Wednesday 1 March 2017

MAJALIWA ABAINI MADUDU MINADA YA MADINI, AWAONYA VIONGOZI WA MASHIRIKA YANAYOJIENDESHA KWA HASARA


WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema anafuatilia kwa makini minada ya madini inayofanyika nchini kwa sababu anazo taarifa za kukiukwa utaratibu kwenye minada hiyo.

Amesema ukiukwaji huo unachangia kutobadilika kwa mapato ya mauzo yatokanayo na mnada, hata kama kuna vito viliyokatwa au havijakatwa.

Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo juzi, wakati akihitimisha kikao alichokiitisha kwenye makazi yake, Oysterbay, Dar es Salaam, kilichojumuisha Waziri wa Fedha na Mipango, Waziri wa Nishati na Madini, Mkuu wa Mkoa wa Manyara na watendaji wake, Mbunge wa Simanjiro, wamiliki wa mgodi wa Tanzanite One, watumishi waliofukuzwa kazi na wachimbaji wadogo.

Alisema licha ya kuwa Kitengo cha Uthaminishaji wa Madini ya Almasi na Vito cha Wizara ya Nishati na Madini (TANSORT), kinasifiwa kwa kuongeza mapato ya madini, bado kuna kazi ya ziada inabidi ifanyike kwenye minada hiyo ili serikali iweze kunufainika na madini hayo.

“Uzoefu wa kwenye minada ya korosho unaonyesha kuwa wanaushirika ndiyo wanaiba fedha za wakulima. Nimekuwa ninafuatilia kwa muda sasa uendeshaji wa hii minada na sijaridhishwa na uendeshaji wake. Hakuna tofauti ya bei madini ya Tanzanite yanapokuwa yamekatwa au la,”alisema.

Kwa mujibu wa wataalamu wa madini na vito, inapotokea kuna madini yamekatwa, bei inapaswa kuwa juu ikilinganishwa na madini ghafi yanapouzwa moja kwa moja.

Alimwagiza Kaimu Kamishna wa Madini, Benjamini Mchwampaka, ambaye alihudhuria kikao hicho kwa niaba ya Kamishna wa Madini, aende Mirerani na kufuatilia utendaji kazi wa mgodi wa Tanzanite One na suala la teknolojia inayotumika kiwandani hapo.

Waziri Mkuu aliitisha kikao hicho kutokana na ahadi aliyoitoa kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Mirerani, wilayani Simanjiro, mkoa wa Manyara, Februari 16, mwaka huu.

Katika ahadi hiyo, Waziri Mkuu Majaliwa alisema atakapomaliza ziara ya mkoa huo, ataitisha kikao na wawekezaji wa Tanzanite One, baada ya kupokea malalamiko kwamba hali ya watumishi ilikuwa nafuu wakati kampuni hiyo ilipokuwa inamilikiwa na wazungu kuliko ilivyo hivi sasa.

Ili kuhakikisha ukusanyaji wa mapato katika sekta ya madini unaongezeka, Waziri Mkuu alimwagiza Kamishna wa Mamlaka ya Mapato (TRA), aimarishe ukaguzi kwenye viwanja wa ndege vya Arusha na KIA cha Kilimanjaro.

“Kamishna wa TRA na watu wako inabidi mjipange kwa sababu kuna njia nyingi za ukwepaji kodi zinafanyika kwenye sekta ya madini, wakiwemo hata hawa wachimbaji wadogo. Simamieni utaratibu wa kufuatilia kodi, nendeni kule walipo, msisubiri waje wakuleteeni malipo ofisini. Wasipokuja je? Au wakija na wasikukuteni ofisini je?” Alihoji.

Akizungumzia kuhusu uelewa wa sheria miongoni mwa wachimbaji wadogo, Waziri Mkuu alisema Wizara ya Nishati na Madini kupitia kwa Kamishna wa Madini, wanapaswa kutoa elimu na uelewa wa kisheria kwa wachimbaji hao ili kupunguza migogoro, ambayo imekuwa ikijitokeza kwenye maeneo mengi nchini.

