100,000.

Alisema licha ya mfuko huo kuwekeza katika kiwanda hicho, pia umetoa mkopo wa sh. bilioni 3.1, kwa Kiwanda cha Kuzalisha Viuatalifu kilichoko Kibaha mkoani Pwani, lengo likiwa ni kuongeza uzalishaji katika sekta ya kilimo nchini .

Licha ya mkopo huo, Majaliwa alisema NSSF imetoa mkopo wa sh. bilioni 3.67, kwa bodi ya nafaka na mazao mchanganyiko  kwa ajili ya kuwezesha ukuzaji wa biashara kwenye nafaka.

Kuhusu suala la uwiano wa kiwango cha kukatwa mwanachama na kile anachoongeza mwajiri, Waziri Mkuu alimwagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge,Kazi, Vijana, Ajira na  Ulemavu pamoja na Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Mifuko ya Jamii nchini (SRAA), kusimamia suala hilo pamoja na kuweka mazingira mazuri ya ushindani wa haki.

Awali, Profesa Kahyarara alisema kauli mbiu ya mkutano huo ni hifadhi ya jamii na maendeleo ya viwanda, mwelekeo katika kukuza uchumi na ajira nchini, ambapo wameanza kuwekeza katika vinu vilivyokuwa vya Shirikala Taifa la Usagishaji na Mafuta ya Alizeti pamoja na kusaga na kukoboa mahindi.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NSSF, Profesa Samwel Wangwe , alisema wametoa kiasi sh. milioni 500, kwa ajili ya shule ya sekondari ya Lindi, iliyoungua kutokana na hitilafu ya umeme.

Profesa Wangwe alimkabidhi Waziri Mkuu, Majaliwa, tani  45 za saruji, sawa na mifuko 900, yenye thamani ya sh. milioni 15, kwa ajili ya kusaidia waathirika wa tetemeko la ardhi lililotokea hivi karibuni katika mkoa wa Kagera.

No comments:

Post a Comment