Wednesday 1 March 2017

NAPE ASEMA YUKO TAYARI KUJIUZULU


WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, amesema hahusiki kwa namna yoyote na tuhuma zilizoelekezwa kwake wiki kadhaa zilizopita, juu ya uhusiano kati yake na msanii wa maigizo nchini, Wema Sepetu.

Amesema kutokana na tuhuma zilizotolewa, anatoa uhuru kwa mtu yeyote mwenye ushahidi juu ya suala hilo na kwamba, yuko tayari kujiuzulu nafasi yake ya uwaziri kama itathibitishwa.

"Wema ni mdogo wangu kabisa, ukaribu uliokuwepo baina ya wazazi wetu yaani Mzee Sepetu na Mzee Nnauye, ulifanya tuwe kama ndugu, sasa inashangaza mtu anatoa maneno yasiyo na maana kabisa," alisema.

Nape alitoa kauli hiyo usiku wa kuamkia jana, alipokuwa akihojiwa kwenye kipindi cha televisheni cha Dakika 45, kinachorushwa na kituo cha ITV cha Dar es Salaam.

Nape alisema maneno yote (aliyoyaita ya kipuuzi), yalianza mara tu baada ya kumaliza kikao chake na wanahabari mjini Dodoma, ambapo pamoja na mambo mengine, alitoa ushauri kuwa katika sakata la tuhuma za matumizi ya dawa za kulevya, busara inahitajika kwenye namna ya kuwafikia wasanii ambao huitangaza nchi kwa kazi zao.

Alisema baada ya mkutano ule, alishangaa kuona baadhi ya watu wakimjia juu kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, kwa tuhuma zisizo za kweli, badala ya kumshauri kwa utaratibu mzuri kuhusiana na alichokizungumza.

"Ningeelezwa tu kuwa suala la 'brand' kwa wasanii sikulielezea vizuri ili kwenda sambamba na mapambano haya ya dawa za kulevya, lakini nilishangaa kilichotokea ndio maana nikaamua kukaa kimya kwanza," alisema.

Waziri Nape alisema anashukuru kwa hatua ya Rais Dk. John Magufuli, kumteua mtu, ambaye ana mamlaka kamili ya kushughulika na masuala ya dawa za kulevya, Kamishna Rogers Sianga.

"Sianga ni mtu makini, ndiyo maana alipopewa majina ya watuhumiwa, hakupenda yatangazwe kwenye vyombo vya habari, ndio utaratibu mzuri katika kushughulika na kesi za aina hiyo," alisema.

Aliongeza kuwa vita hiyo ni ya kila mtu kwenye nafasi yake, lakini ni vyema baada ya uteuzi wa Rais, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na maofisa wengine serikalini wakawa wasaidizi kwenye mapambano hayo.

Aliongeza kwa kusema kuwa, anampongeza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kwa jitihada zake za kuibua sakata hilo, lakini alisema kiongozi akishauriwa juu ya namna ya kufanya vizuri jambo, anatakiwa kufikiria na kuufuata.

"Ukifanya jambo, wenzio wakakushauri ili ufanye vizuri ni vyema ukafuata ushauri, lengo ni kuboresha," alisema.

Alifafanua kuwa wasanii wako chini ya uangalizi wake kisheria na kwamba, anao wajibu wa kuwatetea kwenye masuala mbalimbali, ndio sababu alijitokeza na kuzungumzia suala la kukamatwa na kuhojiwa kwa baadhi ya wasanii kuhusiana na tuhuma za dawa za kulevya.

Katika mkutano wake na wanahabari uliofanyika Februari 5, mwaka huu, mkoani Dodoma, Nape alisema wizara yake inaunga mkono mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa sababu kwa namna moja ama nyingine, yanadhoofisha nguvu kazi ya vijana.

Alisema: "Kama wizara, tunaunga mkono juhudi za mapambano hayo, lakini ni vizuri tukaangalia tunalifanya katika namna, ambayo inalinda haki ya mtuhumiwa ya kumpa 'room' ya kesho na keshokutwa kama ikithibitika kwamba hahusiki, bado atakuwa na heshima ambayo alikuwa ameitengeneza kwa miaka mingi."

Waziri Nape alisema watumiaji ni wengi, lakini wanaoonekana zaidi ni wale wenye majina makubwa, hivyo jambo la muhimu ni kulinda haki, na kwamba suala la utaratibu uliotumika kwa watuhumiwa wa dawa, anaiachia jamii iendelee kujadili na kuamua.

No comments:

Post a Comment