“STAMICO na Kamishna wa Madini, fanyeni kazi pamoja, waelewesheni wachimbaji wadogo kuwa uwepo wa vitalu maana yake kuna mipaka ambayo pia inajumisha utoaji wa leseni kwa wenye vitalu hivyo. Kwa hiyo, waelimisheni kuwa mtu hapaswi kwenda upande wa pili wa mwenye leseni, akifanya hivyo atakuwa anavunja sheria.

“Nyinyi ni wadau wakubwa wa sekta hii kwa hiyo mnapaswa kushiriki katika kutoa elimu. Mnayo maeneo mengi ya uchimbaji, lakini yana migogoro, mfano ni kule Ngaka na Kiwira. Maeneo yote haya yanahitaji usimamizi mzuri. Mnayo bodi, mwenyekiti yupo kwa hiyo mnatosha kuifanya kazi hii,” alisisitiza.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka wamiliki wa mgodi wa Tanzanite One kuboresha uhusiano na vijiji vilivyo jirani na mgodi huo.

“Kuweni karibu na wananchi ili wajue umuhimu na uwepo wenu na waweze kusaidia kulinda mali zenu. Shirikianeni na Halmashauri na Baraza la Madiwani, tangazeni kazi zenu za CSR ili wananchi wajue mmechangia nini katika kusaidia maendeleo yao,”alisema.

Kuhusu suala la watumishi waliofukuzwa kazi kwenye mgodi huo, Waziri Mkuu alimwagiza Katibu Mkuu Ofifisi ya Waziri Mkuu (OWM-Kazi, Ajira na Vijana), Erick Shitindi, kusimamia suala lao na kuwapatia majibu kuhusu hatma yao.

Watumishi hao walikuwa wanawakilisha wenzao 201, ambao walifukuzwa kazi Februari 8, 2016, kwa sababu ya kufuatilia maslahi yao, yakiwemo malipo ya saa za kazi za ziada (overtime), mishahara ya miezi miwili, malipo ya NSSF, vitendea kazi na usalama wa kazi migodini.

Wakati huo huo, Mussa Yusuph ameripoti kuwa, Waziri Mkuu Majaliwa, amesema ni kosa kubwa kwa watendaji wakuu wa mashirika ya umma kuendesha mashirika hayo kiholela na kuyafanya mtambo wa kutengeneza hasara.

Aidha, amesema ukosefu wa menejimenti nzuri na wataalamu wenye tija ndio chanzo kikuu cha mashirika hayo kuendeshwa kwa kutozalisha faida, badala yake kutegemea ruzuku kutoka serikalini.

Majaliwa aliwataka watendaji hao kuangalia utaratibu unaotumika kuwateua wajumbe wa bodi za mashirika ya umma, kama unapaswa kuendelea au kubadilishwa kwa sababu ya kuwepo wa malalamiko kutoka kwa wananchi.

Waziri Mkuu alisema kuna umuhimu wa kupitia muundo, rasilimali na teknolojia kama Ofisi ya Msajili wa Hazina ina uwezo wa kutosha katika kusimamia mashirika ya umma kwa ufanisi.

Alisema hayo jana, Ikulu, Dar es Salaam, katika mkutano wa kujadili nafasi ya mashirika ya umma katika kutekeleza mpango wa pili wa taifa wa maendeleo wa miaka mitano (2016/17-2020/21).

Majaliwa alisema mashirika hayo yanapaswa kujiendesha kwa kutengeneza faida na kwamba, mafanikio makubwa yaliyopatikana kwenye  baadhi ya  mashirika ya umma ya nchi za kigeni, hususan Shirika la Ndege la Ethiopia yalitokana na ubunifu na matumizi mazuri ya rasilimali chache walizozipata.

“Kwa bahati mbaya hapa kwetu, baadhi ya watendaji wa mashirika hayo wanachokifanya ni kuhakikisha mashirika hayafi ila yanakuwepo kama kuweka boya kwenye chombo baharini, kuzuia kisitembee au kuzama.

“Ni sawa na kuku aliyeyatamia mayai bila kuyatotoa na kila mwaka yako vile vile. Mashirika ya umma ya wenzetu yameweza kufungua kampuni tanzu zilizovuka mipaka ya nchi zao, lakini tunaweza kuvuka kwa namna tulivyo sasa?” Alihoji Waziri Mkuu.

No comments:

Post a Comment