Tuesday, 28 February 2017

DK. SHEIN AWASHUKIA WAPINZANI, ASEMA HANA MPANGO WA KULIVUNJA BARAZA LA WAWAKILISHI


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema hana mpango wa kulivunja Baraza la Wawakilishi.

Dk. Shein amesema hakuna Baraza la Wawakilishi linalovunjwa ndani ya mwaka mmoja na kiutaratibu, baraza hilo huvunjwa baada ya miaka mitano kwa sheria na kanuni zake.

Rais huyo wa Zanzibar amewataka wananchi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuepuka kauli za upotoshwaji zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

Alisema hayo juzi, kwenye ukumbi wa CCM, mkoa wa Mjini, baada ya kukabidhi vifaa vya michezo kwa vijana kwa ajili ya maandalizi ya ligi ya soka ya Unguja, inayotarajiwa kuzishirikisha timu 18.

Dk. Shein alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, anayoiongoza, itaendelea kuwa madarakani na kuongeza kuwa, mazungumzo aliyoyafanya juzi, kati yake na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, ni ya kawaida baada ya kumwita kwa lengo la kubadilishana naye mawazo na kueleza changamoto zilizopo katika majimbo yao.

Alisema akiwa Rais wa Zanzibar, sio jambo jipya au la ajabu kwake kuzungumza na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na kwamba, ameshawahi kufanya hivyo kutokana na taratibu na kanuni zilizopo.

Aliwasisitizia wana-CCM na wananchi kuwa, hakuna baraza linalovunjwa mapema kiasi hicho, hivyo kauli zinazozungumzwa na kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii ni za upotoshaji na hazina ukweli.

Dk. Shein alisema mihimili mitatu iliyopo, ikiwemo Mahakama, Serikali na Baraza la Wawakilishi, hakuna hata mmoja unaomshurutisha mwenziwe, bali hufanyakazi kwa ushirikiano ili kufikia malengo yaliyokusudiwa katika nchi.

Kwa upande wake, Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idd, alisema
uzushi unaosambazwa katika mitandao hauna maana.

Alisema amepokea simu nyingi kutoka kwa wananchi kuhusu taarifa hizo za kwenye mitandao, ambazo alisisitiza kuwa hazina ukweli wowote.

Balozi Seif alisema kauli za aina hiyo hazikuanza leo, bali ni za kawaida kutolewa na wapinzani na kuwataka wana-CCM na wananchi kuzipuuza.

No comments:

Post a Comment