Tuesday 21 February 2017

MBATIA AJIUZULU- SUNGURA


ALIYEKUWA Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NCCR-Mageuzi, Faustin Sungura, ametoa siku tatu kwa Mwenyekiti wa chama hicho James Mbatia, kujiuzulu wadhifa wake na kurejesha mali za chama anazodaiwa kupora.

Wengine waliotakiwa kujiuzulu ni Katibu Mkuu, Martin Ndanda na Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamaini, Mohamed Tibanyendela.

Sungura alidai vigogo hao wa NCCR -Mageuzi wasipojiuzulu atahakikisha anawapeleka mahakamani kwa kesi ya jinai kutokana na ubadhirifu wa mali za chama.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Sungura alitoa ushahidi wa mkataba wa ununuzi wa nyumba mbili eneo lisilopimwa Bunju “B”na kusema mali hiyo na shamba la ekari 56 Kilomo, Bagamoyo, Mbatia amelipora na kujimilikisha.

Alidai ununuzi wa shamba hilo ni michango ya wanachama ambayo Mbatia alipatiwa ili eneo la shamba hilo lijengwe chuo cha chama na katika maadhimisho ya miaka 10 ya chama, walitembelea na kukata vichaka na Mbatia kuunda kamati ya upembuzi wa ujenzi huo.

Sungura alisema baada ya Mbatia kuingia madarakani kumekuwa na wimbi kubwa la wanachama na viongozi kujiuzulu, kukata tamaa, kufitinishwa, kufukuzwa na chuki kwa wanaokijua chama au historia yake.

“Mbatia ni mkarimu kwa wageni wasiokijua chama ili awadanganye kuwa mali zote zisizohamishika ni mali zake ameziazimisha kwa muda kwenye chama,”alidai.

Aliongeza kuwa kumekuwapo na viongozi wanaoshirikiana na mwenyekiti huyo kufuja mali za chama, ikiwemo uuzaji wa nyumba Tarime kwa sh. milioni 45, fedha ambazo ziliwekwa katika akaunti ya chama na kuchotwa kwenda akaunti ya mjumbe wa baraza la wadhamini.

Mkurugenzi huyo alidai hivi sasa kumekuwapo na mkakati wa kuuza nyumba nyingine za chama  Sumbawanga, mkoani Rukwa na Mpanda, Katavi  na mauzo yatakabidhiwa kwa mjumbe kwa madai kuwa anakidai chama.

Sungura alidai lengo la Mbatia ni kuiua NCCR-Mageuzi na kuhamia CHADEMA mkakati ambao unaandaliwa chini ya mwamvuli wa UKAWA.

Kwa upande wake, Florian Kaijage ambaye ni Ofisa Tawala na Msemaji wa NCCR-Mageuzi,  alisema tuhuma hizo za Sungura dhidi ya viongozi wa juu ni za uongo, zikiwa na lengo la  kuchafuana, hivyo kumtaka Sungura kwenda mahakamani ili wakutane kila mmoja akiwa na ushahidi na siyo kuzungumza vitu visivyo na tija.

“Sungura tangu afukuzwe makao makuu, amekuwa na chokochoko zisizo na tija, lakini ni muhimu aelewe mali zisizoondosheka na zinazoondosheka ni mali zilizokuwa chini ya  baraza la wadhamini, hivyo aende  mahakamani tukutane huko mimi ndiyo natunza kumbukumbu asitake kuchafuana,”alisema Kaijage.

No comments:

Post a Comment