Tuesday 28 February 2017

POMBE ZA VIROBA MWISHO LEO, WAFANYABIASHARA WAHAHA


WAFANYABIASHARA wa vileo katika jiji la Dar es Salaam, wameiomba serikali ieleze hatima yao kibiashara na utaratibu utakaofuata, hususan kwenye utengenezaji wa pombe, inayojulikana kwa jina maarufu la viroba.

Wamesema wengi wao wana hifadhi kubwa ya pombe hiyo kwa sababu ilikuwa inapendwa na watumiaji wengi.

Kauli hizo zimekuja siku moja kabla ya kuanza kwa utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, la kupiga marufuku biashara ya pombe hiyo maarufu, ambayo imetajwa kuwa chanzo cha matatizo mengi kwenye jamii.

Baadhi ya matatizo hayo ni wanafunzi kutokuzingatia masomo na kugeukia ulevi wa bidhaa hiyo, inayopatikana kwa gharama nafuu na kwenye vifungashio rahisi kubebeka, ikiwemo kufichika pale mtumiaji anapohitaji kufanya hivyo.

Pia,  kifamilia imetajwa kuwa kichocheo kikubwa cha ugomvi baina ya wanandoa, kutokana na utamaduni uliojengeka kuwa, yeyote anaweza kutumia kama moja ya njia za kusahau matatizo, lakini matokeo yake yakawa sababu ya kuyatengeneza makubwa zaidi.

Kimazingira, vifungashio vya pombe hiyo vimetajwa kutokuwa rafiki na mazingira, hususan wakati huu, ambao serikali iko kwenye mapambano ya kuyaokoa mazingira kwa kupiga marufuku vifungashio jamii ya mifuko ya plastiki, hasa ile isiyooza kirahisi.

Akizungumza Februari 16, mwaka huu, mkoani Manyara, alipokuwa kwenye ziara yake ya siku mbili ya kikazi, Waziri Mkuu Majaliwa, alisema serikali itapiga marufuku matumizi ya pakiti za plastiki kufungashiwa pombe hiyo ya viroba.

“Tumekaa na wenye viwanda na kukubaliana kuwa, wanaotengeneza pombe waziweke katika ukubwa unaokubalika na sio kama ilivyo sasa, tunaua nguvu kazi ya taifa.

“Sasa hivi viroba vimeenea kila kona, hata watoto wa shule za msingi wanatumia kwa sababu ni rahisi kuweka mfukoni na kutembea navyo,” alisema kwenye mkutano huo uliofanyika Mererani, wilayani Simanjiro.

Kauli hizo za Waziri Mkuu, zilifuatiwa na tamko kuwa kuanzia Machi 1, mwaka huu (kesho), atakayekamatwa ameshika pombe ya viroba, ‘ama zake ama za serikali’.

Alisema agizo hilo linakwenda sambamba na vita dhidi ya dawa za kulevya, kwa sababu mji wa Mererani, unaongoza kwa matumizi ya dawa hizo haramu.

Wakizungumza jana na gazeti la Uhuru, jijini Dar es Salaam, wafanyabiashara hao walisema wanafahamu kuwa agizo la Waziri Mkuu ni agizo, lakini wanaomba kupewa mwongozo.

“Tunaomba tuambiwe ni wapi tunapaswa kwenda kuteketeza bidhaa hizi badaa ya tarehe moja, hatuelewi, binafsi sijachukua hatua yoyote tangu Waziri Mkuu mlipoagiza, nilidhani utani,” alisema Quiton De Boers, mkazi wa Msasani.

Kwa upande wake, Penina Mzee, alisema yeye kama mmiliki wa sehemu ya kuuzia vileo, vikiwemo viroba, hajui atafidiwa wapi gharama ya hasara itakayopatikana baada ya uteketezaji.

“Hali tete mwandishi, hapa sina mbele wala nyuma, akili yote imevurugwa kwa sababu siku hizi hata hao waliokuwa wanakunywa sana, wamepunguza,” alilalama.

Baada ya mazungumzo hayo, Uhuru liliendelea kutembea kwenye maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam na viunga vyake, kujionea hatua za awali za utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, lakini maeneo mengi yalionekana kawaida.

No comments:

Post a Comment