Wednesday 1 March 2017

UKIKUTWA NA KIROBA JELA MIAKA MITATU AU FAINI 50,000


SERIKALI imesema utekelezaji wa maamuzi kuhusu usitishaji, uingizaji, uzalishaji na matumizi ya vifungashio vya pklastiki vya kufungia pombe kali, utaanza rasmi leo, katika mikoa yote ya Tanzania Bara.

Pia, imesema kuanzia leo, mtu atakayekamatwa anamiliki pombe kali iliyowekwa kwenye vifunganisho vya plastiki (viroba), adhabu yake ni faini ya sh. 50,000 au kifungo cha miaka mitatu jela ama faini na kifungo.

Mbali na hilo, imesema kuanzia kesho, kamati za ulinzi na usalama za mikoa, wilaya, tarafa, kata, vijiji na mitaa pamoja na kamati za mazingira, zitaendesha operesheni kali ya kukagua utekelezaji wa agizo hilo la serikali la usitishaji, utengenezaji, uuzaji na matumizi ya pombe zinazofungwa kwenye vifunganisho vya plastiki.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Januari Makamba, alisema hayo jana, ofisini kwake Dar es Salaam, alipokuwa akitoa taarifa kuhusu mpango wa upigaji marufuku uzalishaji, uingizaji, usambazaji na matumizi ya vifungashio vya plastiki (viroba) vya pombe kali nchini.

Alisema kufuatia zuio hilo, watakaoingiza pombe kali kutoka nje ya nchi, adhabu yake ni faini isiyozidi sh. milioni tano au kifungo cha miaka miwili jela, watakaozalisha adhabu yake ni faini ya sh. milioni mbili au kifungo cha miaka miwili na watakaouza, kusambaza faini yake ni sh.  100,000 au kifungo.

Januari alisema Februari 20, mwaka huu, Ofisi ya Makamu wa Rais ilitoa tamko la serikali la utaratibu utakaotumika kutekeleza agizo la kusitisha utengenezaji, uuzaji na matumizi ya pombe kali zinazofungashwa kwenye vifungashio vya plastiki, kuanzia leo.

“Utekelezaji wa katazo hili utazingatia Ibara ya 8(1) (b) na 14, Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 na kanuni zake zilizotungwa kupitia kifungu 230 (2) (f) cha sheria hiyo na Sheria ya Leseni za Vileo Namba 28 ya mwaka 1968 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2012,” alisema.

Januari alisema Februari 24, mwaka huu, kiliitishwa kikao cha mawaziri na viongozi wa taasisi za serikali kujadili mpango wa utekelezaji wa zuio hilo na kwamba katika kikao hicho, wizara na taasisi za serikali zilipewa majukumu mbalimbali.

Alisema katika majukumu hayo, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),  kwa kuzingatia umuhimu wa ujazo katika utozaji kodi, imeanzisha mfumo wa stempu za kielektroniki ili kudhibiti ujazo wakati wa uzalishaji kwa ajili ya kupata mapato stahiki.

Aidha, TRA itahakikisha kwamba wazalishaji na waingizaji nchini wa malighafi ya pombe kali (ethanol), wamesajiliwa na mfumo wa ufuatiliaji wa usambazaji malighafi hiyo unawekwa.

Januari alisema wazalishaji na waingizaji wa malighafi hiyo watawauzia wale, ambao wamepewa kibali na pia watatakiwa kutoa taarifa kila baada ya miezi mitatu ya kiasi cha ujazo kilichouzwa na wateja waliouziwa ambao wamesajiliwa.

Alisema uuzaji wa malighafi kwa watengezaji wa pombe kali, ambao hawajasajiliwa, itakuwa ni kosa la jinai kulingana na sheria.

Januari alisema Mkemia Mkuu wa Serikali, ambaye ndiye msajili wa kemikali za viwandani na majumbani, atasajili kampuni na taasisi zinazoingiza kemikali za viwandani na majumbani nchini, ikiwa ni pamoja na ethanol.

“Kulingana na sheria ya leseni ya vileo na 28 ya mwaka 1968 na marekebisho yake ya mwaka 2012, Ofisi ya Rais, TAMISEMI katika operesheni hii itaratibu zoezi hili katika mikoa, wilaya, tarafa, kata, vijiji na mitaa yote Tanzania Bara kwa kuhakikisha kuwa wanaofanya biashara ya pombe ya kawaida na pombe kali (spirit) na watumiaji kinyume na masharti ya leseni za vileo wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria,” alisema.

Alisema Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, kupitia Shirika la Viwango Tanzania (TBS), katika operesheni hiyo watakagua viwanda vyote vinavyojihusisha na uzalishaji wa vileo na vifungashio vya aina mbalimbali vya kufungia pombe kali kama vimekidhi viwango vya kitaifa  vilivyowekwa.

Januari alisema ukaguzi katika viwanda vya plastiki utachunguza kama kuna mitambo ya kuzalisha vifungashio vya plastiki kwa ajili ya pombe kali.

Alisema mitambo ya kuzalisha vifungashio vya plastiki itakayokutwa inaendelea kuzalisha pombe kali na kufungashia vifungashio vya plastiki, itakamatwa na kutaifishwa na wahusika watashitakiwa.

Waziri huyo alisema Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kupitia Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na mabwana afya, katika operesheni hiyo watatoa elimu kwa umma na kukagua maeneo yote yanayotumika kuhifadhia, kuuza na kusambaza vileo vya aina zote.

Alibainisha kwamba Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, kupitia Idara ya Habari Maelezo, itasaidia kutoa elimu kwa umma kuhusu suala hilo.

Alisema Wizara ya Mambo ya Ndani, kupitia Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, itashiriki katika operesheni, ikiwemo kwenye masuala ya inteligensia.

Januari alisema Ofisi ya Makamu wa Rais na  Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira, wataratibu operesheni hiyo. 

Alisema kama tangazo lililotolewa Februari 20, mwaka huu, lilivyoonesha muda wa nyongeza unaweza kutolewa kwa wazalishaji halali ambao wataonyesha ushahidi wa kuelekea kuhamia kwenye teknolojia ya chupa na kwamba watahitaji muda mchache kufanya hivyo.

Januari alisema hadi sasa serikali imepokea maombi ya wazalishaji tisa, na wanasubiri leo kama kuna ambao walikidhi masharti au la.

Hata hivyo, alisema wamepokea malalamiko kwa wazalishaji wengi kwamba zoezi hilo limekuja ghafla na wengine wana malighafi na bidhaa kwenye maghala.

Alisema ukweli ni kwamba, serikali ilitoa taarifa Bungeni, kuanzia mwezi Mei, mwaka jana, na mara kadhaa baada ya hapo na rekodi zipo, kuhusu hatua hizi.

Aliwataka wananchi wote kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa  zoezi hilo la upigaji marufuku matumizi ya pombe zinazofungashwa katika vifungashio vya plastiki  kwa kutoa taarifa kwa vyombo husika ili wale wanaozalisha na kuuza au kuhifadhi waweze kuchukuliwa hatua stahiki.

Alisema zawadi itatolewa kwa watakaotoa taarifa zitakazowezesha kukamatwa kwa watakaokiuka zuio hili.

No comments:

Post a Comment