Tuesday, 21 February 2017

MAHAKAMA KUU YAZUIA MBOWE KUKAMATWA


MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, imetoa zuio la muda la kutomkamata Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, hadi maombi yake ya kutaka kutokamatwa na kuwekwa kizuizini yatakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.

Hatua hiyo inatokana na jopo la majaji watatu wa mahakama hiyo, likiongozwa na Jaji Sekiet Kihiyo, kukubaliana na ombi lililowasilishwa na mawakili wa Mbowe la kutaka hali ibaki kama ilivyo hadi hapo maombi aliyoyawasilisha yatakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.

Hayo yalijiri mahakamani hapo jana, wakati kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na Mbowe dhidi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (Paul Makonda), Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam (Simon Sirro) na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa kanda hiyo (Camillius Wambura) na maombi aliyoyawasilisha yalipotajwa mbele ya jopo hilo.

Majaji wengine walioketi kusikiliza shauri hilo ni Jaji Lugano Mwandambo na Pellagia Khaday, ambapo Mbowe alihudhuria kesi hiyo akiwakilishwa na mawakili Tundu Lissu, Peter Kibatala, Albert Msando, John Mallya, Faraji Mangula na Omary Msemo huku Wakili wa Serikali Mkuu, Gabriel Malata akitinga kuwawakilisha Makonda na wenzake.

Mbowe kwa kupitia mawakili wake, alifungua mahakamani hapo kesi ya kikatiba namba moja, baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kumtaja katika orodha ya watu 65, wanaojihusisha na dawa za kulevya katika mkoa huo na kutakiwa kufika katika kituo cha polisi kati. Hata hivyo, Mbowe alikaidi na kupewa saa 48, kujisalimisha polisi, ambapo juzi alitiwa mbaroni.

Baada ya kufungua shauri hilo, Mbowe aliwasilisha maombi mahakamani hapo akiiomba itoe zuio la kukamatwa na kuwekwa kizuizini kusubiri usikilizwaji wa kesi yake ya kikatiba na kutolewa uamuzi.

Jana, mbele ya jopo la majaji hao, mawakili wa Mbowe, wakiongozwa na Lissu, waliiomba mahakama hali ibaki kama ilivyo kusubiri usikilizwa na uamuzi wa maombi ya zuio la kukamatwa na kuwekwa kizuizini.

Baada ya kusikiliza maombi hayo, Jopo hilo lilitoa zuio la muda la kukamatwa Mbowe hadi maombi yake yatakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.

“Mahakama inaamuru hali ibaki kama ilivyo, mpaka maombi yatakaposikilizwa na kutolewa uamuzi,” lilisema jopo hilo na kuongeza kuwa, polisi waendelee na uchunguzi wao. Maombi hayo yamepangwa kusikilizwa keshokutwa.

Wakati huo huo, Jopo hilo lilikubaliana na ombi la Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) la kuingizwa katika kesi hiyo na kuamuru Mbowe kufanya marekebisho ya hati yake ya madai.

Ombi hilo lilikubaliwa baada ya kuibuka mabishano ya kisheria baina ya mawakili wa Mbowe na Wakili wa Serikali Mkuu, Malata kutoka ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, aliyefika mahakamani hapo kwa ajili ya kuwatetea mkuu wa mkoa na wenzake.

Malata alipofika mahakamani hapo, alieleza kwamba yuko kwa ajili ya wajibu maombi, hoja ambayo ilipingwa na mawakili wa Mbowe kwa madai si mmoja wa walalamikiwa katika hati ya madai.

Hata hivyo, Malata alidai licha ya kwamba AG sio sehemu ya walalamikiwa kwa kuwa waliolalamikiwa sio mtu binafsi bali ni mkuu wa mkoa, kamanda wa polisi na mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai, hivyo ana mamlaka ya kuwawakilisha.

Jopo hilo la majaji lilikubaliana na ombi la mwanasheria mkuu wa serikali na kumruhusu Mbowe kufanya marekebisho ya hati ya madai kwa kumuungiza kama sehemu ya walalamikiwa.

Jopo hilo limeamuru hati ya madai iliyofanyiwa marekebisho iwasilishwe mahakamani hapo Februari 27, mwaka huu na upande wa serikali wapatiwe Februari 28, mwaka huu na kuwasilisha majibu yao Machi 6, mwaka huu na shauri hilo litatajwa Machi 8, mwaka huu.

Mbowe alifika mahakamani hapo mapema asubuhi kwa kutumia gari aina ya Toyota Landcruiser lenye namba T 830 DEW, huku umati wa wanachama wa chama hicho na viongozi wakifika mahakamani hapo.

Mwenyekiti huyo wa CHADEMA na kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni, alikuwa miongoni mwa watu 65, waliotajwa na Makonda na kutakiwa kufika polisi kwa tuhuma za kujihusisha na dawa za kulevya.

Hata hivyo, Mbowe alikaidi agizo hilo akidai kuwa mkuu wa mkoa hana mamlaka ya kumwamuru aende polisi.

Februari 18, mwaka huu, Kamishna wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Sirro alimtaka Mbowe kujisalimisha na asipofanya hivyo polisi itatumia nguvu kumkamata.
 

No comments:

Post a Comment