Tuesday, 21 February 2017

MBOWE ADAKWA NA POLISI




HATIMAYE Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam imemtia mbaroni Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe.
Mbowe alitiwa mbaroni jana na kufikishwa kituo kikuu cha polisi, saa 9.05alasiri.
Taarifa za uhakika zilieleza kuwa Mbowe alitiwa mbaroni baada ya kuwekewa mtego na polisi wakati akitokea mafichoni.
Ilidaiwa  Mbowe alikamatwa akitokea kwenye jengo moja kwenda nyingine, akitumia gari lenye rangi nyeusi, iliyokuwa na  vioo vyeusi na namba za usajili T 830 DEW, aina ya Toyota VX.
Alidaiwa  akiwa nje ya geti ya nyumba hiyo ambayo inadaiwa kuwa ni miongoni mwa majengo ya siri yanayomilikiwa na CHADEMA, Mbowe alitiwa nguvuni na polisi.
Baada ya hapo alifikishwa kwenye  katika kituo cha kituo kikuu cha polisi Dar es Salaam kwa ajili ya kuhojiwa.
Ilipofika saa 11: 38, Mbowe alitolewa na akaingia kwenye gari aina ya Toyota Land Cruiser, lenye namba za usajili T . 886 BWX akiwa na polisi. Haikujulikana mara moja alikuwa akipelekwa wapi.
Mbowe alikuwa ni miongoni mwa watu 65 waliotajwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kutakiwa kufika polisi kwa tuhuma za kujihusisha na dawa za kulevya.
Hata hivyo  mwenyekiti huyo wa CHADEMA alikaidi agizo hilo akidai kuwa mkuu wa mkoa hana mamlaka ya kumwamuru aende polisi.
Februari 18, mwaka huu, Kamishna wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro alimtaka Mbowe kujisalimisha na asipofanya hivyo polisi itatumia nguvu kumkamata.
Vita dhidi ya kupambana na dawa za kulevya imepamba moto nchi nzima ambapo imeelezwa kuwa tayari vigogo watatu wanaojihusisha na biashara hiyo wanashikiliwa.


No comments:

Post a Comment