RAIS mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, amewataka Watanzania kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi, ikiwezekana kila siku, kwa sababu ndiyo yamemfanya awe imara na madhubuti mpaka sasa.
Amesema licha ya kuwa na umri wa zaidi ya miaka zaidi ya 90, amekuwa akifanya mazoezi mara kwa mara na kwa takriban 40 sasa, hajawahi kupatwa na ugonjwa wowote.
“Wosia wangu kwenu wenye umri wa wanangu na wajuu wangu, nawausia mfanye mazoezi msichoke, ikiwezekana kila siku. Kama hauwezi, basi ufanye kwa wiki mara moja, mbili au tatu, hii inatokana na manufaa ya mazoezi.
“Mfano halisi wa manufaa hayo ni kwangu mimi. Huu ni mwaka wa 40, sijapa homa, niko mzima, madhubuti. Kwa mwaka 40, nimeonesha kitu gani naweza kuwa na nyie nakutamanieni muwe kama mie,” alisema Mzee Mwinyi, jana, alipokuwa akizindua Wiki ya Utoaji Elimu ya Sheria, ambayo yanakwenda sambamba na Maonesho ya Sheria, katika viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam.
Kabla ya kuzindua wiki hiyo, Mzee Mwinyi aliongoza matembezi yaliyoshirikisha wadau mbalimbali wa sheria na vikundi vya michezo, yaliyoanzia viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kuishia viwanja vya Mnazi Mmoja.
Rais mstaafu Mwinyi aliipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kuadhimisha Wiki ya Utoaji Elimu ya Sheria kwa miaka mitatu mfululizo, tangu Februari mosi, 2015, ambapo yamekuwa yakifanyika sambamba na mazoezi.
Alisema taasisi hiyo inastahili pongezi hizo kwa kuanzisha jambo hilo lenye mafanikio makubwa na kuliendeleza na ni matumaini yake kwamba, kwamba litakuwa endelevu.
“Mahakama imeanzisha utamaduni mzuri wa matembezi, lengo likiwa ni kupasha miili moto, hivyo wananchi wanapaswa kujua manufaa ya matembezi au mazoezi, kwani mie leo nipo hapa sauti yangu inasikika bila ya kukwaruza na nimesoma hotuba bila ya kuvaa miwani, yote hayo ni kwa sababu ya mazoezi,” alisema.
Aliongeza: “Umri wangu unazidi miaka 90, nasema, nasikika, mmeniona nikisoma hotuba sina miwani, nimeshirikiana nanyi katika mazoezi makali, haya ni manufaa ya mazoezi. Kwa miaka 40 sasa, nimekuwa nikifanya mazoezi, yakiwemo ya baisheki na sijapata homa, hamjasikia Mwinyi yuko hospitali, mkinialika mazoezi nakuja kufanya, kisa nafanya mazoezi.”
Mzee Mwinyi alisema mwaka jana, alikwenda kufanya uchunguzi wa afya yake, ambapo daktari alimweleza kuwa moyo wake bado ungali wa kitoto na alipokwenda kwa daktari wa macho, naye alimwambia bado ni ya kitoto, ndio maana amesoma hotuba bila ya kuvaa miwani.
Mbali na hilo, alisema mazoezi ni njia mojawapo ya kupunguza msongo wa mawazo, hujenga akili na kufanya akili kuwa timamu, hivyo aliwasihi wananchi iwe desturi yao kufanya mazoezi mara kwa mara, badala ya kusubiri matembezi ya Wiki ya Utoaji Elimu ya Sheria.
Akizungumzia kuhusi wiki hiyo, Mzee Mwinyi alisema wananchi wengi wamekuwa hawana uelewa kuhusu masuala ya sheria na taratibu za mahakama, hivyo wengine kuamua kujichukulia sheria mkononi.
“Wananchi wengi hawana uelewa juu ya sheria na taratibu za mahakama, hawajui haki zao na hatua za kuchukua, hivyo kuamua kujichukulia sheria mkononi,” alisema.
Aliongeza kuwa, wananchi ambao wamekuwa hawaridhika na uamuzi, lakini kutokana na kutoelewa hatua za kufuata, huamua kwenda katika ofisi za Mkuu wa Wilaya, badala ya kukata rufani.
“Njia sahihi iwapo mtu hajaridhika na uamuzi ni kukata rufani. Nategemea mtawafundisha wananchi taratibu za kukata rufaa,” alisema na kuongeza kuwa, waendelee kutenga muda wa kupokea kero, kuzichambua na kuzijadili.
Alisema hatua ya Mahakama ya Tanzania kuanzisha wiki hiyo na maonesho, ambayo yanawashirikisha wadau mbalimbali wa sheria, itawawezesha wananchi kuelimishwa kuhusu masuala ya kisheria.
Alitoa wito kwa wananchi kufika katika viwanja mbalimbali
vilivyoandaliwa katika kuadhimisha wiki hiyo, kwa ajili ya kuwasilisha kero zao na matatizo yao ili yaweze kupatiwa ufumbuzi.
Alisema elimu itakayotolewa katika kuadhimisha wiki hiyo, itagusa masuala, ambayo ni kero kubwa katika jamii, yakiwemo ya taratibu za kukata rufaa, unyanyasaji wa kijinsia, ndoa na mirathi.
Alisema ni mategemeo yake kwamba, wananchi wataelimishwa kuhusu taratibu za kukata rufani.
Awali, akimkaribisha mgeni rasmi, Kaimu Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Profesa Ibrahim Juma, alisema sheria ina umuhimu mkubwa sana katika nchi na ni lazima ilenge katika kumnufaisha mwananchi.
Alisema wakati wa kuadhimisha wiki hiyo, lazima jamii kwa ujumla itafakari na kuangalia umuhimu wa sheria.
Kaimu Jaji Mkuu huyo alitoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika maadhimisho hayo ili wapate fursa ya kujifunza, kueleza malalamiko yao na madukuduku yao ili yaweze kufanyiwa kazi na kuelewa mpango mkakati wa mahakama wa miaka mitano inaoutekeleza.
“Hii ni mahakama ya wananchi wa Tanzania, imani ya wananchi katika mahakama ni kitu muhimu sana, tunajaribu kujenga imani hiyo, hivyo mkiona mahakama haiendi na maadili, simu zipo, msisite kutuambia ili tuweze kujirekebisha,” alisisitiza.
No comments:
Post a Comment