Monday, 27 February 2017
MUSEVENI AWAFAGILIA WAWEKEZAJI WA NDANI
RAIS Yoweri Museveni wa Uganda, amehitimisha ziara yake ya siku mbili nchini kwa kutoa wosia kwa Watanzania kuunga mkono wawekezaji wa ndani na kutokuwa waoga kwenye kutekeleza kwa vitendo dhana ya uchumi wa viwanda.
Amewataka kuunga mkono kwa vitendo jitihada za serikali ya awamu ya tano, inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli, ya kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, badala ya kusubiri wageni kuja kutekeleza kwa niaba yao.
Rais Museveni alisema hayo jijini Dar es Salaam, jana,
wakati alipotembelea viwanda viwili vinavyomilikiwa na mfanyabishara Said Salim Bakhressa, eneo na Buguruni na Vingunguti wilayani Ilala.
Alisema amesukumwa kuhitimisha ujio wake Tanzania kwa kutembelea uwekezaji huo mkubwa wa mfanyabiashara huyo mzalendo, baada ya kuelezwa na mwenyeji wake juu ya uwezo wake wa kuthubutu, uliomfanya awekeze viwanda hapa nchini, Uganda pamoja na nchi nyingine za Afrika Mashariki.
"Bakhressa kule Uganda nimeambiwa ana kiwanda cha ngano na anataka kukitanua kwa kuanzisha kingine cha mahindi, hivyo nimeona kwa kuwa nimepata fursa ya kuja Tanzania, nije kuona kazi yake," alisema Rais Museveni.
Alitumia nafasi hiyo kuwataka Watanzania kuiga mfano wa mfanyabiashara huyo, huku akiwashauri kuanza na viwanda vidogo vidogo kabla ya kufikiria kuwekeza kwenye viwanda vikubwa.
"Kuliko kuwaachia wageni wanyonyaji waje nchini (ambao kule kwangu wapo wengi) na kutufanya kama soko kwa bidhaa zao, watu kama hawa ni bahati kuwa nao, wanasaidia kuhifadhi fedha za kigeni zisipotee," alisema.
Akionekana mwenye furaha wakati wote tangu alipowasili nchini mwishoni mwa wiki iliyopita, Rais Museveni alifika kwenye kiwanda cha ngano cha Buguruni, saa 4.30 asubuhi, kabla ya kwenda kiwanda cha vinywaji na matunda cha Vingunguti.
Akiwa Vingunguti, alitembelea kiwanda hicho kwenye baadhi ya mashine kisha alikabidhiwa zawadi mbalimbali, zikiwemo juisi ya sharubati kutoka kampuni tanzu ya kampuni za Azam, kwa ajili ya kurudi nazo Uganda.
Naye Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, ambaye alikuwa miongoni mwa viongoni kwenye ziara hiyo, sambamba na Waziri wa Mambo ya Nje, Dk. Augustine Mahiga, alisema ushirikiano wa kibiashara baina na Tanzania na Uganda bado hauridhishi.
Alisema kwa takwimu za hivi karibuni, kuna jumla ya Dola milioni 190, zinazoingia serikalini kutokana na biashara halali baina na nchi hizo na kwamba, baada ya mazungumzo ya wakuu wa nchi, wamekiri hazitoshi ikizingatiwa Tanzania ni ndugu wa Uganda kwa muda mrefu.
Waziri huyo alimpongeza Bakhressa kwa kuzalisha ajira na kushiriki kimamilifu kwenye uanzishaji wa viwanda vikubwa Tanzania na Uganda na kumtaka aendeleze jitihada hizo.
"Ni kweli biashara ya Tanzania na Uganda bado iko chini, tunaendelea kushauri wananchi wetu washirikiane kwenye biashara, kwa sababu kwa umoja wetu, tunaanzisha kituo pale Mtukula, Kagera na bandari bubu mkoani Mwanza ili bidhaa zetu na Uganda, ziende vizuri.
"Kama mlivyosikia kwa mwaka tunafanya biashara ya Dola milioni 190, lakini kuna zile biashara za mipakani na bandarini kwa njia za vificho vificho, wazirasimishe ili tuzitambue, tujue kwa kiasi gani hasa biashara za nchi hizi mbili zinaingiza fedha," alisema.
Waziri huyo aliongeza kuwa, kiwanda cha Azam kilichoko Uganda, kinaunga mkono juhudi za makubaliano ya mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika uliofanyika Januari, mwaka huu, nchini Ethiopia wa kushirikiana kwenye biashara huria kabla ya Desemba, mwaka huu.
"Ni lazima tuwe na viwanda vyetu, kwa mfano takwimu zinatueleza kuwa, Tanzania tunatumia Dola milioni 60, kila mwaka, kuagiza mahindi kutoka nchi za wenzetu barani Afrika na Dola bilioni 110, kutoka nje ya Afrika.
"Kwahiyo tunatakiwa kuchangamkia fursa hiyo. Waganda huzalisha tani milioni nne za mahindi, lakini wanatumia tani milioni moja tu, sisi tuwe wateja wao, badala ya kununua mbali zaidi kujiongezea gharama," alisema.
Aidha, alisema Watanzania hawapaswi kuwa waoga kwenye suala zima la uchumi wa viwanda, kwa sababu sio lazima waanzishe viwanda vikubwa kama vya Bakhressa, bali hata kulima matunda bora kwa ajili ya malighafi ya viwanda ni kushiriki kwenye kuufikia uchumi huo.
"Tena kwenye matunda ndio kuna fursa lukuki. Pamoja na hivi vya Bakhressa, kuna viwanda vingine vitatu vya matunda vitaanzishwa kule Mbeya, Mwanza na Mboga mkoani Pwani, hivyo soko lipo," alisema Waziri Mwijage.
Kwa upande wake, Hussein Sufian, ambaye ni Mkurugenzi wa Uhusiano wa Kampuni za Bakhressa, alisema kiwanda cha Azam cha nchini Uganda, kinazalisha tani 1,100 za ngano kwa siku na kilianzishwa 1998.
Alisema kiwanda hicho kimewekezwa kwa mtaji wa Dola milioni 60, ambapo wana mpango wa kukitanua ili kizalishe tani 2,000, za ngano kwa kwa siku na kingine kipya kitazalisha tani 500, za mahindi yaliyosagwa kwa siku.
Rais Museveni aliondoka nchini jana kurudi Uganda, akisindikizwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Dk. Augustine Mahiga, Waziri Mwijage na Katibu Mkuu wizara ya viwanda, Dk. Adlehem Meru.
Aliwasili nchini mwishoni mwa wiki iliyopita na kulakiwa na mwenyeji wake, Rais John Magufuli, kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, kabla ya kufanyika dhifa ya kitaifa Ikulu, jijini Dar es Salaam.
Akiwa nchini, alifanya mazungumzo na Rais Magufuli na kufikia makubaliano mazuri ya kudumisha ushirikiano, ikiwemo kuanza mara moja ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima, Uganda mpaka Tanga.
Pia, walizungumzia kuhusu umuhimu wa kubatilisha maamuzi ya Uganda ya kutia saini mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi wa Jumuia ya Ulaya (EPA), dhidi ya EAC, kutokana na kutokuwa na maslahi kwa jumuia hiyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment