Wednesday, 1 March 2017

ASKOFU MOKIWA AFUTA KESI MAHAKAMANI


ALIYEKUWA Askofu Mkuu wa Kanisa  la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam, Dk. Valentino Mokiwa, ameamua kuiondoa kesi ya madai aliyokuwa  ameifungua katika Mahakama ya  Hakimu Mkazi Kisutu, dhidi ya Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk. Jacob Chimeledya.

Dk. Mokiwa  kupitia wakili wake, Mathew Kabunga kutoka Kampuni ya  M. B Kabunga and Co. Advocates,  aliwasilisha ombi hilo jana, mbele ya  Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, wakati shauri hilo namba 20 la mwaka  huu, lilipopelekwa kwa kutajwa.

Kutokana na hilo, Mahakama hiyo ilikubaliana na ombi hilo, hivyo  kuamua kuiondoa kesi hiyo, ambayo Dk. Mokiwa alifungua baada ya  kulazimishwa kustaafu kwa lazima  katika nafasi hiyo.

Dk. Mokiwa alifungua shauri hilo dhidi ya Dk. Chimeledya na Bodi ya  Wadhamini wa kanisa hilo, ambapo  pamoja na mambo mengine, alikuwa  akiiomba mahakama hiyo kutamka kwamba, kilichofanywa na kanisa  hakikuwa sahihi.

Jana, shauri hilo lilitajwa mbele ya Hakimu Simba, ambapo Wakili Kabunga aliieleza mahakama kuwa, amepewa maelekezo na mteja wake (Dk. Mokiwa) ya kuomba kuondoa kesi hiyo mahakamani.

"Nina hoja, baada ya kujadiliana kwa kina na mteja wangu na kwa makini, tunaomba kuondoa kesi mahakamani. Haya ndio maelekezo ya mteja wangu," aliomba.

Kwa upande wa Wakili Emmanuel Nkoma, anayemwakilisha Dk. Chimeledya na Bodi ya Wadhamini ya kanisa hilo, alidai hana pingamizi kuhusu ombi hilo.

"Hatuna pingamizi juu ya ombi hilo kwa sababu aliyeleta ndiye aliyeomba kuliondoa, lakini tayari wadaiwa wa kwanza na wa pili wameingia gharama kwa kuweka mawakili, hivyo tunaomba mahakama itoe maelekezo kwa usumbufu huu," aliomba.

Hakimu Simba alikubaliana na ombi la kuondoa kesi hiyo na kusema mdai awalipe gharama wadaiwa.

Baada ya Dk. Mokiwa kufungua shauri hilo, mawakili wa uongozi wa kanisa hilo, waliwasilisha pingamizi la awali kupinga shauri hilo.

Miongoni mwa hoja za kisheria zilizokuwa zimewasilishwa na wadaiwa, kupinga shauri hilo ni kwamba, mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo, hivyo kuomba kutupiliwa mbali.

Walidai kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kuingilia migogoro ya kidini kwa kuwa inatakiwa kutafutiwa ufumbuzi katika nyumba za imani.

Baada ya kuwasilisha pingamizi hilo la awali, Dk. Mokiwa kupitia wakili wake, Kabunga, aliwasilisha barua mahakamani hapo akiomba kuondolewa kwa shauri hilo, kwa madai kuwa kuna juhudi zinafanywa katika nyumba ya maaskofu kumaliza mgogoro huo.

Barua hiyo ilisomwa mahakamani hapo, Februari 23, mwaka huu, baada ya mawakili wa kanisa, Gabriel Masinga na Nkoma, kufika mbele ya Hakimu Simba.

Mawakili hao walimweleza hakimu huyo kuwa, wamepatiwa barua iliyokuwa ikiomba kurudishwa nyuma kwa siku ya kutajwa shauri hilo kwa kuwa wanataka kuwasilisha maombi ya kuondoa kesi hiyo.

Katika barua hiyo iliyoandikwa na Wakili Kabunga, ilieleza kuwa amepewa maelekezo na mteja wake ya kuondoa shauri hilo mahakamani kwa kuwa kuna juhudi zinafanywa za kutatua mgogoro huo katika nyumba ya maaskofu.

Ilieleza kuwa jitihada hizo haziwezi kufanyika bila ya kesi hiyo kuondolewa mahakamani.

Januari 7, mwaka huu, Dk. Chimeledya alimvua uaskofu mkuu Dk. Mokiwa, baada ya kukataa kustaafu kwa lazima, kutokana na tuhuma 10 zilizofunguliwa na walei takriban 28, wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam, zikiwemo za ufisadi wa mali za kanisa.

No comments:

Post a Comment