Friday, 24 February 2017
ASKOFU DK. MOKIWA AKIMBILIA KORTINI
ALIYEKUWA Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam, Dk. Valentino Mokiwa, amefungua kesi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akiiomba itengue uamuzi wa kuvuliwa uaskofu na kumtangaza kuwa askofu.
Dk. Mokiwa kwa kupitia kampuni ya uwakili ya M. B Kabunga and Co. Advocates, Mathew Kabunga, alifungua kesi hiyo namba 20, ya mwaka huu, dhidi ya Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk. Jacob Chimeledya na bodi ya wadhamini ya kanisa hilo, akipinga kuvuliwa uaskofu.
Shauri hilo lililoko mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, limepangwa kutajwa mahakamani hapo Februari 28, mwaka huu. Mawakili wa kanisa hilo, Gabriel Masingwa na Emmanuel Nkoma, jana nao walitinga mahakamani hapo.
Mawakili hao walifika mbele ya Hakimu Simba, wakidai kwamba walipewa maelezo ya kutakiwa kufika mahakamani hapo, ambapo Hakimu Simba alisema katika kumbukumbu za kesi, shauri hilo limepangwa Februari 28, mwaka huu.
Mawakili hao walieleza kuwa walipatiwa barua kutoka na wakili wa Dk. Mokiwa, M. B Kabunga. Hata hivyo, upande wa mlalamikaji hawakuwepo mahakamani hapo licha ya kuwapatia walalamikaji barua ikionesha kwamba, kuna jitihada za kumaliza mgogoro huo katika nyumba ya maaskofu.
“Hapa mahakamani kuna hati ya madai na hati ya kujibu madai na kesi ilishapangwa kuja Februari 28, mwaka huu, hivyo kwa leo siwatambui na siwezi kuingiza chochote katika kumbukumbu za mahakama,” alisema Hakimu Simba.
Kwa mujibu wa barua hiyo kutoka kwa wakili wa Dk. Mokiwa, anaomba tarehe ya kutajwa kwa shauri hilo irudishwe nyuma kwa kuwa kuna juhudi za kutatua mgogoro katika nyumba ya maaskofu.
Barua hiyo inaeleza kutokana na hilo, wakili huyo ameelekezwa na mteja wake kuondoa shauri hilo mahakamani kwa kuwa utaratibu wa kumaliza mgogoro huo hauwezi kufanyika isipokuwa kuondoa kesi.
Dk. Mokiwa baada ya kufungua kesi hiyo, mawakili wa kanisa hilo, waliamua kuwasilisha mahakamani hapo majibu yao, wakiiomba kuitupilia mbali kesi hiyo kwa kuwa haina mamlaka ya kuisikiliza.
Kwa kupitia hati yake ya maadai, Dk. Mokiwa anadai kwamba waumini takriban 28, wa kanisa hilo, waliandika barua ikiwa na mashitaka 10, dhidi yake, lakini barua hiyo haikuwasilishwa kwake na ilionesha kuna nakala.
Anadai kwamba Desemba 20, mwaka jana, mlalamikiwa wa kwanza (Dk. Chimeledya) alimuandikia barua kumtaka kustaafu mwenyewe katika nafasi yake bila ya kueleza sababu na kumpa nafasi ya kuweza kujibu tuhuma.
Kwa kupitia hati yake ya madai, Dk. Mokiwa anadai kwamba, tuhuma hizo hazina vielelezo vyovyote vya kuzithibitisha, bali ni mambo ya kupika kumuharibia askofu huyo. Kutokana na hayo, anaiomba mahakama kuamuru Dk. Mokiwa ni askofu halali, kumlipa gharama za kesi na kutoa amri nyingine inazoona zinafaa.
Katika hati yao ya majibu, walalamikiwa hao wanadai hati ya madai haipo sahihi mahakamani hapo, kwa kuwa haina uwezo wa kuingilia masuala ya kiimani kwani yanapaswa kusikilizwa na kutafutiwa ufumbuzi kwenye vyombo vya kidini.
Aidha, wanadai kitendo cha Dk. Mokiwa kufungua kesi hiyo mahakamani ni kwenda kinyume na Katiba ya Kanisa la Anglikana ya mwaka 1970, ambayo ilifanyiwa marekebisho Oktoba, 2014.
Januari 7, mwaka huu, Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk. Chimeledya alimvua uaskofu mkuu Dk. Mokiwa, kutokana na mashitaka 10, aliyofunguliwa na walei 32, wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam, yakiwemo ya ufisadi wa mali za kanisa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment