KUNDI la majambazi wenye silaha limewapiga risasi na kuwaua OC CID wa Wilaya ya Kibiti, Peter Kubezya na watu wengine wawili katika Kijiji cha Jaribu Mpakani.
Mauaji hayo yalitokea saa 4 usiku wa kuamkia jana ambapo majambazi hayo yapatayo sita, yakiwa na silaha aina ya SMG na SRA walivamia kituo cha ukaguzi wa mazao ya misitu.
Taarifa zilieleza kuwa OC CID huyo aliuawa kwa kupigwa risasi kiunoni wakati wa majibizano ya kurushiana risasi kwenye eneo la tukio.
Wengine waliouawa ni Mkaguzi Maliasili wa kituo hicho, Peter Kitundu na askari mgambo Shaban Ngambob ambapo wote waliuawa kwa kupigwa risasi kichwani na begani.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Boniventure Mushongi, baada ya tukio hilo majambazi hayo yaliwaita wananchi kuiba mkaa na mazao ya misitu, wito ambao baadhi yao waliuitikia kwa kuiba mazao hayo.
“Baada ya kutokea kwa tukio hilo, kundi la makachero lililokuwa likiongozwa na OC CID Kubezya lilifika eneo hilo kwa lengo la kupambana na wahalifu hao.
“Wakiwa kwenye majibizano hayo mkuu huyo wa upelelezi alijeruhiwa kiunoni ambapo alifariki dunia akiwa njiani akipelekwa Hospitali ya Mission ya Mchukwi, " alieleza Mushongi.
Kamanda Mushongi alifafanua kwamba katika eneo la tukio kulikutwa pikipiki mbili zenye namba za usajili MC 853 AHH aina ya Toyo na MC 799 aina ya Sunlag na kipeperushi chenye ujumbe wa kitisho.
Kutoka vyanzo mbalimbali huko Kibiti vinasema vipeperushi hivyo vinaeleza kupinga kuwepo kwa vizuizu vya mazao ya misitu wilayani humo.
No comments:
Post a Comment