Tuesday, 21 February 2017

UVCCM YAPONGEZWA KWA KUWANYOOSHA WAPOTOSHAJI



KATIBU wa Halmashauri Kuu Taifa (NEC) ya CCM, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (SUKI), Kanali mstaafu Ngemela Lubinga, ameupongeza Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) na kusema bado una kazi kubwa ya kuwanyoosha wanasiasa wapotoshaji.

Amesema licha ya kazi kubwa iliyofanywa na umoja huo katika uchaguzi mkuu, bado una jukumu la kuhakikisha unasafisha uchafu wa upotoshaji unaofanywa na wanasiasa wanaopotosha ukweli wa mambo mbalimbali yenye maslahi ya taifa.

Aidha, ameitaka UVCCM na Watanzania wote kuelekeza nguvu zao kuunga mkono juhudi za kupambana na dawa za kulevya kwa kuwa jambo hilo ni la kitaifa.

Akizungumza na viongozi wa UVCCM, walioongozwa na Kaimu Katibu Mkuu wa umoja huo, Shaka Hamdu Shaka, jana, Dar es Salaam, Kanali Lubinga alisema UVCCM ilifanya kazi kubwa wakati wa uchaguzi hadi kufanikisha ushindi wa CCM.

"Kila mmoja anatambua kuwa uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka 2015, haukuwa rahisi na utabaki katika historia. Lakini nakupongezeni UVCCM kwa kazi kubwa mliyoifanya.

"Haikuwa kazi rahisi kama ambavyo kila mmoja alishuhudia, lakini mwisho tulichohitaji ni ushindi wa CCM, ambao ulipatikana tena kwa kishindo,"alisema.

Kanali mstaafu Lubinga alisema anaziona na kutambua juhudi zinazofanywa na UVCCM katika kukabiliana na upotoshaji wa mambo mbalimbali na kusema hilo ni miongoni mwa majukumu ya vijana wa Chama.

"Nakupongeza hasa wewe Kaimu Katibu Mkuu kwa kazi unayoifanya. Endelea hiyo ndio kazi ya UVCCM,"alisema.

Aliutaka umoja huo kuwabana wanasiasa wapotoshaji wanaogeuka kama kinyonga kukwepa mafanikio yenye maslahi ya taifa.

Alisema wanasiasa hao, hususan wa upinzani, kwa muda mrefu walikuwa wakipiga kelele kutaka serikali iwe kali na kuchukua hatua pale mtumishi anapovurunda, lakini sasa wamebadilika.

Katibu huyo wa SUKI alisema wanasiasa kama hao hawapaswi kuachwa waendelee kuudanganya umma, bali waelezwe ukweli kuueleza ulimwengu dhamira nzuri ya serikali pale inaposimamia mambo mbalimbali yenye maslahi kwa nchi.

"Hivi sasa tupo kwenye mapambano dhidi ya dawa za kulevya. Hili ni janga linalomuathiri kila mmoja, lakini cha kushangaza hatua zimeanza kuchukuliwa, lakini wale wale waliokuwa wakihamasisha hatua zichukuliwe sasa wamebadilika. Hawa nendeni nao sawa pamoja na kuiunga mkono serikali katika hili,"alisema.

Kwa upande wake, Shaka alimhakikisha Kanali Lubinga kwamba, UVCCM ipo imara na kwamba itaendelea kusimamia mambo ya kitaifa kwa lengo la kuhakikisha CCM inafanikiwa kwenye mambo mbalimbali.

Shaka alisema licha ya wakati mwingine kuwepo kwa vuguvugu ndani ya umoja huo, lakini hakuna jambo lolote linalohatarisha umoja, mshikamano au utekelezaji wa jukumu la kusimamia mafanikio ya CCM.

"Tunakuhakikishia kiongozi wetu kuwa tupo imara kwa ajili ya maendeleo ya Chama. Tunaendelea kwenda na kasi ya serikali ya awamu ya tano, hususan kuwa na Tanzania ya viwanda. Katika kufanikisha hilo, huenda miezi michache ijayo baada ya mambo yetu kukaa sawa, tutatangaza kujiendesha wenyewe bila ya kutegemea ruzuku ya Chama.

No comments:

Post a Comment