Tuesday, 28 February 2017
SERIKALI YASEMA WALIOTIMULIWA MSUMBIJI WALIKIUKA SHERIA
SERIKALI imesisitiza kuwa Watanzania waliofukuzwa nchini Msumbiji, walikiuka taratibu na sheria za kuishi na kufanya kazi nchini humo.
Kauli hiyo imetolewa huku kukiwa na malalamiko kwa baadhi ya Watanzania waliofukuzwa nchini humo na baadhi ya wananchi, ambao wanadai kuwa walitimuliwa kwa njia za uonevu.
Akizungumza ofisini kwake, mwishoni mwa wiki, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Halima Dendego, alisema hakukuwa na uonevu wala chuki ya aina yeyote kutokana na uamuzi huo.
Alisema kilichofanywa na serikali ya Msumbiji kilikuwa sahihi kwa sababu Watanzania hao walikuwa wakiishi kimakosa na kwamba walikiuka taratibu na sheria.
“Binafsi ile mara ya kwanza niliposikia wananchi hao wakilalamika, kwamba walifukuzwa kwa uonevu, roho iliniuma sana. Iliniuma kutokana na uhusiano uliopo kati yetu na wenzetu wa Msumbiji, ambapo tumefika mahali tumekuwa tukiishi kama ndugu wa kuzaliwa tumbo moja, sasa iweje leo wafukuzwe,” alisema Halima.
Alisema muda mfupi baada ya kupokea taarifa hizo, alikutana na viongozi wa Idara ya Uhamiaji na vikosi vya ulinzi na usalama na kuanza kulifanyia kazi sakata hilo ili kupata ukweli.
Kwa mujibu wa mkuu huyo wa mkoa, baada ya kufuatilia kwa undani suala hilo, walibaini kwamba Watanzania hao walikuwa wakiishi nchini humo kinyume cha sheria.
“Hawakuwa na uhalali wa kuishi katika nchi ile. Hawakuwa na vibali vya kuishi wala kufanyakazi," alisema na kuongeza kuwa, wengi walikwenda kufanya biashara kienyeji na wengine waliweka makazi kwenye machimbo ya madini.
Halima alisema kadri mambo yalivyokuwa yakiwanyokea, ndivyo Watanzania hao waliokuwa machimboni walivyozidi kujazana huko kutafuta maisha.
Alisema haikua kosa kuishi na kufanyakazi nchini humo, lakini walitakiwa kufuata taratibu na sheria za nchi hiyo ili kuondoa usumbufu uliojitokeza.
Kwa mujibu wa Halima, hadi kufikia mwishoni mwa wiki iliyopita, ofisi yake ilipokea wananchi 5,222, ambapo ilibainika kuwa, 20 hawakuwa Watanzania.
“Tulifanya kila jitihada tukawapokea na kuwasafirisha na mpaka dakika hii wamebaki wananchi kama 1,000, ambao muda wowote tutawasafirisha kwenda makwao. Na huko Msumbiji mpaka sasa hatujapata taarifa ya kuwepo kwa watu kama hao na kama watakuwepo, basi watakuwa wachache," alisema.
Alitoa wito kwa Watanzania wanaokwenda kuishi na kufanya kazi nchini humo au kwengineko, kufuata taratibu na sheria za nchi husika.
Alisema kufanya hivyo kutawaondolea bughudha na majanga mengine yanayoweza kujitokeza kwa kuishi nchi za watu kinyume cha sheria.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment