Tuesday 28 February 2017

KICHANGA CHAIBWA HOSPITALINI KAHAMA


KICHANGA cha kike chenye umri wa siku sita, kinadaiwa kuibwa na watu wasiofahamika ndani ya wodi ya wazazi katika Hospitali ya Mji wa Kahama na kutokomea nacho kusikojulikana.

Tukio hilo lilitokea wakati mama mzazi wa mtoto huyo, aliyejulikana kwa jina la Zuhura Khamisi, kwenda bafuni kuoga huku akimwacha mwanaye akiwa amelala kitandani.

Akizungumza na Uhuru, jana, Muuguzi wa zamu hospitalini hapo, Konchesta Felix, alisema tukio hilo lilitokea baada ya yeye kwenda kuhudumia wagonjwa wodi nyingine huku akimwacha mama huyo akiwa na mtoto wake.

“Hili tukio ni la kushangaza sana. Mimi nilikwenda wodi nyingine kuhudumia wagonjwa, niliporudi nikapata taarifa ya mtoto huyo kuibwa. Mama huyo alikuwa na bibi wa mtoto, ambaye ndiye alimpeleka bafuni kumwogesha, lakini wanadai waliporudi kutoka bafuni, hawakumkuta mtoto
kitandani,"alisema.

Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Emmanuel Kadelya, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa, lilitokea juzi, saa moja asubuhi, wakati mama mzazi wa mtoto huyo alipopelekwa bafuni kuoga.

Dk. Kadelya aliwatupia lawama walinzi wa hospitali kwa kuzembea na kutokuwa na mpangilio mzuri wa ulinzi kwa wanaoingia na kutoka kuwaona wagonjwa.

“Tukio hili limesababishwa na mpangilio mbovu wa walinzi kutokana na watu wanaoingia na kutoka wodini kuangalia wagonjwa. Walinzi wanapaswa kujipanga kudhibiti uingiaji holela wodini,”alisema Dk. Kadelya na kuongeza;

“Ni kweli mama kajifungua kwa upasuaji, lakini jukumu la kuangalia mtoto ni lake. Iwapo atatoka leba akiwa hajitambui, mtoto atalindwa na wauguzi wetu hadi hapo akili itakapomjia na ndiyo maana alipopata akili, alikabidhiwa mtoto wake.”

Kwa upande wake, Suzana Bundala, mama mzazi wa Zuhura Khamisi, alisema amesikitishwa na tukio hilo la mwanawe kufungua mtoto huyo katika mazingira magumu ya upasuaji kisha mtoto anaibwa.

Mashuhuda wa tukio hilo walishauri ulinzi uimarishwe wodini ili kuhakikisha kila anayejifugua anaondoka salama na mtoto wake.

No comments:

Post a Comment