Tuesday, 21 February 2017

MAKAMBA: VIROBA NI HATARI KULIKO DAWA ZA KULEVYA


SERIKALI imeendelea kupigilia msumari kwa watumiaji wa pombe maarufu kwa jina la viroba baada ya kueleza kuwa ni hatari zaidi kuliko dawa za kulevya kwa sababu ya urahisi wa bei na upatikanaji.

Imesisitiza kuwa ifikapo Machi Mosi, mwaka huu, itapiga marufuku utengenezwaji na uuzwaji wa pombe za viroba na yeyote atakayepatikana akiuza atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), January Makamba,  wakati akizungumza jana na waandishi wa habari, Dar es Salaam.

Makamba alisema hatua ya kupiga marufuku pombe hizo siyo uamuzi wa ghafla, bali ilishaeleza dhamira ya kupiga marufuku pombe hizo bungeni pamoja na kutoa matangazo kupitia vyombo vya habari.

Alisema Ofisi ya makamu wa rais itatangaza utaratibu wa utekelezaji wa uamuzi wa serikali, ambapo waziri mwenye dhamana ya mazingira atatunga kanuni zitakazodhibiti uzalishaji wa vifungashio (viroba) vya pombe kali, kwa mujibu wa kifungu 230 (2) (f) cha sheria ya mazingira ya mwaka 2004.

Waziri huyo alisema kanuni hizo zitaweka sharti la kutaka pombe kali inayozalishwa viwandani, zifungashwe kwenye chupa zinazoweza kurejelezwa (recycled) kwa ujazo usiopungua miligramu 250.

“Kanuni hizo zitapiga marufuku uzalishaji, uuzaji, uingizaji nchini na matumizi pombe zilizofungwa kwenye viroba na mitambo ya malighafi ya vifungashio vya plastiki (viroba) vitakavyotumika kufungashia pombe kali.

“Atakayebainika kukiuka masharti ya kanuni hizo atawajibishwa kwa kulipa faini, kufungwa jela au vyote kwa pamoja, kama itakavyoainishwa kwenye kanuni,” alisema.

Makamba alibainisha kuwa, dhamira ya serikali si kupiga marufuku vinywaji vya pombe kali bali ni kutekeleza ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo inatoa haki ya kuishi katika mazingira yaliyo safi, salama na yenye afya.

Alieleza kuwa haki hiyo pia imetiliwa mkazo katika sheria ya mazingira ya mwaka 2004, hivyo dhamira ya serikali ni kudhibiti upatikanaji kwa urahisi wa pombe kali inayofungwa kwenye plastiki kwenye ujazo mdogo.

Hata hivyo alisema wazalishaji hao wanatakiwa kuomba kibali maalum cha muda mfupi, ambacho hakitatolewa hadi mwombaji awasilishe kabla ya Februari 28, mwaka huu.

Alisema mwombaji huyo anatakiwa awasilishe ushahidi wa barua kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwamba amelipa kodi katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Ushahidi mwingine ni barua, cheti kutoka Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), ambapo alisema mzalishaji atatakiwa kuwa na kibali cha usalama wa kinywaji kwa miaka yote ambayo atazalisha.

Pia alisema mzalishaji atatakiwa kuwa na cheti cha tathmini ya athari ya mazingira (EIA) au ukaguzi wa mazingira (EA) kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

Makamba aliwataka wakuu wa wilaya kupitia kamati za ulinzi na usalama za kamati za mazingira, kufanya operesheni ya kukamata na kuzuia viroba vinavyoingizwa nchini.

No comments:

Post a Comment