Tuesday 28 February 2017

MWANASHERIA MKUU AONDOA RUFANI MBILI DHIDI YA LEMA


OFISI ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeondoa rufani mbili namba tisa na 10, zilizokatwa dhidi ya Mbunge Godbless Lema (Arusha Mjini-CHADEMA) katika Mahakama ya Rufani, inayoendelea na vikao vyake jijini hapa.

Awali, kabla ya rufan hiyo kusikilizwa, Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi akisaidiwa na Wakili wa Serikali, Paul Kadushi kutoka Jijini Dar es Salaam, waliieleza Mahakama hiyo kuwa, wana maombi ya hoja za awali.

Baada ya maelezo hayo, jopo hilo la majaji watatu wanaosikiliza rufani hiyo chini ya Mwenyekiti wao, Jaji Bernard Luanda akisaidiwa na Musa Kipenga  na Stella, alikubali maombi hayo ya kutaka yawasilishwe kabla ya rufani hiyo kusikilizwa.

Nchimbi aliileza mahakama hiyo kuwa, upande wa Jamhuri, Februari 24, mwaka huu, ulikaa na kukusudia kutoendelea na rufaa namba tisa juu ya Lema kunyimwa dhamana.

Baada ya maelezo hayo,  mahakama ilikubalina na ombi hilo na kuiondoa rufani hiyo mahakamani.

Kuhusu rufani namba 10,  Kadushi aliieleza Mahakama kuwa, wana ombi pia kabla ya rufani hiyo kusikilizwa, ambapo alidai kuwa upande wa Jamhuri hauna nia ya kuendelea na rufaa hiyo kutokana na kuwa haikuwa na kibali cha Mahakama ya Rufani.

Baada ya maelezo hayo, jopo hilo la majaji lilishauriana kwa muda kisha Jaji Stela kusoma uamuzi wa mahakama, ambapo alisema kuwa ombi la upande wa Jamhuri limekubaliwa na rufani hiyo imeondolewa mahakamani.

Kwa upande wa wakili wa upande wa mjibu maombi, Peter Kitabala akisaidiwa na Adam Jabir, aliiomba mahakama kutoa hoja juu ya upande wa Jamhuri kuondoa rufaa zote mahakamani hapo.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa jopo la majaji hao, Jaji Luanda alikataa ombi hilo la Kibatala na kumweleza: "DPP wamedai mahakamani hapa rufaa yao haipo sawa. Sasa mnataka kutoa hoja za nini wakati hakuna rufaa? Mlango ulishafungwa, unataka kupitia dirishani?"

Baada ya maelezo hayo, Jaji Luanda aliwaonya mawakili wa serikali kuacha kuitia najisi tasnia ya sheria, hali inayosababisha watu wote katika tasnia tuonekane watu wa hovyo na kusema jambo hilo sio sahihi.

Lema, ambaye ameshakaa mahabusu kwa zaidi miezi mitatu na wiki mbili sasa tangu alipokamatwa na polisi katika viwanja vya bunge mjini  Dodoma,   Novemba 2, mwaka jana na kufikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi, Novemba 8, mwaka jana, anatuhumiwa kwa kesi mbili, namba 440 na 441 za  uchochezi dhidi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli.

Katika kesi hizo,  Wakili Kadushi, aliwasilisha notisi ya kukata rufani Mahakama Kuu, kupinga Lema kupewa dhamana, ombi ambalo alilitamka muda mfupi kabla ya Hakimu Desdery Kamugisha kutoa masharti ya dhamana.

Kutokana na pingamizi hilo, Kamugisha aliahirisha kesi hiyo kwa dakika 10, kisha kurejea na kutoa maamuzi kwamba, hawezi kumpa Lema dhamana kufuatia notisi iliyowasilishwa na Mwanasheria wa Serikali, ambapo ilimlazimu mbunge huyo  kurejeshwa  mahabusu katika Gereza la Kisongo.

Hata hivyo, upande wa mawakili wa utetezi wakiongozwa na John Mallya akisaidiwa na Sheck Mfinanga, walikata rufani dhidi ya dhamana ya mteja, ambayo ilikuwa isikilizwe Januari 4, mwaka huu.

Jaji Salma Magimbi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, katika rufani hiyo namba 135 ya mwaka jana, alisema hawezi kutoa uamuzi wa kumpa Lema dhamana au la, kwa kuwa  upande wa Jamhuri  ulikuwa umeshawasilisha notisi ya kupinga rufani yao isisikilizwe katika Mahakama ya Rufani Tanzania.

No comments:

Post a Comment