Tuesday 21 February 2017

MAJALIWA: HATUNA PINGAMIZI HYDOM KUWA HOSPITALI YA KANDA


WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema serikali haina kipingamizi na wazo la kuifanya hospitali ya rufaa ya Haydom kuwa ya kanda, kwani hatua hiyo itaupunguzia mzigo.

Alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa kata ya Haydom, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa kata.

Majaliwa alisema serikali ni sikivu, hivyo kuifanya hospitali hiyo kuwa ya kanda ni kazi ndogo, kwani atamwagiza Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, awasimamie kufikia vigezo vya kuifanya hospitali hiyo kuwa ya kanda.

"Serikali haina kipingamizi na wazo lenu. Cha msingi ni vigezo muhimu vifuatwe. Kwa hiyo, nitamleta waziri wa afya awasaidie kuangalia vigezo.

“Nia yetu ni kupunguza gharama kwa mgonjwa anayelazimika kutoka Simiyu hadi Bugando (Mwanza) au kutoka Arusha hadi Muhimbili (Dar es Salaam).  Hapa ni katikati na nimearifiwa kuwa wagonjwa kutoka mikoa mitano ya Tabora, Simiyu, Arusha, Singida na Manyara wanafika hapa kupatiwa matibabu,” alisema.

Alisema serikali imepokea maombi kwa ajili ya watumishi wanaotakiwa kwenye hospitali hiyo na kwamba hivi karibuni itaajiri watumishi kati ya 5,000 hadi 6,000 wa sekta ya afya peke yake.

“Tumekwishaanza kuajiri, tumeanza na sekta ya elimu kwa kuajiri walimu 4,693 ambao wote ni wa fani ya sayansi. Na sekta inayofuata ni ya afya, kwa hiyo hao watumishi 90 wanaohitajika watapatikana kwenye kundi hilo hilo,” alisema.

Wakati huo huo, Balozi wa Norway nchini, Hannamarie Kaarstad, ambaye alikuwepo kwenye mkutano huo, alisema amefarijika na mchango unaotolewa na serikali kusaidia juhudi zinazofanywa na marafiki wa hospitali hiyo walioko Norway.

“Hospitali ya Haydom ni mahali thabiti ambapo mshikamano baina ya Tanzania na Norway unaweza kuonekana kwa dhahiri. Nawashukuru watumishi wa hospitali kwa moyo wao wa kujitoa kuwahudumia wananchi wa wilaya ya Mbulu na maeneo ya jirani,” alisema.

Hospitali hiyo ambayo inaendeshwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mbulu kwa ufadhili kutoka serikali za Tanzania na Norway, ilianzishwa mwaka 1955, ikiwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 50 ambapo kwa sasa ina uwezo wa kulaza wagonjwa 420 kwa wakati mmoja.

Pia inatoa huduma za upasuaji, magonjwa ya macho, tiba ya mifupa na mazoezi ya viungo.

Akisoma taarifa kwa waziri mkuu, Mkurugenzi Mtendaji wa Tiba wa hospitali hiyo, Dk. Emanuel Nuwass, alisema wameomba kibali cha ajira kwa watumishi 90 kupitia bajeti ya mwaka 2016/2017.

“Tumeomba pia hospitali ipandishwe hadhi na kuwa ya rufaa ya kanda (Kaskazini kati au Kanda maalumu) ili itoe huduma bora kwa mkoa wa Manyara na mikoa jirani kwani wahisani wa maendeleo wako tayari kuchangia ujenzi wa miundombinu,” alisema.

Pia aliomba waongezewe ruzuku ya dawa ikilinganishwa na ya sasa  ambayo ni asilimia 15 na pia waongezwe malipo ya posho kwa ajili ya madaktari na watumishi wengine wa hospitali hiyo.

No comments:

Post a Comment