Friday, 24 February 2017
RUFANI YA NANGOLE YATUPILIWA MBALI
MAHAKAMA ya Rufani Tanzania, inayoendelea na vikao vyake Jijini hapa, imetupa rufani ya ubunge wa Jimbo la Longido, iliyofunguliwa na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Onesmo Nangole (CHADEMA) dhidi ya Steven Kiluswa (CCM) na wenzake wawili.
Akisoma uamuzi wa mahakama hiyo jana, mahakamani hapo, Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Amir Msumi, alisema jopo la majaji hao lilipitia kwa kina hoja za kisheria za pande zote mbili na kubaini pingamizi lililowasilishwa na mawakili wa upande wa mjibu maombi, wakiongozwa na Dk. Masumbuko Lamwai, kuwa mawakili wa waleta maombi walikiuka maagizo yaliyotolewa na mahakama hiyo ya kuwataka kuwaongeza Mwanasheria Mkuu wa Serikali na aliyekuwa Msimamizi wa Uchaguzi.
Kwa mujibu wa Msumi, jopo hilo la majaji baada ya kupitia matoleo mbalimbali ya kamusi ya lugha ya Kiingereza kutafuta tafsiri halisi ya neno “Amend”, ambalo lilitumika wakati wa kutoa maelekezo hayo, walibaini kwamba mawakili wa upande wa utetezi hawakwenda kufanya marekebisho,
badala yake waliamua kuandika rufani hiyo upya.
Alisema baada ya Mahakama kujiridhisha kuwa mawakili wa upande wa mleta maombi wakiongozwa na Method Kimomogoro, walikiuka maagizo ya Mahakama pamoja na kanuni namba 96 ya Mahakama ya Rufaa Tanzania, mahakama hiyo imetupilia mbali rufani hiyo.
Msajili huyo pia alisema Mahakama hiyo imewaagiza mawakili wa upande wa mleta maombi kulipa gharama za wakili mmoja wa upande wa mjibu maombi, badala ya mawakili watatu kama ilivyoombwa awali.
Awali akiwasilisha pingamizi mbili za kuwezesha rufaa hiyo kutupwa mbele ya jopo la majaji watatu, chini ya Mwenyekiti wake, Jaji Bernad Luanda, Jaji Musa Kipenga na Jaji Stella Mugasha, Wakili Dk. Masumbuko Lamwai akisaidiwa na Edmond Ngemela na Daud Haraka, alidai kuwa rufaa hiyo ina mapungufu makubwa ya kisheria.
Kwa mujibu wa Dk. Lamwai, mawakili wa mleta maombi waliagizwa na mahakama hiyo kuwaongeza Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na aliyekuwa Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi katika jimbo la Longido kwenye hati yao ya maombi.
Dk. Lamwai alidai badala ya kufuata maelekezo ya mahakama kwa mujibu wa kanuni namba 96 ya Mahakama ya Rufaa, mawakili wa mleta maombi wamefanya marekebisho makubwa katika rufaa hiyo bila kibali cha mahakama hiyo.
“Waheshimiwa majaji mliwaelekeza wakili wa mleta maombi kumuongeza Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na aliyekuwa Msimamizi wa Uchaguzi kama tulivyoiomba mahakama hii tukufu, lakini cha ajabu mawakili wasomi wenzangu wamekiuka na kufanya marekebisho makubwa bila kibali cha mahakama na kusababisha ongezeko la vitabu kutoka saba hadi nane vyenye mwenendo mzima wa rufaa hii.
“Marekebisho hayo yamesababisha kumbukumbu za awali kabla ya kuongeza majina hayo na baada ya kuongeza kuwa vitu viwili tofauti, kufuatia maneno mengi ya ujanja ujanja waliyoyaongeza bila kibali cha mahakama hii tukufu.
Kufuatia ukiukwaji huu wa sheria, tunaiomba mahakama hii itupilie mbali rufaa hiyo pamoja na kulipa gharama za mawakili watatu wa mjibu maombi,” alidai.
Akiwasilisha pingamizi la pili, Dk Lamwai aliieleza mahakakama hiyo kuwa mawakili wa mleta maombi pia walikiuka kanuni ya 96 (1) (B) ya kutoonyesha anuani wakati wa kuwapatia nakala ya rufaa hiyo.
NJE YA MAHAKAMA
Akizungumza nje ya mahakama hiyo, Dk. Kiluswa aliishukuru mahakama hiyo kwa kumtendea haki na kwamba, haki yake haijachelewa, na mhilimili wa mahakama umeonyesha dhahiri jinsi unavyofanya kazi kwa kuzingatia sheria katika kutenda haki.
Dk.Kiluswa alisema Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ilitenda haki kwa kutengua ubunge wa Nangole, lakini hakuridhika na kuamua kukata rufaa na leo mahakama imedhihirisha kuwa njia ya muongo ni fupi, mbio zake zimeishia hapo.
“Naishukuru Mahakama ya Rufaa Tanzania kwa kutenda haki, haki yangu haijacheleweshwa naishukuru pia Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kwani ilitenda haki, lakini mwenzangu Nangole hakuridhika, kaamua kukata rufaa na leo mbio zake zimeishia hapa, njia ya muongo siku zote ni fupi," alisema.
Kwa upande wake, Wakili wa Utetezi, Kimomogoro, alidai bado anatafakari kutupwa kwa rufaa hiyo na kwamba, atawasiliana na mteja wake ili washauriane kama wataomba kukata rufaa nje ya muda.
WANANCHI WALONGA
Wakizungumza nje ya mahakama hiyo, wananchi waliohudhuria katika kesi hiyo kutoka jimbo la Longido, wamemtaka Nangole kukubaliana na rufaa hiyo na kuacha uchaguzi kurudiwa kama Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ilivyoelekeza awali na maamuzi yatapatikana kwenye sanduku la kura.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Emmael Kiluswa, alisema mahakama imedhihirisha kuwa Nangole hakushinda kihalali na kama anataka kupata haki yake, akubali arudi kwa wananchi uchaguzi ufanyike.
Kiluswa alisema wananchi wa jimbo hilo kwa zaidi ya miaka miwili sasa hawanana mwakilishi wa kuwasemea bungeni na kwamba, wanakosa maendeleo kutokana na Nangole kutoridhika na maamuzi ya Mahakama.
“Wananchi wa jimbo la Longido tuna kiu kubwa ya maendeleo. Tunakabiliwa na changamoto nyingi, hakuna mtu wa kutusemea bungeni, ninachomuomba Nangole akubali turudi kwa wananchi ili waaamue kupitia sanduku la kura nani atawawakilisha bungeni,” alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment